The chat will start when you send the first message.
1Sasa nitaandika kuhusu suala jingine mliloniandikia mkiuliza kuhusu nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu. Ni kweli kuwa “Sote tuna ujuzi”, kama mnavyosema. Lakini ujuzi huu unawajaza watu majivuno. Upendo ndiyo unaolisaidia kanisa kuwa imara.[#8:1 Mnyama aliyechinjwa na kutolewa kuonesha ibada. Pia katika mstari wa 10.]
2Wale wanaodhani kuwa wanajua jambo fulani bado hawajui chochote kwa namna inavyopaswa.
3Lakini Mungu anamjua mtu anayempenda.
4Hivyo sasa vipi kuhusu kula nyama iliyotolewa sadaka kwa sanamu? Tunajua kuwa “sanamu si lolote katika ulimwengu” huu na tunajua kuwa “kuna Mungu mmoja tu”.
5Baadhi ya watu husema kuwa kuna miungu wanaoishi mbinguni na miungu wengine huishi duniani. Hata kama kuna “miungu” na “mabwana” wanaoaminiwa na watu, hilo si muhimu kwetu.
6Tuna Mungu mmoja tu, na ambaye ndiye Baba yetu. Vitu vyote vilitoka kwake nasi tunaishi kwa ajili yake. Na kuna Bwana mmoja tu, Yesu Kristo. Vitu vyote viliumbwa kupitia yeye, nasi tunaishi kwa ajili yake.
7Lakini si watu wote wanaojua hili. Baadhi ya watu walikuwa na tabia ya kuabudu sanamu huko nyuma. Hivyo wanapokula nyama, bado wanahisi kuhukumiwa kana kwamba wanakula nyama iliyotolewa kwa sanamu. Hawana uhakika ikiwa ni sahihi kula nyama.
8Lakini chakula hakitatuweka karibu na Mungu. Kukataa kula hakutufanyi tumpendeze kidogo Mungu wala kula hakutuweki karibu na Mungu.
9Lakini iweni makini na uhuru wenu. Uhuru wa kula kitu unaweza kuwafanya walio na mashaka wakaanguka katika dhambi kwa kula vyakula hivyo.
10Mnaelewa kuwa inaruhusiwa kula kitu chochote, hivyo unaweza kula hata katika hekalu la sanamu. Lakini hilo linaweza kumfanya mtu mwenye mashaka akaona kuwa kula chakula kama hicho ni kitendo cha kuabudu sanamu.
11Hivyo ndugu huyu aliye dhaifu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake, anaweza akaangamizwa kwa sababu ya uelewa wako ulio mzuri zaidi.
12Unapomtenda dhambi kinyume cha ndugu zako walio katika Kristo kwa namna hii na unawaumiza kwa kuwafanya wafanye mambo wanayoyachukulia kuwa mabaya, nawe pia unamtenda dhambi Kristo.
13Hivyo ikiwa chakula ninachokula kinamfanya mwamini mwingine kutenda dhambi, siwezi kula chakula hicho tena. Nitaacha kula chakula hicho ili nisimfanye ndugu yangu atende dhambi.