Rum 12

Rum 12

Maisha Mapya katika Kristo

1Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.[#Rum 6:11,13; 1 Pet 2:5; Yn 4:24]

2Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.[#Efe 4:23; 5:10,17; Rum 1:28; Gal 1:4]

3Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.[#1 Kor 12:11; Efe 4:7]

4Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;[#1 Kor 12:12]

5Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.[#1 Kor 12:27; Efe 4:25]

6Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;[#1 Kor 12:4-11]

7ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;[#1 Pet 4:10,11]

8mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.[#Mt 6:3; 2 Kor 8:2; 9:7]

Sifa za Mkristo

9Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.[#1 Pet 1:22; 1 Tim 1:5; Amo 5:15]

10Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;[#2 Pet 1:7; Flp 2:3]

11kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;[#Ufu 3:15; Mdo 18:25]

12kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;[#1 The 5:17]

13kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.[#Ebr 13:2]

14Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.[#Mt 5:44; Lk 6:28; Mdo 7:59; 1 Kor 4:12]

15Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.[#Zab 35:13]

16Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.[#Mit 3:7; Rum 15:5; 11:20]

17Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.[#Isa 5:21; 1 The 5:15]

18Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.[#Mk 9:50; Ebr 12:14]

19Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.[#Kum 32:35; Law 19:18; Mt 5:39; 2 The 1:6,7; Rum 13:4; Ebr 10:30]

20Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.[#Mit 25:21-22; Mt 5:44]

21Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania