1 Wakorintho 6

1 Wakorintho 6

1JE! mtu wa kwenu akiwa na neno juu ya mwenzake athubutu kuhukumiwa mbele ya wasio haki wala si mbele ya watakatifu?

2Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! hamstahili kuhukumu hukumu zilizo ndogo?

3Hamjui ya kuwa tutawahukumu malaika, bassi si zaidi sana mambo ya maisha haya?

4Bassi, mkiwa ita mahali yanapohukumiwa mambo ya maisha haya, wekeni hao waliohesabiwa kuwa si kitu katika kanisa.

5Nasema haya nipate kuwatahayarisheni. Je! ndivyo hivyo, kwamba kwenu hakuna hatta mtu mmoja mwenye hekima, awezae kukata maneno ya ndugu zake?

6Bali mwashitakiana, ndugu na ndugu, tena mbele yao wasioamini.

7Bassi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyangʼanywa mali zenu?

8Bali ninyi mwadhulumu watu na kunyangʼanya mali zao; naam, za ndugu zenu.

9Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike. Waasharati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wa kike, wala wafira,

10wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyangʼanyi.

11Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hizi; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa kuwa na haki katika jina la Bwana Yesu na katika Roho ya Mungu wetu.

12Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote.

13Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu ataharibu vyote viwili, tumbo na vyakula. Na mwili si kwa zina, hali ni kwa Bwana, nae Bwana ni kwa mwili.

14Na Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua na sisi kwa uweza wake.

15Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Bassi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaha? Hasha!

16Hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja nae? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.

17Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja nae.

18Ikimbieni zina. Killa dhambi aifanyayo mwana Adamu ni nje ya mwili wake; bali yeye afanyae zina hufanya dhambi juu ya mwili wake mwenyewe.

19Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu ya Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyopewa na Mungu? Na ninyi si mali yenu wenyewe;

20Maana mlinunuliwa kwa thamani. Kwa kuwa ni hivyo, mtukuzeni Mungu kwa mwili wenu, na kwa roho yenu, ambayo ni mali ya Mungu.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania