Rum 10

Rum 10

1Ndugu zangu, nitakayo sana moyoni mwangu, na dua yangu nimwombayo Mungu, ni kwa ajili yao, ili waokolewe.[#Mdo 22:3]

2Kwa maana nawashuhudia kwamba wana juhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si katika maarifa.

3Kwa maana, wakiwa hawaijui haki ya Mungu, na wakitaka kuithibitisha haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.[#Rum 9:31,32]

4Kwa maana Kristo ni mwisho wa sheria, ili kila aaminiye ahesabiwe haki.[#Mt 5:17; Yn 3:18; Ebr 8:13]

Wokovu ni kwa Wote

5Kwa maana Musa aliandika juu ya haki itokayo kwa sheria, ya kuwa, Mtu afanyaye hiyo ataishi kwa hiyo.[#Law 18:5; Gal 3:12]

6Bali ile haki ipatikanayo kwa imani yanena hivi, Usiseme moyoni mwako, Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni? (Yaani, ni kumleta Kristo chini),[#Kum 30:12-14]

7au, Ni nani atakayeshuka kwenda kuzimuni? (Yaani, ni kumleta Kristo juu, kutoka kwa wafu.)

8Lakini yanenaje? Lile neno li karibu nawe, katika kinywa chako, na katika moyo wako; yaani, ni lile neno la imani tulihubirilo.[#Kum 30:14]

9Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.[#2 Kor 4:5]

10Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.

11Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika.[#Isa 28:16]

12Kwa maana hakuna tofauti ya Myahudi na Myunani; maana yeye yule ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao;[#Mdo 10:34; 15:9]

13kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana ataokoka.[#Yoe 2:32]

14Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri?

15Tena wahubirije, wasipopelekwa? Kama ilivyoandikwa, Ni mizuri kama nini miguu yao wahubirio habari ya mema![#Isa 52:7]

16Lakini si wote walioitii ile habari njema. Kwa maana Isaya asema, Bwana, ni nani aliyeziamini habari zetu?[#Isa 43:1]

17Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.[#Yn 17:20]

18Lakini nasema, Je! Wao hawakusikia? Naam, wamesikia,[#Zab 19:4]

Sauti yao imeenea duniani mwote,

Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.

19Lakini nasema, Je! Waisraeli hawakufahamu? Kwanza Musa anena,[#Kum 32:21]

Nitawatia wivu kwa watu ambao si taifa,

Kwa taifa lisilo na fahamu nitawaghadhibisha.

20Na Isaya anao ujasiri mwingi, asema,[#Isa 65:1]

Nalipatikana nao wasionitafuta,

Nalidhihirika kwao wasioniulizia.

21Lakini kwa Israeli asema, Mchana kutwa naliwanyoshea mikono watu wasiotii na wakaidi.[#Isa 65:2]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania