Ufunuo 8

Ufunuo 8

1HATTA alipofungua muhuri ya saba kukawa kimya mbinguni kama muda wa nussu ya saa.

2Nikawaona malaika saba wasimamao mbele za Mungu, wakapewa baragumu saba.

3Na malaika mwingine akaja akasimama mbele ya madhbahu, mwenye cheteso cha dhahabu, akapewa manukato mengi illi ayatie pamoja na sala za watakatifu juu ya madhbahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.

4Na moshi wa yale manukato ukapanda pamoja na sala za watakatifu, katika mkono wa malaika, mbele za Mungu.

5Malaika akakitwaa cheteso akakijaza moto wa madhbahu, akautupa juu ya inchi, kukawa sauti na radi na umeme na tetemeko la inchi.

6Na wale malaika saba wenye baragumu saba wakajifanya tayari illi wazipige.

7Malaika wa kwanza akapiga baragumu, kukawa mvua ya mawe na moto vilivyotangamana na damu, vikatupwa juu ya inchi: thuluth ya miti ikateketea, majani mabichi yote yakateketea.

8Malaika wa pili akapiga baragumu, na kitu, mfano wa mlima mkubwa uwakao moto, kikatupwa katika bahari, thuluth ya bahari ikawa damu.

9Wakafa thuluth ya viumbe vilivyo katika bahari, vyenye uhayi: thuluth ya merikebu zikaharibiwa.

10Malaika wa tatu akapiga baragumu, nyota kubwa ikaanguka kutoka mbinguni, iliyokuwa ikiwaka kama taa, ikaanguka juu ya thuluth ya mito, na juu ya chemchemi za maji.

11Na jina lake, ile nyota yaitwa Absintho, thuluth ya maji ikawa absintho, na wana Adamu wengi wakafa kwa maji hayo kwa kuwa yalitiwa uchungu.

12Malaika wa nne akapiga baragumu, thuluth ya jua ikapigwa, na thuluth ya mwezi, na thuluth ya nyota, illi ile thuluth itiwe giza, mchana usiangaze thuluth yake wala usiku vivyo hivyo.

13Nikaona, nikasikia tai akiruka kati kati ya mbingu, akisema kwa sauti kuu, Ole, ole, ole wao wakaao juu ya inchi, kwa sababu ya sauti zisaliazo za baragumu ya malaika watatu, walio tayari kupiga.

Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.
Published by: Bible Society of Tanzania