1 Wathesalonike 1

1 Wathesalonike 1

1Salamu toka kwa Paulo, Sila, na Timotheo.

Kwa kanisa lililoko Thesalonike lililo milki ya Mungu baba na Bwana Yesu Kristo.

Neema na amani ziwe zenu.

Maisha na Imani ya Wathesalonike

2Kila mara tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu nyote na kuwataja katika maombi yetu.

3Kila tunapomwomba Mungu baba yetu, tunawakumbuka kwa yote mliyofanya kwa sababu ya imani yenu. Na tunawakumbuka kwa kazi mliyofanya kwa sababu ya upendo wenu. Na tunakumbuka jinsi mlivyo imara kwa sababu ya tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo.

4Ndugu zetu, Mungu anawapenda. Nasi twajua yakuwa amewachagua muwe watu wake.

5Tulipowaletea Habari Njema kwenu, tulikuja na yaliyo zaidi ya maneno. Tuliwaletea ile Habari Njema yenye uweza, pamoja na Roho Mtakatifu, na tulikuwa na uhakika kamili hiyo ilikuwa ni Kweli halisi. Pia mnafahamu tulivyo enenda tulipo kuwa pamoja nanyi. Tuliishi hivyo ili kuwasaidia ninyi.

6Nanyi mkauiga mfano wetu na mfano wa Bwana. Mliteseka sana, lakini bado mliyakubali mafundisho na furaha inayotokana na Roho Mtakatifu.

7Mlifanyika mfano wa kuigwa na waaminio wote wa Makedonia na Akaya.

8Mafundisho ya Bwana yameenea toka Makedonia mpaka Akaya na nje ya mipaka yake. Kwa kweli, imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali, hivyo hatuna haja ya kumwambia mtu yeyote kwa habari hii.

9Watu kila mahali wanasimulia habari ya namna mlivyotupokea vizuri tulipo kuwa pamoja nanyi. Wanasimulia namna mlivyoacha kuiabudu miungu ya uongo na kubadilika na kuanza kumwabudu Mungu aliye hai na wa kweli.

10Na mkaanza kumngoja mwana wa Mungu aje kutoka mbinguni, Mwana ambaye Baba alimfufua kutoka kwa wafu. Yeye ni Yesu, anayetuokoa kutoka katika hukumu yenye hasira ya Mungu inayokuja.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International