The chat will start when you send the first message.
1Hivyo acheni uovu wote, pamoja na uongo, hali za unafiki na wivu na aina zote za kashfa.
2Kama watoto wachanga, mnapaswa kuyatamani maziwa ya kiroho yaliyo safi, ili kwa ajili ya hayo muweze kukua na kuokolewa,
3kwa vile mmekwisha kuujaribu wema wa Bwana.
4Mkaribieni Bwana Yesu, aliye Jiwe lililo Hai, lililokataliwa na watu, bali kwa Mungu ni jiwe lililoteuliwa na kuheshimika.
5Ninyi pia, kama mawe yaliyo hai mnajengwa ili kuwa hekalu la kiroho. Mmekuwa makuhani watakatifu mkimtumikia Mungu kwa kutoa sadaka za kiroho zinazokubalika kwake kwa njia ya Yesu Kristo.
6Hivyo, Maandiko yanasema,
“Tazameni, naweka katika Sayuni Jiwe la msingi katika jengo,
lililoteuliwa na kuheshimika,
na yeyote anayeamini hataaibishwa.”
7Inamaanisha heshima kwenu mnaoamini, bali kwa wasioamini,
“jiwe walilolikataa wajenzi
limekuwa jiwe la muhimu kuliko yote.”
8Na,
“jiwe linalowafanya watu wajikwae
na mwamba unaowafanya watu waanguke.”
Walijikwaa kwa sababu hawakuutii ujumbe wa Mungu, na Mungu alisema hilo litatokea wasipotii.
9Lakini ninyi ni watu mlioteuliwa, ni Ukuhani unaomtumikia Mfalme. Ninyi ni taifa takatifu nanyi ni watu wa Mungu. Yeye aliwaita Ili muweze kutangaza matendo yake yenye nguvu. Naye aliwaita mtoke gizani na mwingie katika nuru yake ya ajabu.
10Kuna wakati hamkuwa watu,
lakini sasa mmekuwa watu wa Mungu.
Kuna wakati hamkuoneshwa rehema,
lakini sasa mmeoneshwa rehema za Mungu.
11Rafiki zangu, ninawasihi kama wapitaji na wageni katika ulimwengu huu kuwa mbali na tamaa za kimwili, ambazo hupingana na roho zenu.
12Muwe na uhakika wa kuwa na mwenendo mzuri mbele ya wapagani, ili hata kama wakiwalaumu kama wakosaji, watayaona matendo yenu mazuri nao wanaweza kumpa Mungu utukufu katika Siku ya kuja kwake.
13Nyenyekeeni kwa mamlaka yoyote ya kibinadamu kwa ajili ya Bwana. Mnyenyekeeni mfalme, aliye mamlaka ya juu kabisa.
14Na muwatii viongozi waliotumwa na mfalme. Wametumwa ili kuwaadhibu wale wanaokosa, na kuwapongeza wale wanaofanya mazuri.
15Kwa kuwa mapenzi ya Mungu ni kwamba, kwa kutenda mema mtayanyamazisha mazungumzo ya kijinga ya watu wasio na akili.
16Muishi kama watu walio huru, lakini msiutumie uhuru huo kama udhuru wa kufanya maovu. Bali muishi kama watumishi wa Mungu.
17Onesheni heshima kwa watu wote: Wapendeni ndugu zenu na dada zenu waliomo nyumbani mwake Mungu. Mcheni Mungu na mumheshimu mfalme.
18Watumwa mlio nyumbani, watumikieni mabwana wenu kwa heshima yote, siyo tu wale walio wapole na wenye busara, bali hata wale walio wakali.[#2:18 Au “kwa heshima na taadhima kwa Mungu”.]
19Baadhi yenu mtapata mateso wakati ambapo hamjafanya kosa lolote. Ikiwa utaweza kuvumilia maumivu na kuweka fikra zako kwa Mungu, hilo linampendeza sana Mungu.
20Kwani kuna sifa gani iliyopo kwako kama utapigwa kwa kutenda mabaya na kuvumilia? Lakini kama utateseka kwa kutenda mema na kustahimili, hili lampendeza Mungu.
21Ni kwa kusudi hili mliitwa na Mungu, kwa sababu Kristo pia aliteseka kwa ajili yenu na kwa kufanya hivyo aliacha kielelezo kwenu, ili tuweze kuzifuata nyayo zake.
22“Hakutenda dhambi yoyote,
wala hakukuwa na udanganyifu uliopatikana kinywani mwake.”
23Alipotukanwa hakurudishia matusi. Alipoteseka, hakuwatishia, bali wakati wote alijitoa mwenyewe kwa Mungu ahukumuye kwa haki.
24Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu kwenye mwili wake hadi pale msalabani, ili tuweze kuacha kuishi kwa ajili ya dhambi na kuishi kwa ajili ya haki. Ilikuwa ni kwa njia ya majeraha yake kwamba mliponywa.
25Kwani mlikuwa kama kondoo wanaotangatanga huko na huko, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa maisha yenu.