1 Wakorintho 6

1 Wakorintho 6

Kutatua Migogoro Miongoni Mwa Waamini

1Kwa nini mnakwenda kwenye mahakama za kisheria mmoja wenu anapokuwa na shauri dhidi ya mwingine aliye miongoni mwenu? Mnajua ya kwamba mahakimu wa aina hiyo hawawezi kutegemewa kuamua kwa haki iliyo ya kweli. Sasa kwa nini mnawaruhusu wawaamulie aliye na haki? Kwa nini msiwaruhusu watakatifu wa Mungu waamue ni nani aliye na haki?

2Hamjui kuwa watakatifu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Hivyo, ikiwa mtauhukumu ulimwengu, hakika mnaweza kutatua mashauri kama hayo miongoni mwenu.

3Hakika mnajua kuwa tutawahukumu malaika. Kwa kuwa hiyo ni kweli basi hakika tunaweza kuhukumu masuala ya kawaida ya maisha.

4Sasa, ikiwa mna masuala kama haya ya kawaida ya maisha yanayotakiwa kuamuliwa, kwa nini mnayapeleka kwa wasio waamini? Hao ambao hawana umuhimu wo wote kwenu?

5Ninasema hivi ili kuwatahayarisha. Nina uhakika yupo mwenye hekima miongoni mwa waamini katika kanisa lenu anayeweza kutatua mgogoro kati ya waamini wawili.

6Lakini sasa mwamini mmoja anamshtaki mwamini mwenzake na mnaruhusu watu wasio waamini wawaamulie!

7Ule ukweli kuwa mnayo mashitaka baina yenu ninyi kwa ninyi tayari ni uthibitisho wa kushindwa kwenu kabisa. Ingekuwa bora kwenu kustahimili yasiyo haki ama kulaghaiwa.

8Lakini ninyi ndiyo mnaotenda mabaya kwa kudanganya. Na mnawafanyia hivi ndugu zenu katika Kristo!

9Msijidanganye. Hamjui ya kuwa wanaowatendea mabaya hawana nafasi katika ufalme wa Mungu. Ninasema kuhusu wazinzi, wanaoamini miungu wa uongo, wasio waaminifu katika ndoa, nao wanaolawitiana.[#6:9 Neno la Kiyunani linajumuisha wale wanaolawitiwa na wale wanaolawiti. Ina maana ya “[wanaume] waliolegea”, wenye haiba ya kike wanaokosa uthabiti walio nao wanaume. Hii ni pamoja na wanaume ambao kwa kawaida wanashiriki matumizi ya wanawake.]

10Pia wezi, walafi, walevi, watukanaji, au waongo wanaowadanganya wengine ili wawaibie hawatakuwa na sehemu katika ufalme wa Mungu.

11Baadhi yenu mlikuwa hivyo huko nyuma. Lakini mlisafishwa mkawa safi, mkafanywa kuwa watakatifu na mkahesabiwa haki na Mungu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.

Miili Yenu Itumike kwa Ajili ya Utukufu wa Mungu

12Mtu mmoja anaweza kusema, “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote.” Nami ninawaambia ya kuwa si vitu vyote vilivyo na manufaa. Hata kama ni kweli kuwa “Ninaruhusiwa kufanya kitu chochote,” Sitaruhusu kitu chochote kinitawale kama vile ni mtumwa.

13Mmoja wenu anasema, “Chakula ni kwa ajili ya tumbo na tumbo ni kwa ajili ya chakula, na Mungu ataviteketeza vyote.” Hiyo ni dhahiri, lakini mwili si kwa ajili ya zinaa, bali kwa ajili ya Bwana, na Bwana ni kwa ajili ya mwili.

14Na Mungu ataifufua miili yetu kutoka kwa wafu kwa nguvu ile ile aliyoitumia kumfufua Bwana Yesu.

15Hakika mnajua kuwa miili yenu ni sehemu ya Kristo mwenyewe. Hivyo sitakiwi kamwe kuchukua sehemu ya Kristo na kuiunganisha na kahaba!

16Maandiko yanasema, “Watu wawili watakuwa mmoja.” Hivyo mnapaswa kujua kuwa kila aliyeungana na kahaba, amekuwa mwili mmoja na kahaba.[#Mwa 2:24]

17Lakini aliyeungana na Bwana, yu mmoja naye katika roho.

18Hivyo ikimbieni dhambi ya uzinzi. Mnasema kuwa, “Kila dhambi ni kitu kilichomo katika akili tu haihusiki na mwili.” Lakini ninawaambia, anayetenda dhambi ya uzinzi anautendea dhambi mwili wake mwenyewe.

19Nina uhakika mnajua kuwa mwili wenu ni hekalu kwa ajili ya Roho Mtakatifu mliyepewa na Mungu na Roho Mtakatifu anaishi ndani yenu. Hamjimiliki ninyi wenyewe.[#6:19 Nyumba ya Mungu, mahali ambapo watu wa Mungu humwabudu. Hapa, inamaanisha kuwa waamini ndiyo hekalu la kiroho ambamo Mungu anaishi.]

20Mungu alilipa gharama kubwa ili awamiliki. Hivyo mtukuzeni Yeye kwa kutumia miili yenu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International