1 Wakorintho 12

1 Wakorintho 12

Karama Kutoka kwa Roho Mtakatifu

1Na sasa ninataka mwelewe kuhusu karama za Roho Mtakatifu.

2Mnayakumbuka maisha mliyoishi kabla hamjawa waamini. Mlipotoshwa na kuongozwa kuziabudu sanamu, ambazo hata kuzungumza haziwezi.

3Hivyo ninawaambia ya kwamba hakuna mtu anayezungumza kwa Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu alaaniwe.” Na hakuna anayeweza kusema “Yesu ni Bwana,” bila msaada wa Roho Mtakatifu.

4Kuna karama mbalimbali za Roho, lakini zote zinatoka kwa Roho yule yule.

5Kuna namna mbalimbali za kutumika, lakini sote tunatumika kwa niaba ya Bwana yule yule.

6Na kuna namna ambazo Mungu hufanya kazi ndani yetu sote, lakini ni Mungu yule yule anayetenda kazi ndani yetu ili tutende kila kitu.

7Kitu fulani kutoka kwa Roho kinaweza kuonekana ndani ya kila mtu. Roho humpa kila mtu hili ili awasaidie wengine.

8Roho humpa mtu fulani uwezo wa kuzungumza kwa hekima. Na Roho huyo huyo humpa mwingine uwezo wa kuzungumza kwa maarifa.

9Roho huyo huyo humpa mtu karama ya imani na humpa mwingine karama ya kuponya.

10Roho humpa mtu nguvu ya kutenda miujiza, na humpa mwingine uwezo wa kutabiri, na mwingine uwezo wa kupambanua kujua kilichotoka kwa Roho na ambacho hakikutoka kwa Roho. Roho humpa mtu fulani uwezo wa kusema kwa lugha zingine tofauti, na humpa mwingine uwezo wa kufasiri lugha hizo.

11Roho mmoja, Roho yule yule hufanya mambo yote haya. Roho ndiye huamua ampe nini kila mtu.

Mwili wa Kristo

12Mtu ana mwili mmoja, lakini una viungo vingi. Kuna viungo vingi, lakini viungo vyote hivyo ni mwili mmoja. Kristo yuko vivyo hivyo pia.

13Baadhi yetu ni Wayahudi na baadhi yetu si Wayahudi; baadhi yetu ni watumwa na baadhi yetu ni watu tulio huru. Lakini sisi sote tulibatizwa ili tuwe sehemu ya mwili mmoja kwa njia ya Roho mmoja. Nasi tulipewa Roho mmoja.[#12:13 Au “tulinyweshwa”.]

14Na mwili wa mtu una viungo zaidi ya kimoja. Una viungo vingi.

15Mguu unaweza kusema, “Mimi si mkono, na hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kusema hivi hakutafanya mguu usiwe kiungo cha mwili.

16Sikio linaweza kusema, “Mimi si jicho, hivyo mimi si wa mwili.” Lakini kwa kusema hivi hakutafanya sikio lisiwe kiungo cha mwili.

17Ikiwa mwili wote ungekuwa jicho, usingeweza kusikia. Ikiwa mwili wote ungekuwa sikio, usingeweza kunusa kitu chochote.

18-19Ikiwa viungo vyote vya mwili vingekuwa kiungo kimoja, mwili usingekuwepo. Kama jinsi ilivyo, Mungu aliweka viungo katika mwili kama alivyotaka. Alikipa kila kiungo sehemu yake.

20Hivyo kuna viungo vingi, lakini kuna mwili mmoja tu.

21Jicho haliwezi kuuambia mkono, “Sikuhitaji!” Na kichwa hakiwezi kuuambia mguu, “sikuhitaji!”

22Hapana, viungo vya mwili vinavyoonekana kuwa dhaifu zaidi, ndivyo vilivyo na umuhimu zaidi.

23Na viungo ambavyo tunadhani kuwa vina umuhimu mdogo ndivyo tunavitunza kwa heshima kubwa. Na tunavitunza kwa kuvifunika kwa uangalifu maalum viungo vya mwili tusivyotaka kuvionesha.

24Viungo vinavyopendeza zaidi visipofunikwa havihitaji matunzo haya maalum. Lakini Mungu aliuunganisha mwili pamoja na akavipa heshima zaidi viungo vilivyohitaji hadhi hiyo.

25Mungu alifanya hivi ili mwili wetu usigawanyike. Mungu alitaka viungo vyote tofauti vitunzane kwa usawa.

26Ikiwa kiungo kimoja cha mwili kinaugua, basi viungo vyote vinaugua pamoja nacho. Au ikiwa kiungo kimoja kinaheshimiwa, basi viungo vingine vyote vinashiriki heshima ya kiungo hicho.

27Ninyi nyote kwa pamoja ni mwili wa Kristo. Kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.

28Na Mungu ameweka katika kanisa, kwanza, baadhi kuwa mitume, pili manabii, na tatu walimu. Kisha Mungu ametoa nafasi kwa wale wanaofanya miujiza, wenye karama ya uponyaji, wanaoweza kuwasaidia wengine, wanaoweza kuwaongoza wengine na wale wanaoweza kuzungumza kwa lugha zingine.

29Je! wote ni mitume? Je! wote ni manabii? Je! wote ni walimu? Je! wote hufanya miujiza?

30Si wote wenye karama ya uponyaji. Si wote wanaozungumza kwa lugha zingine. Si wote wanaofasiri lugha.

31Endeleeni kuwa na ari ya kuwa na karama za Roho mnazoona kuwa ni kuu zaidi. Lakini sasa ninataka kuwaonesha njia iliyo kuu zaidi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International