1 Wathesalonike 5

1 Wathesalonike 5

Uwe tayari kwa ujio wa Bwana

1Na sasa ndugu zangu, hatuna haja ya kuwaandikia juu ya nyakati na tarehe.

2Ninyi mnafahamu vizuri kuwa siku ambayo Bwana atakuja itakuwa ya kushitukiza, kama mwizi anavyokuja usiku.

3Watu watasema, “tuna amani na tuko salama.” Wakati huo ndipo uharibifu utakapowajia haraka, kama maumivu anayoyapata mwanamke anapojifungua. Na watu hao hawataweza kukwepa.

4Lakini ninyi ndugu zangu, hamuishi katika giza. Na hivyo ile siku haitawashangaza kama mwivi.

5Nyote ni watu wa nuru. Ni watu wa mchana. Hatuko katika usiku wala giza.

6Hivyo tusiwe kama watu wengine. Tusiwe wasinziao. Tuwe macho na wenye kiasi.

7Watu walalao, hulala usiku. Watu wanywao kupita kiasi, hunywa usiku.

8Bali sisi ni watu wa mchana, hivyo tujitawale wenyewe. Tuvae imani na upendo vitulinde. Na tumaini la wokovu liwe kwetu kama kofia ya vita.

9Mungu hakutuchagua tuangamie katika hasira yake. Mungu alituchagua tuwe na wokovu katika Bwana wetu Yesu Kristo.

10Yesu alikufa kwa ajili yetu ili tuishi pamoja nae. Haijalishi kama tu hai au wafu atakapokuja.

11Hivyo farijianeni ninyi kwa ninyi na msaidiane kukua imara katika imani, kama mnavyofanya sasa.

Maagizo ya Mwisho na Salamu

12Tunawaomba mwatambue wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao, kama wafuasi wa Bwana, wanatumika kama viongozi wenu na kuwafundisha namna ya kuishi.

13Wapeni heshima ya hali ya juu na upendo kwa sababu ya kazi wanayofanya.

Ishini kwa amani kila mmoja na mwenzake.

14Tunawasihi, kuwaonya wale wanaokataa kuishi kwa kuwajibika. Watieni moyo wanaoogopa. Wasaidieni walio dhaifu. Mvumilieni kila mmoja.[#5:14 Ikiwa na maana ya “kuishi kwa kufuata utaratibu unaofaa” Kuishi pasipo kuwajibika ni kutofanya kazi.]

15Asiwepo anae jaribu kulipiza baya kwa baya. Lakini kila mara mfanye lililo jema kwa kila mmoja wenu na kwa watu wote.

16Muwe na furaha daima.

17Msiache kuomba.

18Shukuruni kwa kila jambo. Hivi ndivyo Mungu anavyotutaka tuishi katika Kristo Yesu.

19Msiizimishe kazi ya Roho Mtakatifu.

20Msiuchukulie unabii kama kitu kisicho cha muhimu.

21Lakini pimeni kila kitu. Lishikeni lililo jema,

22na mkae mbali na kila aina ya ovu.

23Tunaomba kwamba Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, atawafanya muwe watakatifu mkiwa wake. Tunaomba kwamba katika roho yote, nafsi yote, na mwili mzima mtahifadhiwa salama pasipo lawama Bwana wetu Yesu Kristo atakapokuja.

24Yeye awaitae atawatendea haya. Mnaweza kumtumainia.

25Kaka na dada zangu, tafadhali mtuombee.

26Wasalimuni ndugu wote kwa salamu maalum ya watu wa Mungu.[#5:26 Kwa maana ya kawaida, “busu takatifu”.]

27Ninawaagiza kwa mamlaka ya Bwana kuusoma walaka huu kwa waamini wote huko.

28Neema ya Bwana wetu Yesu kristo iwe nanyi nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International