The chat will start when you send the first message.
1Ole wake yeye aliyeasi na kutiwa unajisi, mji wa udhalimu!
2Hakuitii sauti; hakukubali kurudiwa; hakumwamini BWANA; hakumkaribia Mungu wake.[#Yer 22:21; 5:3]
3Wakuu wake walio ndani yake ni simba wangurumao; makadhi wake ni mbwa-mwitu wa jioni; hawasazi kitu cho chote hata siku ya pili.
4Manabii wake ni watu hafifu, wadanganyifu; makuhani wake wamepatia unajisi patakatifu, wameifanyia sheria udhalimu.[#Yer 23:11; Eze 22:26]
5BWANA kati yake ni mwenye haki; hatatenda uovu; kila asubuhi hudhihirisha hukumu yake, wala hakomi; bali mtu asiye haki hajui kuona haya.[#Kum 32:4; Zab 99:3,4]
6Nimekatilia mbali mataifa, buruji zao zina ukiwa; nimeziharibu njia kuu zao, hata hapana mmoja apitaye; miji yao imeangamizwa; hamna mtu hata mmoja, wala hapana akaaye huko.
7Nalisema, Hakika utaniogopa, utakubali kurudiwa; ili yasikatiliwe mbali makao yake, sawasawa ya yote niliyoagiza katika habari zake; lakini waliondoka mapema na kuyaharibu matendo yao yote.[#Mwa 6:12]
8Basi ningojeni, asema BWANA, hata siku ile nitakapoondoka kuteka mateka; maana nimeazimia kuwakusanya mataifa, ili nizikutanishe falme, nipate kuwamwagia ghadhabu yangu; naam, ukali wote wa hasira yangu; kwa maana dunia yote itateketezwa kwa moto wa wivu wangu.[#Mit 20:22; Yoe 3:2]
9Maana hapo ndipo nitakapowarudishia mataifa lugha iliyo safi, wapate kuliitia jina la BWANA, wamtumikie kwa nia moja.
10Maana toka nchi iliyo mbali na mito ya Kushi, waniombao dua, yaani, binti za watu wangu waliotawanyika, wataleta matoleo yangu.[#Zab 68:31; Mal 1:11; Mdo 8:27]
11Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu.[#Mt 3:9]
12Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la BWANA.[#Isa 14:32; 57:15; Mt 5:3; Lk 6:20]
13Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya.[#Ufu 14:5]
14Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli;[#Zab 14:7]
Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu.
15BWANA ameziondoa hukumu zako,[#Yn 1:49; Eze 48:35; Ufu 21:3]
Amemtupa nje adui yako;
Mfalme wa Israeli, naam, yeye BWANA, yu katikati yako;
Hutaogopa uovu tena.
16Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa,[#Isa 35:3]
Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee.
17BWANA, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa;
Atakushangilia kwa furaha kuu,
Atakutuliza katika upendo wake,
Atakufurahia kwa kuimba.
18Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao.[#Omb 2:6]
19Tazama, wakati huo nitawapatiliza watu wote wanaokutesa; nami nitamponya yeye achechemeaye, nami nitamkusanya yeye aliyefukuzwa; nami nitawafanya kuwa sifa na jina, hao ambao fedheha yao ilikuwa katika dunia yote.
20Wakati huo nitawaingizeni, na wakati huo nitawakusanya; kwa maana nitawafanya ninyi kuwa sifa na jina, miongoni mwa watu wote wa dunia, nitakapowarudisha wafungwa wenu mbele ya macho yenu, asema BWANA.[#Zab 22:27]