The chat will start when you send the first message.
1Natamani mngekuwa na subira nami hata pale ninapokuwa mjinga kidogo. Tafadhali muwe na subira nami.
2Nina wivu unaotoka kwa Mungu kwa ajili yenu. Niliahidi kuwatoa ninyi kama bibi harusi kwa mume mmoja. Niliahidi kuwatoa ninyi kwa Kristo muwe bibi harusi wake aliye safi.[#11:2 Kwa maana ya kawaida, “bikira au mwanamwali”.]
3Ila nina hofu kuwa nia zenu zitapotoshwa muache kujitoa kwa dhati na kumfuata Yesu Kristo kwa moyo safi. Hili laweza kutokea kama vile Hawa alivyodanganywa na nyoka kwa akili zake za ujanja wenye udanganyifu.
4Mnaonekana kuwa na subira na mtu yeyote anayekuja kwenu na kuwaeleza habari za Yesu aliye tofauti na Yesu yule ambaye sisi tuliwaambia habari zake. Mnaonekana kuwa radhi kuipokea roho au ujumbe ulio tofauti na roho na ujumbe ambao mlioupokea kutoka kwetu.
5Sidhani kuwa hao “mitume wakuu” ni bora kuliko mimi nilivyo.
6Ni kweli kuwa mimi siye mtu nilyefunzwa kwa mzungumzaji, lakini nina ufahamu wa mambo. Tumeliweka hili wazi kwenu kwa njia zote na kwa mazingira yote.
7Nilifanya kazi ya kutangaza Habari Njema za Mungu kwenu bila malipo. Nilijinyenyekeza ili kuwafanya ninyi kuwa wa muhimu. Je! Mwadhani nilikosea katika hilo?
8Nilipokea malipo toka makanisa mengine. Ilikuwa kana kwamba nimechukua fedha toka kwao ili niweze kuwatumikia ninyi.
9Kama nilihitaji chochote nilipokuwa nanyi, sikumsumbua yeyote kati yenu. Kina kaka waliofika kutoka Makedonia walinipa yote niliyohitaji. Sikutaka kuwa mzigo kwenu kwa namna yeyote ile. Na kamwe sitakuwa mzigo kwenu.
10Hakuna mtu yeyote katika jimbo lote la Akaya anayeweza kunizuia kujivuna juu ya hilo. Nasema hili katika kweli ya Kristo iliyo ndani yangu.
11Kwa nini siwalemei? Je! Mnadhani ni kwa sababu siwapendi? Mungu anajua ya kwamba ninawapenda.
12Na nitaendelea kufanya kile ninachokifanya sasa, kwa sababu nataka kuwazuia watu hao wasiwe na sababu ya kujivunia. Wangependa kusema kuwa kazi ile wanayojivunia ni sawa na kazi yetu.
13Wao ni mitume wa uongo, watenda kazi walio wadanganyifu. Wao hujifanya kuwa ni mitume wa Kristo.
14Hilo halitushangazi sisi, kwa sababu hata Shetani mwenyewe hujigeuza na kujifanya kuwa malaika wa nuru.[#11:14 Mtumishi au tarishi wa Mungu. Shetani anawadanganya watu waone kuwa ametumwa na Mungu.]
15Hivyo, hiyo haitufanyi sisi kustaajabu ikiwa watumishi wa shetani watajigeuza na kujifanya kuwa watumishi wanaofanya yaliyo ya haki. Lakini mwishowe watapokea hukumu wanayostahili.
16Ninawaambia tena: Asiwepo yeyote wa kudhani kuwa mimi ni mjinga. Lakini kama mnadhani kuwa mimi ni mjinga, basi nipokeeni kama vile ambavyo mngempokea mjinga. Kisha nami naweza kujivuna angalau kidogo zaidi pia.
17Lakini mimi sizungumzi kwa namna ambavyo Bwana angelizungumza. Mimi ninajivuna kama vile mjinga.
18Wengi wengine wanajivuna jinsi ambavyo watu wa dunia hii wanafanya. Hivyo, nami nitajivuna kwa namna hiyo.
19Mna busara, hivyo mtamvumilia kwa furaha mjinga!
20Nasema haya kwa sababu mnamvumilia hata mtu yule anayewatumia vibaya. Mnawavumilia wale wanaowarubuni akili na kudhani kuwa wao ni bora kuliko ninyi, au wanaowapiga usoni!
21Ninaona aibu kusema haya, lakini tulikuwa “dhaifu sana” kuyafanya mambo kama hayo kwenu.
Lakini kama kuna mtu aliye jasiri vya kutosha kujivuna, nami nitajivuna pia. (Ninaongea hivi kama mjinga.)
22Je! watu hao ni Wayahudi? Mimi pia. Je! ni Waebrania? Mimi pia. Je! wanatoka katika familia ya Abrahamu? Mimi pia.
23Je! wanamtumikia Kristo? Mimi ninamtumikia zaidi sana. (Je! mimi ni mwendawazimu kuongea kwa jinsi hii?) Nimefanya kazi kwa juhudi kuliko wao. Nimekuwa gerezani mara nyingi. Nimepigwa vibaya sana. Nimekuwa katika hali za hatari ya kufa mara nyingi.
24Mara tano Wayahudi wamenipa adhabu ya viboko 39.
25Mara tatu katika nyakati tofauti nimepigwa kwa fimbo. Mara moja nilikuwa karibu kuuawa kwa kupigwa kwa mawe. Mara tatu nimevunjikiwa na merikebu, na mara moja katika hizo nilikesha usiku na kushinda kutwa nzima tukielea baharini.
26Katika safari zangu za mara kwa mara nimekuwa katika hatari za kwenye mito, majambazi, watu wangu wenyewe, na toka kwa watu wasio Wayahudi. Nimekuwa katika hatari mijini, katika maeneo wasioishi watu, na katika bahari. Na nimekuwa katika hatari za watu wanaojifanya kuwa waamini lakini siyo waamini.
27Nimefanya kazi ngumu na za kuchosha, na mara nyingi sikuweza kulala usingizi. Nimekuwa mwenye njaa na kiu. Mara nyingi nimekosa kula chakula. Nimekuwa katika hali ya baridi na kutokuwa na nguo za kujifunika.
28Na kuna matatizo mengine mengi zaidi. Mojawapo ya hayo ni mzigo nilio nao kila siku wa majukumu yangu: Ninawaza juu ya makanisa yote.
29Ninajisikia kuwa mdhaifu kila mara mtu mwingine anapokuwa dhaifu. Ninapata hasira sana pale mtu yeyote anapoingizwa dhambini.
30Ikiwa ni lazima nisifu, nitajisifu katika vitu vinavyonidhihirisha kuwa mimi ni dhaifu.
31Mungu ajua kuwa sisemi uongo. Yeye ni Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, na anapaswa kutukuzwa milele.
32Nilipo kuwa Dameski, gavana wa mfalme Areta alitaka kunikamata, hivyo aliweka walinzi nje ya malango ya jiji.
33Lakini baadhi ya rafiki wakaniweka ndani ya kikapu. Kisha wakaniteremsha chini kupitia dirisha lililokuwa kwenye katika ukuta wa mji. Hivyo nikamtoroka gavana.