The chat will start when you send the first message.
1TUSEME nini bass? Tudumu katika dhambi illi neema iwe nyingi zaidi?
2Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?
3Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Yesu Kristo, twalibatizwa katika mauti yake?
4Bassi tulizikwa pamoja nae kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tutembee katika upya wa uzima.
5Kwa maana kama tulivyounganika nae katika mfano wa mauti yake, kadhalika kwa mfano wa kufufuka kwake;
6tukijua haya, ya kuwa mtu wetu wa kale alisulibishwa pamoja nae, illi mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;
7kwa maana yeye aliyekufa ameachiliwa akawa mbali ya dhambi.
8Lakini tukiwa twalikufa pamoja na Kristo, twaamini ya kuwa tutaishi pamoja nae,
9tukijua ya kuwa Kristo akiisha kufufuka hafi tena, mauti haimtawali tena.
10Kwa kule kufa kwake, aliifia dhambi marra moja; lakini kule kuishi kwake, amwishia Mungu.
11Vivyo hivyo na ninyi jihesabuni kuwa wafu kwa dhambi, na wahayi kwa Mungu katika Kristo Yesu.
12Bassi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti hatta mkazitii tamaa zake;
13wala msitoe viungo vyenu kuwa silaha ya dhulumu kwa dhambi; bali jitoeni nafsi zenu sadaka kwa Mungu kama walio hayi baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki.
14Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi, kwa sababu hamwi chini ya sharia, hali chini ya neema.
15Ni nini bassi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi chini ya sharia bali chini ya neema? Hasha!
16Hamjui ya kuwa kwake yeye ambae mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake na kumtumikia, m watumwa wake yule mmtiiye, ikiwa utumishi wa dhambi uletao mauti, au utumishi wa utii uletao haki.
17Lakini Mungu ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake;
18na mlipokwisha kuandikwa huru mkawa mbali ya dhambi, mlifanywa watumwa wa haki.
19Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa maana kama mlivyotoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na maasi mpate kuasi, vivyo sasa toeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa.
20Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali ya haki.
21Faida gani bassi mliyopata siku zile kwa mambo haya mnayotahayarikia sasa? kwa maana mwisho wa mambo haya ni mauti.
22Lakini sasa mkiisha kuandikwa huru, na kuwa mbali ya dhambi, na kufanywa watumwa wa Mungu, faida yenu mnayo, ndio kutakaswa, na mwisho wake uzima wa milele.
23Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; hali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu.