Matendo 12

Matendo 12

Matatizo Mengi kwa waamini

1Katika wakati huu huu, Mfalme Herode akaanza kuwatesa baadhi ya waamini waliokuwa sehemu ya kanisa.

2Aliamuru Yakobo aliyekuwa kaka yake Yohana, auawe kwa upanga.

3Herode alipoona kuwa Wayahudi wamelifurahia jambo hili, aliamua kumkamata Petro pia. Hii lilitokea katika kipindi cha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu.

4Alimkamata Petro na kumfunga gerezani, ambako alilindwa na kundi la askari kumi na sita. Herode alipanga kumleta Petro mbele ya watu ili ahukumiwe, lakini alisubiri mpaka baada ya sikukuu ya Pasaka.[#12:4 Askari hawa walikuwa na zamu ya kulinda ya askari wanne wanne.]

5Hivyo Petro aliwekwa gerezani lakini kanisa lilikuwa likiomba kwa Mungu bila kuacha kwa ajili yake.

Petro Atolewa Nje ya Gereza

6Wakati wa usiku kabla ya siku ambayo Herode alipanga kumhukumu mbele ya watu, Petro, akiwa amefungwa minyororo miwili, alikuwa amelala katikati ya askari wawili. Na askari waliokuwa nje ya mlango walikuwa wanalinda gereza.

7Ghafla malaika wa Bwana alikuwa amesimama pale, na chumba kilijaa mwanga. Malaika akamwamsha Petro kwa kumpiga upande, akasema, “Amka haraka!” Minyororo ikaanguka kutoka mikono mwa Petro.

8Malaika akasema, “Vaa nguo na viatu vyako.” Petro alifanya kama alivyoambiwa. Kisha malaika akasema, “Vaa koti lako na unifuate.”

9Hivyo malaika akatoka nje na Petro alimfuata. Hakujua kama kweli malaika alikuwa anafanya hili. Alidhani alikuwa anaona maono.

10Petro na malaika wakavuka lindo la kwanza na lindo la pili. Kisha walifika kwenye lango la chuma lililowatenganisha na mji. Lango likafunguka. Baada ya kuvuka lango na kutembea umbali wa kama mtaa mmoja, malaika akatoweka ghafla.

11Ndipo Petro akatambua kuwa haikuwa ndoto. Akawaza moyoni akisema, “Sasa ninajua kwamba Bwana hakika alimtuma malaika wake kwangu. Ameniokoa kutoka kwa Herode na kutoka kwenye mabaya yote ambayo Wayahudi walidhani yatanipata.”

12Petro alipotambua hili, alikwenda nyumbani kwa Mariamu, mama yake Yohana, aliyeitwa Marko. Watu wengi walikuwa wamekusanyika pale wakiomba.

13Petro alibisha kwenye mlango wa nje. Mtumishi wa kike aliyeitwa Rhoda alikuja ili afungue mlango.

14Alipoitambua sauti ya Petro, alifurahi sana hata akasahau kufungua mlango. Akakimbilia ndani na kuliambia kundi, “Petro yuko mlangoni!”

15Waamini wakamwambia, “Wewe una kichaa!” Lakini alipoendelea kusema kwamba ni kweli Petro yuko mlangoni. Waamini walisema, “Lazima atakuwa malaika wa Petro.”

16Lakini Petro aliendelea kubisha mlangoni. Waamini walipoufungua mlango na kumwona, wakashangaa.

17Petro akawafanyia ishara kwa mkono wake kuwaambia wanyamaze. Akawaeleza namna Bwana alivyomtoa nje ya gereza. Akasema, “Mwambieni Yakobo na ndugu wengine kilichotokea.” Kisha akawaacha na kwenda sehemu nyingine.

18Siku iliyofuata askari walichanganyikiwa. Walijiuliza nini kimempata Petro.

19Herode alimtafuta kila mahali lakini hakumpata. Hivyo aliwahoji walinzi na kuamuru wauawe.

Kifo cha Herode Agripa

Baadaye, Herode alihama kutoka Uyahudi na kwenda katika mji wa Kaisaria na kukaa huko kwa muda.

20Herode aliwakasirikia sana watu katika miji ya Tiro na Sidoni. Lakini miji hii ilihitaji chakula kutoka katika nchi yake, hivyo baadhi yao walimjia wakitaka amani naye. Waliweza kumshawishi Blasto mtumishi binafsi wa Mfalme ili awasaidie.

21Herode alichagua siku maalumu ya kukutana nao. Siku hiyo alivaa vazi zuri la kifalme. Aliketi kwenye kiti chake cha enzi na kuwahutubia watu.

22Watu wakapaza sauti zao na kusema, “Hii ni sauti ya mungu, siyo mwanadamu!”

23Herode hakumpa Mungu utukufu. Hivyo malaika wa bwana akampiga kwa ugonjwa. Akaliwa na minyoo ndani na kufa.

24Ujumbe wa Mungu ulikuwa unasambaa, ukiwafikia watu wengi zaidi.

25Baada ya Barnaba na Sauli kumaliza kazi yao Yerusalemu, walirudi Antiokia, walimchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International