Zek 10

Zek 10

Matengenezo ya Yuda na Israeli

1Mwombeni BWANA mvua wakati wa masika, naam, BWANA afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.[#Yer 14:22; Yoe 2:23]

2Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.[#Mt 9:36; Mk 6:34]

3Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana BWANA wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.[#Kut 4:31; Rut 1:6; Sef 2:7; Lk 1:68; 1 Pet 2:12]

4Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja.[#Isa 22:23]

5Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu BWANA yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.

6Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni BWANA, Mungu wao, nami nitawasikia.

7Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia BWANA.

8Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka.[#Isa 5:26]

9Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.

10Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana.[#Rum 11:25; Kut 14:26,27; Isa 49:20]

11Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.[#Eze 30:13]

12Nami nitawatia nguvu katika BWANA; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema BWANA.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania