The chat will start when you send the first message.
1Basi, nauliza, Je! Mungu aliwasukumia mbali watu wake? Hasha! Kwa kuwa mimi nami ni Mwisraeli, mmoja wa wazao wa Ibrahimu, mtu wa kabila ya Benyamini.[#Flp 3:5; Zab 94:14; 1 Sam 12:22; Yer 31:37]
2Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,[#1 Fal 19:10,14]
3Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.[#1 Fal 19:10,14]
4Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.[#1 Fal 19:18]
5Basi ni vivi hivi wakati huu wa sasa, yako mabaki waliochaguliwa kwa neema.[#Rum 9:27]
6Lakini ikiwa ni kwa neema, haiwi kwa matendo tena, au hapo neema isingekuwa neema.[#Gal 3:18]
7Imekuwaje basi? Kitu kile ambacho Israeli alikuwa akikitafuta hakukipata; lakini wale waliochaguliwa walikipata, na wengine walitiwa uzito.[#Rum 9:31]
8Kama ilivyoandikwa, Mungu aliwapa roho ya usingizi, macho hata wasione, na masikio hata wasisikie, hata siku hii ya leo.[#Kum 29:4; Isa 29:10]
9Na Daudi asema,[#Zab 69:22-23; 35:8]
Meza yao na iwe tanzi na mtego,
Na kitu cha kuwakwaza, na malipo kwao;
10Macho yao yatiwe giza ili wasione,
Ukawainamishe mgongo wao siku zote.
11Basi nasema, Je! Wamejikwaa hata waanguke kabisa? Hasha! Lakini kwa kosa lao wokovu umewafikilia Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.[#Kum 32:21; Mdo 13:46; Rum 10:19]
12Basi, ikiwa kosa lao limekuwa utajiri wa ulimwengu, na upungufu wao umekuwa utajiri wa Mataifa, je! Si zaidi sana utimilifu wao?
13Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu,
14nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao.[#1 Tim 4:16]
15Maana ikiwa kutupwa kwao kumeleta upatanisho kwa ulimwengu, je! Kukubaliwa kwao kutakuwa nini kama si uhai baada ya kufa?
16Tena malimbuko yakiwa matakatifu, kadhalika na donge lote; na shina likiwa takatifu, matawi nayo kadhalika.[#Hes 15:17-21]
17Lakini iwapo matawi mengine yamekatwa, na wewe mzeituni mwitu ulipandikizwa kati yao, ukawa mshirika wa shina la mzeituni na unono wake,[#Efe 2:11-19]
18usijisifu juu ya matawi yale; au ikiwa wajisifu, si wewe ulichukuaye shina, bali ni shina likuchukualo wewe.[#Yn 4:22]
19Basi utasema, Matawi yale yalikatwa kusudi ili nipandikizwe mimi.
20Vema. Yalikatwa kwa kutokuamini kwao, na wewe wasimama kwa imani yako. Usijivune, bali uogope.[#Rum 12:16]
21Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, wala hatakuachia wewe.
22Tazama, basi, wema na ukali wa Mungu; kwa wale walioanguka, ukali, bali kwako wewe wema wa Mungu, ukikaa katika wema huo; kama sivyo, wewe nawe utakatiliwa mbali.[#Yn 15:2,4; Ebr 3:14]
23Na hao pia, wasipokaa katika kutokuamini kwao, watapandikizwa; kwa kuwa Mungu aweza kuwapandikiza tena.[#2 Kor 3:16]
24Kwa maana ikiwa wewe ulikatwa ukatolewa katika mzeituni, ulio mzeituni mwitu kwa asili yake, kisha ukapandikizwa, kinyume cha asili, katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana wale walio wa asili kuweza kupandikizwa katika mzeituni wao wenyewe?
25Kwa maana, ndugu zangu, sipendi msiijue siri hii, ili msijione kuwa wenye akili; ya kwamba kwa sehemu ugumu umewapata Israeli, mpaka utimilifu wa Mataifa uwasili.[#Lk 21:24; Yn 10:16; Rum 12:16]
26Hivyo Israeli wote wataokoka; kama ilivyoandikwa,[#Isa 59:20; 27:9; Mt 23:39; Zab 14:7]
Mwokozi atakuja kutoka Sayuni;
Atamtenga Yakobo na maasia yake.
27Na hili ndilo agano langu nao,[#Yer 31:33-34; Isa 27:9]
Nitakapowaondolea dhambi zao.
28Basi kwa habari ya Injili wamekuwa adui kwa ajili yenu; bali kwa habari ya kule kuchaguliwa wamekuwa wapenzi kwa ajili ya baba zetu.
29Kwa sababu karama za Mungu hazina majuto, wala mwito wake.
30Kwa maana kama ninyi zamani mlivyomwasi Mungu, lakini sasa mmepata rehema kwa kuasi kwao;
31kadhalika na hao wameasi sasa, ili kwa kupata rehema kwenu wao nao wapate rehema.
32Maana Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote.[#Gal 3:22; 1 Tim 2:4]
33Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hukumu zake hazichunguziki, wala njia zake hazitafutikani![#Isa 55:8; 45:15; Rum 9:23; 10:12]
34Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani aliyekuwa mshauri wake?[#Isa 40:13; Ayu 15:8; Yer 23:18; 1 Kor 2:16]
35Au ni nani aliyempa yeye kitu kwanza, naye atalipwa tena?[#Ayu 41:11]
36Kwa kuwa vitu vyote vyatoka kwake, viko kwa uweza wake, tena vinarejea kwake. Utukufu una yeye milele. Amina.[#1 Kor 8:6]