The chat will start when you send the first message.
1Fadhili za BWANA nitaziimba milele;
Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
2Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
3Nimefanya agano na mteule wangu,[#Eze 34:23; Hes 3:5; Mdo 2:30; Ebr 7:21]
Nimemuapia Daudi, mtumishi wangu.
4Wazao wako nitawafanya imara milele,[#2 Sam 7:12-16; 1 Fal 9:5; 1 Nya 17:11-14; Zab 132:11; Isa 9:6,7; Lk 1:32; Mdo 2:30; Rum 1:3]
Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele.
5Ee BWANA, mbingu zitayasifu maajabu yako,
Uaminifu wako katika kusanyiko la watakatifu.
6Maana ni nani katika mbingu awezaye kulinganishwa na BWANA?
Ni nani afananaye na BWANA miongoni mwa malaika?
7Mungu huogopwa sana barazani pa watakatifu,
Ni wa kuhofiwa kuliko wote wanaomzunguka.
8BWANA, Mungu wa majeshi,
Ni nani aliye hodari kama Wewe, Ee YAHU?
Na uaminifu wako unakuzunguka.
9Wewe ndiwe ukitawalaye kiburi cha bahari.[#Ayu 38:11; Nah 1:4; Mt 8:26]
Mawimbi yake yainukapo wayatuliza Wewe.
10Ndiwe uliyemseta Rahabu akawa kama aliyeuawa,[#Isa 30:7]
Kwa mkono hodari umewatawanya wakuchukiao.
11Mbingu ni mali yako, nchi nayo ni mali yako,
Ulimwengu na vyote viujazavyo
Ndiwe uliyeupiga msingi wake.
12Kaskazini na kusini ndiwe uliyeziumba,[#Yos 19:22; 12:1; Amu 4:6]
Tabori na Hermoni hulifurahia jina lako.
13Mkono wako ni mkono wenye uweza,
Mkono wako una nguvu,
Mkono wako wa kuume umetukuka.
14Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chako,
Fadhili na kweli zahudhuria mbele za uso wako.
15Heri watu wale waijuao sauti ya shangwe,[#Hes 10:10]
Ee BWANA, huenenda katika nuru ya uso wako.
16Kwa jina lako hufurahi mchana kutwa,
Na kwa haki yako hutukuzwa.
17Maana fahari ya nguvu zao ni Wewe,
Na kwa radhi yako pembe yetu itatukuka.
18Maana ngao yetu ina BWANA,[#Hos 13:10]
Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.
19Ndipo ulipowaambia watakatifu wako kwa njozi,
Ukasema, nimempa aliye hodari msaada;
Nimemtukuza aliyechaguliwa miongoni mwa watu.
20Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,[#1 Sam 13:14; 16:12; Mdo 13:22]
Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
21Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
Na mkono wangu utamtia nguvu.
22Adui hatamwonea,
Wala mwana wa uovu hatamtesa.
23Bali nitawaponda watesi wake mbele yake,
Nitawapiga wanaomchukia.
24Uaminifu wangu na fadhili zangu atakuwa nazo,[#Zab 61:7]
Na kwa jina langu pembe yake itatukuka.
25Nitaweka mkono wake juu ya bahari,
Na mkono wake wa kuume juu ya mito.
26Yeye ataniita, Wewe baba yangu,[#2 Sam 7:14; 1 Nya 22:10; Yn 5:17]
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
27Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,[#Zab 2:7; Ufu 1:5]
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.
28Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
Na agano langu litafanyika amini kwake.
29Wazao wake nao nitawadumisha milele,[#Isa 9:7; Yer 33:17; Dan 7:14; Kum 11:21]
Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.
30Wanawe wakiiacha sheria yangu,[#2 Sam 7:14; Yer 9:13]
Wasiende katika hukumu zangu,
31Wakizihalifu amri zangu,
Wasiyashike maagizo yangu,
32Basi, nitawarudi makosa yao kwa fimbo,
Na uovu wao kwa mapigo.
33Lakini fadhili zangu sitamwondolea yeye,
Wala sitafanya uaminifu wangu kuwa uongo.
34Mimi sitalihalifu agano langu,
Sitalibadili neno lililotoka midomoni mwangu.
35Neno moja nimeliapa kwa utakatifu wangu,[#Zab 110:4; Ebr 6:13,17; Amo 4:2; 8:7]
Hakika sitamwambia Daudi uongo,
36Wazao wake watadumu milele,[#2 Sam 7:16; Lk 1:33; Yn 12:34]
Na kiti chake kitakuwa kama jua mbele zangu.
37Kitathibitika milele kama mwezi;[#Yer 31:35]
Shahidi aliye mbinguni mwaminifu.
38Walakini Wewe umemtupa na kumkataa,
Umemghadhibikia masihi wako.
39Umechukizwa na agano la mtumishi wako,[#Omb 5:16]
Umeinajisi taji yake na kuitupa chini.
40Umeyabomoa maboma yake yote,
Umezifanya ngome zake kuwa magofu.
41Wote wapitao njiani wanateka mali zake;
Amekuwa laumu kwa jirani zake;
42Umeutukuza mkono wa kuume wa watesi wake;
Umewafurahisha wote wanaomchukia.
43Pia umeurudisha nyuma ukali wa upanga wake;
Wala hukumsimamisha vitani.
44Umeikomesha fahari yake;
Kiti chake cha enzi umekitupa chini.
45Umezipunguza siku za ujana wake;
Umemvika aibu.
46Ee BWANA, hata lini? Utajificha hata milele?
Ghadhabu yako itawaka kama moto?
47Ukumbuke jinsi mimi nisivyo wa kudumu;[#Ayu 7:7]
Kwa ubatili gani umeiumba jamii ya wanadamu!
48Ni mwanamume gani atakayeishi asione mauti,[#Ebr 11:5]
Atakayejiokoa nafsi yake na mkono wa kuzimu?
49Bwana, zi wapi fadhili zako za kwanza,[#2 Sam 7:15; Isa 55:3]
Ulizomwapia Daudi kwa uaminifu wako?
50Ee Bwana, ukumbuke,
Wanavyosimangwa watumishi wako;
Jinsi ninavyostahimili kifuani mwangu
Masimango ya watu wengi.
51Ambayo adui zako wamesimanga, Ee BWANA,
Naam, wamezisimanga hatua za masihi wako.
52Na ahimidiwe BWANA milele. Amina na Amina.