The chat will start when you send the first message.
1NA kwa khabari ya vitu, vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; Twajua ya kuwa sisi sote tuna elimu. Elimu huleta majivuno, bali upendo hujenga.
2Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.
3Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejuliwa nae.
4Bassi, kwa khabari ya kuvila vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu; twajua ya kuwa sanamu si kitu katika ulimwengu, na ya kuwa hapana Mungu mwingine illa mmoja tu.
5Kwa maana ijapokuwa wako waitwao waungu, ikiwa mbinguni au duniani, kama vile wako waungu wengi na bwana wengi;
6illakini kwetu sisi yuko Mungu mmoja tu, aliye Baba, ambae vitu vyote vimetokana nae, na sisi twarejea kwake; na yuko Bwana mmoja Yesu Kristo, ambae kwa sabiki yake vitu vyote vimekuwa, na sisi kwa sabiki yake.
7Bali elimu hii haimo ndani ya watu wote; illa wengine kwa kuizoelea ile sanamu hatta sasa hula kama ni kitu kilichotolewa sadaka kwa sanamu; na dhamiri yao, kwa kuwa dhaifu, hunajisika.
8Lakini chakula hakituleti mbele ya Mungu; maana, tukila, hatuongezewi kitu, na tusipokula hatupunguziwi kitu.
9Lakini angalieni huu uwezo wenu usije ukawakwaze wale walio dhaifu.
10Kwa maana, mtu akikuona wewe uliye na elimu, umeketi chakulani ndani ya hekalu ya sanamu, je! dhamiri yake mtu huyu, kwa kuwa yu dhaifu, haitathubutika hatta ale vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu?
11Na yule aliye dhaifu aangamizwa kwa elimu yako, nae ni ndugu ambae Kristo alikufa kwa ajili yake.
12Na hivyo, mkiwatenda dhambi ndugu zenu na kuwajeruhi dhamiri zao zilizo dhaifu, mnamtenda dhambi Kristo.
13Kwa hiyo, chakula kikimkosesha ndugu yangu, sitakula nyama hatta milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.