Ufunuo 10

Ufunuo 10

1NIKAONA malaika mwingine hodari akishuka kutoka mbinguni, amevikwa wingu; na upinde wa mvua juu ya kichwa chake: na uso wake kama jua, na miguu yake kama nguzo za moto.

2Na katika mkono wake alikuwa na kitabu kidogo kimefunuliwa. Akaweka mguu wake wa kuume juu ya bahari, na wa kushoto juu ya inchi,

3Akalia kwa sauti kuu, kama simba angurumavyo. Na alipolia ugurumo saba zikatoa sauti zao.

4Hatta ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika.

5Na yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya inchi akainua mkono wake kuelekea mbinguni,

6akaapa kwa yeye aliye bayi hatta milele na milele, aliyeziumba mbingu na vitu vilivyomo, na inchi na vitu vilivyomo, na bahari na vitu vilivyomo, ya kwamba hapatakuwa na muhulla baada ya haya,

7isipokuwa katika siku zile za malaika wa saba, atakapokuwa tayari kupiga: hapo ndipo siri ya Mungu itakapotimizwa, kama alivyowakhubiri watumishi wake manabii.

8Na sauti ile niliyoisikia kutoka mbinguni ilinena nami tena, ikisema, Enenda, kitwae kile kitabu kidogo kilichofunuliwa katika mkono wa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya inchi.

9Nikamwendea malaika yule nikamwambia, Nipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali.

10Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali katika kinywa changu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu.

11Akaniambia, Imekupasa kutoa unabii tena juu ya watu na taifa na lugha na wafalme wengi.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania