The chat will start when you send the first message.
1AKANIONYESHA mto wa maji ya uzima, wenye kungʼaa kama bilauri, ukitoka katika kiti cha enzi cha Mungu, na cha Mwana kondoo.
2Kati ya njia kuu yake na ule mto, upande huu na upande huu, mti wa uzima, uzaao matunda thenashara, mwenye kutoa matunda yake killa mwezi, na majani ya mti huo ya kuwaponya mataifa.
3Wala hapatakuwa laana yo yote tena. Na kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana kondoo kitakuwa ndani yake.
4Na watumishi wake watamtumikia; nao watamwona uso wake, na jina lake katika vipaji vya nyuso zao.
5Wala hapatakuwa usiku huko; wala hawana haja ya taa wala ya nuru ya jua; kwa kuwa Bwana Mungu awatia nuru, nao watamiliki milele hatta milele.
6Akaniambia, Haya ni maneno ya uaminifu na ya kweli. Na Bwana Mungu wa manabii watakatifu alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake mambo ambayo hayana buddi kuwa upesi.
7Tazama, naja upesi; yu kheri yeye ayashikae maneno ya unabii wa kitabu hiki.
8Na mimi Yohana ndimi niliye mwenye kuona haya na kuyasikia. Na niliposikia na kuyaona nalianguka nisujudu mbele ya miguu ya malaika yule mwenye kunionyesha haya.
9Akaniambia, Angalia, usifanye hivyo; mimi mjoli wako, na wa ndugu zako manabii na wa wale washikao maneno ya kitabu hiki. Msujuduni Mungu.
10Akaniambia, Msiyatie muhuri maneno ya unabii wa kitabu hiki, kwa maana wakati huo umekaribia.
11Mwenye kudhulumu na atende dhuluma tena; na mwenye uchafu na awe mchafu tena, na mwenye haki na afanye haki tena, na mtakatifu na atakaswe tena.
12Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami kumlipa killa mtu kama itakavyokuwa kazi yake.
13Mimi Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa mwisho.
14Wa kheri wazifuazo nguo zao, wawe na amri kuuendea mti wa uzima, na kuuingia mji kwa milango yake.
15Bali nje wako mbwa na wachawi na wazinzi na wauaji nao waabuduo sanamu, na killa mtu apendae uwongo na kuufanya.
16Mimi Yesu nalimtuma malaika wangu kuwashuhudia ninyi mambo hayo katika makanisa. Mimi ndimi niliye Shina na Mzao wa Daud, ile nyota yenye kungʼaa ya assubuhi.
17Na Roho na Bibi arusi wasema, Njoo. Nae asikiae aseme, Njoo. Nae aliye na kiu, na aje: na apendae ayatwae maji ya uzima burre.
18Namshuhudia killa mtu ayasikiae maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu aliye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19Na mtu aliye yote akiondoa baadhi ya maaeno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika kile kitabu cha uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao khabari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.
20Yeye mwenye kuyashuhudia haya asema, Naam; Naja upesi. Amin: na uje Bwana Yesu.
21Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote. Amin.