Zab 77

Zab 77

Matendo Makuu ya Mungu Yasimuliwa

1Nimpazie Mungu sauti yangu,

Naam, nimpazie Mungu, naye atanisikia.

2Siku ya taabu yangu nalimtafuta Bwana;[#Zab 50:15; Isa 26:9]

Mkono wangu ulinyoshwa usiku, haukulegea;

Nafsi yangu ilikataa kufarijika.

3Nilipotaka kumkumbuka Mungu nalifadhaika;

Nilipotaka kutafakari roho yangu ilizimia.

4Ulizishika kope za macho yangu zisifumbike;

Naliona mashaka nisiweze kunena.

5Nalifikiri habari za siku za kale,[#Kum 32:7; Zab 14:5; Isa 51:9]

Miaka ya zamani zilizopita.

6Nakumbuka wimbo wangu usiku,

Nawaza moyoni mwangu,

Roho yangu ikatafuta.

7Je! Bwana atatupa milele na milele?

Hatatenda fadhili tena kabisa?

8Rehema zake zimekoma hata milele?[#Isa 27:11; Yon 2:4; Hes 23:19; Yer 15:18; Rum 9:6]

Ahadi yake imekwisha hata vizazi vyote?

9Mungu amesahau fadhili zake?[#Isa 49:15]

Amezuia kwa hasira rehema zake?

10Nikasema, Ndio udhaifu wangu huo;[#Ayu 42:3; Zab 31:22; Yer 10:19]

Lakini nitaikumbuka miaka ya mkono wa kuume wake Aliye juu.

11Nitayakumbuka matendo ya BWANA;[#1 Nya 16:12; Zab 28:5; Isa 5:1]

Naam, nitayakumbuka maajabu yako ya kale.

12Pia nitaitafakari kazi yako yote;

Nitaziwaza habari za matendo yako.

13Ee Mungu, njia yako i katika utakatifu;[#Zab 73:17]

Ni nani aliye mungu mkuu kama Mungu?

14Wewe ndiwe Mungu ufanyaye maajabu;

Uliudhihirisha uweza wako kati ya mataifa.

15Kwa mkono wako umewakomboa watu wako,

Wana wa Yakobo na Yusufu.

16Ee Mungu, yale maji yalikuona,[#Kut 14:21; Yos 3:15,16]

Yale maji yalikuona, yakaogopa.

Vilindi vya maji navyo vikatetemeka,

17Mawingu yakamwaga maji.

Mbingu nazo zikatoa sauti,

Mishale yako nayo ikatapakaa.

18Sauti ya radi yako ikawa katika kisulisuli;

Umeme uliuangaza ulimwengu.

Nchi ilitetemeka na kutikisika;

19Njia yako ilikuwa katika bahari.[#Hab 3:15; Kut 14:28; Ayu 37:23]

Na mapito yako yalikuwa katika maji makuu;

Hatua zako hazikujulikana.

20Uliwaongoza watu wako kama kundi,[#Isa 63:11]

Kwa mkono wa Musa na Haruni.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania