1 Wakorintho 16

1 Wakorintho 16

Makusanyo kwa Ajili ya Waamini Katika Uyahudi

1Sasa, kuhusu mchango wa pesa kwa ajili ya watu wa Mungu: Fanyeni kama nilivyoyaambia makanisa ya Galatia kufanya.

2Siku ya kwanza ya kila wiki, kila mmoja wenu achukue kiasi cha pesa kutoka kwenye pesa zake na azitenge. Akusanye kiasi anachoweza kutokana na anavyobarikiwa. Na hivyo hamtahitaji kukusanya nitakapokuja.

3Nitakapofika, nitatuma baadhi ya watu wapeleke sadaka yenu Yerusalemu. Hawa watakuwa wale ambao ninyi mtakubali kuwa waende. Nitawatuma na barua ya utambulisho.

4Ikiwa itakuwa vizuri kwangu kwenda pia, basi tutasafiri pamoja.

Mipango ya Paulo

5Nimepanga kupitia Makedonia, hivyo nitakuja kwenu baada ya hapo.

6Pengine nitakaa kwenu kwa muda. Pengine nitakaa kwenu majira yote ya baridi. Hivyo mtaweza kunisaidia katika safari yangu, kila ninapokwenda.

7Sitaki kuja kuwaona sasa, kwa sababu nitaweza tu kukaa nanyi kwa muda mfupi, kabla haijanilazimu kwenda mahali pengine. Ninategemea kukaa pamoja nanyi kwa muda mrefu, ikiwa Bwana ataruhusu.

8Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste.

9Nitakaa hapa, kwa sababu sasa nimepewa fursa nzuri kwa kazi kubwa na inayokua. Na kuna watu wengi wanaopinga.

10Timotheo atakapokuja kwenu, mjitahidi akae kwa raha na amani akiwa kwenu. Anafanya kazi kwa ajili ya Bwana kama mimi.

11Hivyo yeyote miongoni mwenu asikatae kumpokea Timotheo. Msaidieni aendelee katika safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu. Ninategemea atakuja kwangu pamoja na ndugu wengine.

12Na sasa kuhusu Apolo: Ninamsihi sana aje na ndugu wengine kuwatembelea ninyi huko Korintho. Hajataka kuja sasa, lakini atakuja kwenu atakapopata nafasi.

Paulo Amalizia Barua Yake

13Iweni waangalifu. Simameni imara katika imani yenu. Muwe jasiri na wenye nguvu.

14Fanyeni kila kitu katika upendo.

15Mnajua kuwa Stefana na familia yake walikuwa waamini wa kwanza katika Akaya. Wamejitia katika kazi ya kuwahudumia watu wa Mungu. Ndugu zangu, ninawaomba,

16mjiweke chini ya uongozi wa watu kama hawa na wengine wanaofanya kazi kwa bidii na kutumika pamoja nao.

17Ninafurahi kwa sababu Stefana, Fortunato na Akaiko wamekuja. Hamko hapa pamoja nami lakini wamejaza nafasi yenu.

18Wamekuwa faraja kuu kwangu na kwenu pia. Basi, mnapaswa kuitambua thamani ya watu kama hawa.

19Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Priska wanawasalimu katika Bwana. Na kanisa linalokutana nyumbani mwao linawasalimu pia.

20Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kila mmoja wenu kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[#16:20 Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.]

21Hii ni salamu yangu kwa mkono wangu mwenyewe: Paulo .

22Ikiwa mtu yeyote hampendi Bwana, mwacheni mtu huyo abaki chini ya laana ya Mungu.

Njoo, Ewe Bwana!

23Neema ya Bwana Yesu iwe pamoja nanyi.

24Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International