The chat will start when you send the first message.
1PAOLO, mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Timothieo ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililo katika Korintho, pamoja na watakatifu wote walio katika inchi yote ya Akaia:
2Neema iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
4atufarijiye katika shidda zetu zote illi tupate kuwafariji wale walio katika shidda za namna zote, kwa faraja tunazofarijiwa na Mungu.
5Kwa kuwa vile vile kama mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
6Lakini ikiwa sisi tu katika shidda, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokofu wenu, ufanyao kazi yake kwa kuvumilia mateso yale yale tuteswayo na sisi: au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokofu wenu.
7Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa vile vile kama mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo m washiriki wa zile faraja.
8Maana hatupendi, ndugu, msijue khabari ya shidda ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hatta tukakata tamaa ya kuishi.
9Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu, illi tusijitumainie nafsi zetu, hali Mungu, awafufuae wafu, aliyetuokoa sisi na mauti kuu namna ile, tena ataokoa;
10ambae tumemtumainia kwamba atazidi kutuokoa;
11ninyi nanyi mkisaidiana kwa ajili yetu katika kuomba, illi, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa kazi ya watu wengi, watu wengi watoe mashukuru kwa ajili yetu.
12Hwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa unyofu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu, si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu, tulienenda katika dunia, na khassa kwenu ninyi.
13Maana hatuwaandikii ninyi neno, illa yale msomayo, au kuyakiri; nami nataraja ya kuwa mtayakiri hatta mwisho;
14vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana Yesu.
15Na nikiwa na timiaini hilo nalitaka kwenda kwenu hapo kwanza, illi mpate karama ya pili;
16na kupita kwenu na kuendelea hatta Umakedoni; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Yahudi.
17Bassi, nilipokusudia haya nalitumia kigeugeu; au niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili illi iwe hivi kwangu, kusema ndiyo, ndiyo, na siyo, siyo?
18Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu halikuwa ndiyo na siyo.
19Maana Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, aliyekhubiriwa na sisi kati yenu, na mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa ndiyo na siyo; bali katika yeye ndiyo imepata kuwako.
20Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni ndiyo; na katika yeye ni Amin, Mungu apate kutukuzwa kwa kazi yetu.
21Bassi Yeye atufanyae imara pamoja na ninyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu,
22nae ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.
23Lakini mimi namwitia Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijaenda Korintho.
24Si kwamba tunatawala imani yenu; hali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana mnasimama kwa imani.