1 Petro 1

1 Petro 1

1Kutoka kwa Petro, mtume wa Yesu Kristo.

Kwa wateule wa Mungu, ambao huonekana kama ni wageni kutoka nchi nyingine, waliotawanyika katika majimbo yote ya Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia, na Bithinia.

2Kwa kadri ya mpango wa Mungu Baba alioufanya muda mrefu uliopita, mliteuliwa muwe wake kwa kufanywa watakatifu na Roho Mtakatifu. Mliteuliwa kuwa waatiifu kwa Mungu na kutakaswa na kujumuishwa miongoni mwa watu wa Agano Jipya kwa kunyunyiziwa damu ya Yesu Kristo.[#1:2 Katika Kut 24:7-8 Musa aliwanyunyizia damu watu wa Israeli ili kukamilisha agano lao pamoja na Mungu, baada ya kuahidi kutii amri zake zote, Damu ya Yesu inakamilisha Agano Jipya kati ya Mungu na watu wake.]

Neema na amani ya Mungu viwe pamoja nanyi kwa wingi.

Tumaini Lililo Hai

3Atukuzwe Mungu Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Katika rehema zake kuu, Mungu alitufanya sisi tuzaliwe upya ili tuwe na tumaini lililo hai, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo kutoka kwa waliokufa,

4na ili kuwa na urithi usioharibika, ulio safi na usiofifia, uliotunzwa kwa ajili yenu kule mbinguni.

5Ni kwa ajili yenu ninyi ambao kwa njia ya imani, mnalindwa na nguvu za Mungu ili mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.

6Hili linawafanya mfurahi sana, hata kama kwa sasa imewalazimu mhuzunishwe kwa kipindi kifupi kwa masumbufu na mateso ya aina mbali mbali.

7Kwa masumbufu haya imani yenu inajaribiwa na kuithibitishwa kuwa ni ya kweli. Hii inafananishwa na dhahabu pale inapopitishwa kwenye moto kuthibitisha uhalisi wake. Lakini hata dhahabu ya kweli inaweza kuharibiwa. Hivyo imani ina thamani zaidi kuliko dhahabu. Pale imani yenu inapothibitika kuwa ni ya kweli, matokeo yake ni sifa, utukufu na heshima kwa Mungu wakati wa kurudi kwake Yesu Kristo.

8Hata kama hamjamwona Yesu, lakini mnampenda. Hata kama hamuwezi kumuona kwa sasa, lakini mnamwamini yeye na mmejazwa na furaha ya ajabu isiyoweza kuelezwa kwa maneno.

9Mnaupokea wokovu wenu ambao ni lengo la imani yenu.

10Manabii waliotabiri juu ya neema ambayo ingeoneshwa kwenu, walipeleleza kwa makini na kwa uangalifu wakaulizia habari za wokovu huu.

11Roho wa Kristo alikuwa ndani yao, naye aliwapa ushuhuda mapema kuhusu Kristo kwamba itamlazimu kuteswa na baada ya hapo atapokea utukufu. Manabii waliuliza kutaka kujua wakati gani na katika mazingira gani mambo haya yangetokea.

12Ilifunuliwa kwao kwamba walikuwa hawajitumikii wenyewe. Badala yake, waliwatumikia ninyi walipotabiri juu ya mambo haya. Na sasa mmesikia juu ya mambo haya kutoka kwa wale waliyowaambia habari Njema kwa msaada wa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Hata malaika wangetamani sana kufahamu zaidi juu ya mambo haya mliyoambiwa.

Mwito Kwa Maisha Matakatifu

13Hivyo mkeshe katika fahamu zenu na kuwa na kiasi. Yawekeni kikamilifu matumaini yenu katika baraka mtakazopewa wakati Yesu Kristo atakapofunuliwa.

14Kama watoto watiifu, msiyaache maisha yenu yandelee kutawaliwa na tamaa mbaya mlizokuwa nazo awali mlipokuwa wajinga.

15Badala yake, kama ambavyo yeye Mungu aliyewaita alivyo mtakatifu, hata ninyi muwe watakatifu katika kila mnalotenda.

16Hivyo Maandiko yanasema: “Iweni watakatifu, kwa sababu mimi ni mtakatifu.”[#Law 11:44-45; 19:2; 20:7]

17Na kama Baba mnayemwita Mungu anayewahukumu watu bila upendeleo kwa kadri ya matendo ya kila mtu, muishi maisha ya utauwa na hofu kwa Mungu katika miaka yenu ya kukaa humu duniani kama wageni.

18Mnajua kwamba siyo kwa mambo yaharibikayo kama fedha au dhahabu, kwamba mliokolewa kutoka katika maisha yasiyofaa mliyoyapokea kutoka kwa babu zenu,

19bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya mwanakondoo asiye na dosari wala ila.

20Kristo alichaguliwa kabla ya uumbaji wa ulimwengu, lakini alidhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu.

21Kupitia Kristo mmekuwa waamini katika Mungu, aliyemfufua kutoka kwa wafu na kumpatia utukufu. Ili imani yenu na matumaini yawekwe katika Mungu.

22Sasa kwa vile mmejitakasa wenyewe kwa kuitii kweli hadi mwisho kwamba mtaonesha upendo wa kweli wa kindugu, jitahidini kupendana ninyi kwa ninyi kwa mioyo iliyo safi.

23Mmezaliwa upya sio kama matokeo ya mbegu inayoharibika, lakini kama matokeo ya mbegu isiyoharibika. Mmezaliwa upya kwa njia ya ujumbe wa Mungu, ambao unaleta uzima ndani yenu.

24Hivyo, kama Maandiko yanavyosema:

“Watu wote ni kama manyasi,

na utukufu wao wote ni kama maua pori katika manyasi.

Manyasi yananyauka na kukauka,

na maua yanapukutika,

25bali ujumbe wa Bwana unadumu milele.”[#Isa 40:6-8]

Na ujumbe huo ni habari njema iliyohubiriwa kwenu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International