1 Wakorintho 11

1 Wakorintho 11

1MWE wafuasi wangu kama mimi nilivyo mfuasi wa Kristo.

2Tena nawasifu, ndugu, kwa sababu mmenikumbuka katika mambo yote, nanyi mmeyashika yale niliyowatolea vile vile kama nilivyowatolea.

3Lakini nataka mjue ya kuwa kichwa cha killa mwanamume ni Kristo na kichwa cha mwanamke ni mwanamume, na kichwa cha Kristo ni Mungu.

4Killa mwanamume, asalipo, au atoapo unabii, nae ana kitu kichwani, yuaibisha kichwa chake.

5Bali killa mwanamke asalipo, au atoapo unabii, bila kufunika kichwa chake, yuaibisha kichwa chake; kwa maana yu sawa sawa nae aliyekata nywele zake.

6Maana mwanamke asipofunikwa na anyoe. Au ikiwa ni unyonge mwanamke akate nywele zake au kunyoa, na afunikwe.

7Kwa maana haimpasi mwanamume kufunikwa kichwa, kwa sababu ni mfano na utukufu wa Mungu. Lakini mwanake ni utukufu wa mwanamume.

8Maana mwanamume hakutoka katika mwanamke, bali mwanamke katika mwanamume.

9Wala mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, bali mwanamke kwa ajili ya mwanamume.

10Kwa hiyo imempasa mwanamke awe na dalili ya kumilikiwa kichwani pake, kwa ajili ya malaika.

11Illakini mwanamume hawi pasipo mwanamke, wala mwanamke pasipo mwanamume, katika Bwana.

12Maana kama vile mwanamke alitoka katika mwanamume, vivyo hivyo mwanamume nae huzaliwa na mwanamke; na vitu vyote asili yake hutoka kwa Mungu.

13Hukumuni ninyi wenyewe katika nafsi zenu. Je! inapendeza mwanamke amwombe Mungu asipofunikwa kichwa chake?

14Je! sharia ya asili yenyewe haiwafundishi ya kwamba mwanamume akiwa na nywele ndefu ni aibu kwake;

15lakini mwanamke akiwa na nywele ndefu ni ntukufu kwake. Kwa sababu amepewa zile nywele ndefu illi ziwe badala ya mavazi.

16Lakini mtu aliye yote, akitaka kuleta fitina, sisi hatuna desturi kama hiyo, wala makanisa ya Mungu.

17Katika kuagiza hayo, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa khasara;

18kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; na nussu kidogo nasadiki:

19kwa maana lazima kuwapo uzushi kwenu, illi waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu.

20Bassi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana;

21kwa maana killa mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hatta huyu ana njaa, na huyu amelewa.

22Je! hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau Kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha wasio na kitu? Niwaambieni? niwasifu kwa haya? Siwasifu.

23Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowakhubirini, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate,

24na akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangii.

25Vivi hivi nacho kikombe baada ya kula, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu: fanyeni liivi killa mnywapo, kwa ukumbusho wangu.

26Maana killa mwulapo mkate huu na kunywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hatta ajapo.

27Bassi killa aulae mkate huu, au kunywea kikombe hiki, asivyostahili, atakuwa amejipatia khatiya kwa ajili ya mwili na damu ya Bwana.

28Lakini mtu ajihoji nafsi yake, ndivyo aule mkate, na kukinywea kikombe.

29Maana alae na kunywa asivyostahili, hula na hunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua mwili wa Bwana.

30Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala.

31Lakini tukijihukumu vema nafsi zetu, tusingehukumiwa.

32Tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, tusipate kupasishwa adhabu pamoja na dunia.

33Bassi, ndugu zangu, mkutanikapo mpate kula, mngojane;

34mtu akiwa na njaa, ale nyumbani; msipate kukutanika kwa hukumu. Nayo yaliyosalia nijapo nitayatengeneza.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania