Zek 11

Zek 11

1Ifungue milango yako, Ee Lebanoni,

Ili moto uiteketeze mierezi yako.

2Piga yowe, msunobari, maana mwerezi umeanguka,

Kwa sababu miti iliyo mizuri imeharibika;

Pigeni yowe, enyi mialoni ya Bashani,

Kwa maana msitu wenye nguvu umeangamia.

3Sauti ya wachungaji, ya uchungu mwingi!

Kwa maana utukufu wao umeharibika;

Sauti ya ngurumo ya wana-simba!

Kwa maana kiburi cha Yordani kimeharibika.

Aina mbili za Wachungaji

4BWANA, Mungu wangu, alisema hivi, Lilishe kundi la machinjo,

5ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe BWANA, kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.[#Kum 29:19; Yer 2:3; Hos 12:8; Yn 16:2; 1 Tim 6:9; 2 Pet 2:3]

6Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema BWANA; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao.

7Basi nikalilisha kundi la machinjo, kweli kondoo waliokuwa wanyonge kabisa.[#Sef 3:12; Mt 11:5]

Kisha nikajipatia fimbo mbili; nami nikaiita ya kwanza, Neema, na ya pili nikaiita, Vifungo; nikalilisha kundi lile.

8Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia.[#Hos 5:7]

9Ndipo nikasema, Sitawalisheni; afaye na afe; atakayekatiliwa mbali na akatiliwe mbali; nao waliosalia, kila mmoja na ale nyama ya mwili wa mwenziwe.[#Yer 15:2]

10Nikaitwaa hiyo fimbo yangu, iitwayo Neema, nikaikata vipande viwili, ili nipate kulivunja agano langu nililolifanya na watu wa kabila zote.

11Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la BWANA.

12Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu.[#Kut 21:32; Mt 26:15]

13Kisha BWANA akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya BWANA.[#Mt 27:9-10]

14Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Vifungo, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli.

15BWANA akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu.[#Eze 34:2]

16Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao.

17Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.[#Yer 23:1; Yn 10:12; Mik 3:6]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania