1 Yohana 3

1 Yohana 3

Tu Watoto wa Mungu

1Baba ametupenda sisi sana! Hili linaonesha jinsi anavyotupenda: Tunaitwa watoto wa Mungu. Ni kweli kuwa tu watoto wa Mungu. Lakini watu waliomo duniani hawaelewi ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu, kwa sababu hawamjui yeye.

2Wapendwa, sasa tu watoto wa Mungu. Mungu hajatuonyesha bado namna tutakavyokuwa wakati unaoukuja. Lakini tunajua ya kwamba Kristo atakapokuja tena, tutafanana naye. Tutamwona kama alivyo.

3Ni mtakatifu, na kila aliye na matumaini haya katika yeye huendelea kuwa mtakatifu.

4Kila atendaye dhambi huivunja sheria ya Mungu. Ndiyo, kutenda dhambi ni sawa na kuishi kinyume na sheria ya Mungu.

5Mwajua ya kuwa Kristo alikuja kuziondoa dhambi za watu. Haimo dhambi ndani ya Kristo.

6Hivyo kila anayeishi katika Kristo haendelei kutenda dhambi. Kama wakiendelea kutenda dhambi, kwa hakika hawajamwelewa Kristo na hawajamjua kamwe.

7Watoto wapendwa, msimruhusu mtu yeyote kuwadanganya. Kristo daima alitenda yaliyo haki. Hivyo kuwa mwema kama Kristo, ni lazima utende yaliyo haki.

8Mwovu amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kila anayeendelea kutenda dhambi ni mali ya Mwovu. Mwana wa Mungu alikuja kwa ajili ya hili: Kuziharibu kazi za Mwovu.

9Wale ambao ni watoto wa Mungu hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wanayo maisha mapya waliyopewa na Mungu. Hawaendelei kutenda dhambi, kwa sababu wamefanyika watoto wa Mungu.[#3:9 Kwa maana ya kawaida, “mbegu yake”.]

10Hivyo tunaweza kuwatambua walio watoto wa Mungu na walio watoto wa Mwovu. Hawa ndiyo wasio watoto wa Mungu: Wale wanaotenda mambo yasiyo haki na wale wasiowapenda ndugu zao wa kike na wa kiume katika familia ya Mungu.

Ni lazima Tupendane Sisi kwa Sisi

11Haya ni mafundisho mliyoyasikia toka mwanzo: Ni lazima tupendane sisi kwa sisi.

12Msiwe kama Kaini. Aliyekuwa upande wa Mwovu. Kaini alimwua ndugu yake. Lakini kwa nini alimwua? Ni kwa sababu alichokifanya Kaini kilikuwa cha kiovu, na alichokifanya nduguye kilikuwa cha haki.

13Kaka zangu na dada zangu, msishangae watu wa dunia hii wakiwachukia.

14Tunafahamu ya kuwa tumevuka kutoka mautini na kuingia uzimani. Tunafahamu hili kwa sababu tunapendana sisi kwa sisi kama ndugu wa kike na wa kiume. Yeyote asiyewapenda kaka zake na dada zake angali amekufa.

15Kila anayemchukia nduguye anayeamini ni muuaji. Nanyi mnajua kuwa hakuna muuaji aliye na uzima wa milele.

16Hivi ndivyo tunavyojua jinsi upendo wa kweli ulivyo: Yesu aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Hivyo nasi tunapaswa kuyatoa maisha yetu, kwa ajili ya ndugu wa kike na wa kiume katika familia ya Kristo.

17Itakuwaje pale muumini tajiri mwenye fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote akamwona dada ama kaka yake aliye maskini na asiye na fedha za kutosha kupata mahitaji yake yote. Endapo muumini huyu tajiri hatamsaidia muumini yule maskini, basi ni wazi kwamba upendo wa Mungu haumo ndani ya muumini yule tajiri.

18Watoto wangu, upendo wetu usiwe wa maneno na kuongea tu. Hapana, upendo wetu unapaswa kuwa halisi. Hatuna budi kuuonyesha upendo wetu kwa mambo yale tunayofanya.

19-20Hivyo ndivyo tunavyojua kuwa sisi tu wa ile njia ya kweli. Pale mioyo yetu inapotufanya tujisikie kuwa na hatia, bado tunaweza kuwa na amani mbele za Mungu, kwa sababu Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu. Yeye anajua kila kitu.

21Rafiki zangu wapendwa, ikiwa hatujisikii kuwa tunatenda yasiyo haki, basi hatupaswi kuwa na hofu tunapoenda kwa Mungu.

22Na Mungu anatupa kile tunachomwomba. Nasi tunapokea kwa sababu tunazitii amri za Mungu na kufanya yanayompendeza.

23Hili ndilo Mungu analoliamuru: Kwamba tumwamini Mwanaye Yesu Kristo, na kwamba tupendane sisi kwa sisi kama alivyoamuru.

24Wote wanaozitii amri za Mungu wanaishi ndani ya Mungu. Na Mungu anaishi ndani yao. Tunajuaje kuwa Mungu anaishi ndani yetu? Tunajua kwa sababu ya Roho aliyetupa sisi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International