The chat will start when you send the first message.
1INGEKUWA kheri kama mngenisamehe kidogo upumbavu wangu; naam, kanisameheni.
2Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; maana naliwaposea mume mmoja, nimletee Kristo bikira safi.
3Lakini naogopa; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikara zenu, mkauacha unyofu wenu kwa Kristo.
4Maana yeye ajae akikhubiri Yesu mwingine ambae sisi hatukumkhubiri, au mkipokea Roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumilia nae.
5Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa kitu walicho nacho mitume walio wakuu.
6Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiojua kunena, illakini hii si hali yangu katika ilmu; lakini katika killa neno tumedhihirishwa kwenu.
7Je! nalifanya dhambi kwa kujinyenyekea illi ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwakhubiri Injili ya Kristo bila ujira?
8Naliwanyangʼanya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu niwakhudumie ninyi.
9Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana ndugu walipokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; na katika mambo yote nalijilinda nafsi yangu nisiwalemee hatta kidogo; tena nitajilinda.
10Kama vile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hapana mtu atakaenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya.
11Kwa nini? kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.
12Lakini nifanyalo nitalifunya, illi niwapinge watafutao nafasi wasipate nafasi; illi katika neno hilo wajisifulo waonekane kuwa kama sisi.
13Maana hawo ni mitume wa uwongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume ya Kristo.
14Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.
15Bassi si neno kubwa wakhudumu wake nao wakijigeuza wawe mfano wa wakhudumu wa haki. Mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.
16Nasema tena mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; mimi nami nipate kujisifu kidogo.
17Nisemalo silisemi agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu.
18Iwapo wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili mimi nami nitajisifu.
19Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnavumilia na wajinga kwa furaha.
20Maana mwavumilia na mtu akiwatieni utumwani, akiwameza, akiwateka, akijikuza, akiwapiga usoni.
21Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Illakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), na mimi niuao ujasiri.
22Wao Waebrania? Na mimi. Wao Waisraeli? Na mimi. Wao uzao wa Ibrahimu? Na mimi.
23Wao wakhudumu wa Kristo? (nanena kiwazimu), mimi zaidi; kwa kazi kuzidi sana; kwa mapigo kupita kiasi; kwa vifungo kuzidi sana; kwa mauti marra nyingi.
24Kwa Wayahudi marra tano nalipata mapigo arubaini kasoro moja.
25Marra tatu nalipigwa bakora; marra moja nalipigwa mawe; marra tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26kwa kusafiri marra nyingi; khatari za mito; khatari za wanyangʼanyi; khatari kwa jamaa; khatari kwa mataifa; khatari za mijini; khatari za jangwani; khatari za baharini; khatari kwa ndugu za uwongo;
27kwa kazi na kusumbuka; kwa kukesha marra nyingi; kwa njaa na kiu; kwa kufunga marra nyingi; kwa baridi na kuwa uchi.
28Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo killa siku, ndio maangalizi ya makanisa yote.
29Nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu na mimi? Nani aliyechukizwa na mimi nisiwake?
30Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.
31Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliye mtukufu hatta milele, ajua va kuwa sisemi nwongo.
32Katika Dameski liwali wa Areta mfalme alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, akitaka kunikamata;
33nikashushwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka na mikono yake.