Matendo 23

Matendo 23

1PAOLO akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa nia safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hatta leo hivi.

2Kuhani akawaamuru wale waliosimama karibu kumpiga kinywa chake.

3Ndipo Paolo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sharia, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sharia?

4Wale waliosimama karibu wakasema, Je! unamtukana kuhani mkuu wa Mungu?

5Paolo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni kuhani mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.

6Paolo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Mafarisayo, na sehemu ya pili Masadukayo, akapaaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana wa Farisayo: mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.

7Alipokwisha kunena hayo palikuwa na fitina beina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukagawanyika.

8Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika na roho: bali Mafarisayo hukiri yote mawili.

9Pakawa makelele mengi. Waandishi wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakamtetea, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema nae tusishindane na Mungu.

10Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paolo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumpokonya mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.

11Usiku ule Bwana akasimama karibu nae, akasema, Uwe na moyo mkuu, Paolo; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia khabari zangu Yerusalemi, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi.

12Kulipopambazuka, baadhi ya Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo wakisema. Hatuli wala hatunywi hatta tutakapokwisha kumwua Paolo.

13Na hao walioapiana hivyo walipata watu arubaini.

14Nao wakaenda kwa makuhani wakuu na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo, tusionje kitu hatta tutakapomwua Paolo.

15Bassi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua khabari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.

16Mjomba wake Paolo akasikia khabari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paolo khabari.

17Paolo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu.

18Bassi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paolo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.

19Yule jemadari akamshika mkono akaenda nae kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?

20Akasema, Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paolo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata khabari zake kwa usahihi zaidi. Bassi wewe usikubali;

21kwa maana watu zaidi ya arubaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hatta watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako.

22Bassi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awae yote ya kwamba umeniarifu haya.

23Akaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari miateen kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabaini, na wenye mikuki miateen, panapo saa tatu ya usiku.

24Akawaambia kuweka nyama tayari wampandishe Paolo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.

25Akaandika barua, kwa nanma hii:

26Klaudio Lusia kwa liwali il aziz Feliki salamu!

27Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, akawa karibu kuuawa nao, nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata khabari ya kuwa yeye ni Mrumi.

28Na nikitaka kuijua sababu hatta wakamshitaki, nikamleta chini nikamweka mbele ya baraza:

29nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sharia yao, wala hakushitakiwa neno lo lote la kustahili kuuawa wala kufungwa.

30Hatta nilipopewa khabari kwamba patakuwa na vitimbi juu ya mtu huyu, marra nikampeleka kwako, nikawaagiza na wale walioshitaki, wanene khabari zake mbele yako. Salamu.

31Bassi, wale askari wakamchukua Paolo kamu walivyoamriwa, wakampeleka hatta Antipatri usiku:

32hatta assubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja nae, nao wakarudi zao ngomeni.

33Na wale walipofika Kaisaria, wakampa liwali ile barua, wakamweka Paolo mbele yake. Nae alipokwislia kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa wilaya gani?

34Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia, akasema,

35Nitakusikia maneno yako watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika praitorio ya Herode.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania