Matendo 15

Matendo 15

Mkutano Yerusalemu

1Kisha baadhi ya watu kutoka Uyahudi wakaja Antiokia na kuanza kuwafundisha jamii ya waamini wasio Wayahudi, wakisema, “Hamwezi kuokolewa ikiwa hamkutahiriwa kama Musa alivyotufundisha.”

2Paulo na Barnaba wakayapinga mafundisho haya na wakahojiana na kubishana na watu hawa juu ya hili. Hivyo kundi la waamini likaamua kuwatuma Paulo, Barnaba, na baadhi ya watu wengine Yerusalemu ili kujadiliana na mitume na wazee kuhusu suala hili.

3Kanisa liliwapa wale waliotumwa kila kitu walichohitaji kwa ajili ya safari yao. Walisafiri kupitia maeneo ya Foeniki na Samaria, ambako walieleza kwa undani mambo yote namna ambavyo wasio Wayahudi wamemgeukia Mungu wa kweli. Habari hii iliwafurahisha waamini wote.

4Walipofika Yerusalemu, mitume, wazee na kanisa lote waliwakaribisha. Paulo, Barnaba, na wengine wakaeleza yote ambayo Mungu alitenda kupitia wao.

5Baadhi ya waamini mjini Yerusalemu waliokuwa Mafarisayo, walisimama na kusema, “Waamini wasio Wayahudi lazima watahiriwe. Ni lazima tuwaambie waitii Sheria ya Musa!”[#15:5 Mtu aliweza kuwa mfuasi wa Yesu na bado akawa Farisayo kama ambavyo baadaye Paulo katika kitabu anasema kuwa yeye ni Farisayo.]

6Ndipo mitume na wazee wakakusanyika kulichunguza jambo hili.

7Baada ya majadiliano ya muda mrefu, Petro akasimama na kuwaambia, “Ndugu zangu, nina uhakika mnakumbuka kilichotokea siku za nyuma. Mungu alinichagua kutoka miongoni mwenu kuzihubiri Habari Njema kwa watu wasio Wayahudi. Kupitia mimi walisikia Habari Njema na kuamini.

8Mungu anamfahamu kila mtu, hata mawazo yao, na amewakubali watu hawa wasio Wayahudi. Amelionyesha hili kwetu kwa kuwapa Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.

9Mbele za Mungu, wasio Wayahudi hawako tofauti na sisi. Mungu aliisafisha mioyo yao walipoamini.

10Kwa nini sasa mnawatwisha mzigo mzito kwenye shingo zao? Je! mnajaribu kumkasirisha Mungu? Sisi na baba zetu hatukuweza kuubeba mzigo huo.

11Hapana, tunaamini kuwa sisi na watu hawa tutaokolewa kwa namna moja iliyo sawa, ni kwa neema ya Bwana Yesu.”

12Ndipo kundi lote likawa kimya. Waliwasikiliza Paulo na Barnaba walipokuwa wanaeleza kuhusu ishara na maajabu ambayo kupitia wao Mungu aliwatendea watu wasio Wayahudi.

13Walipomaliza kusema, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni.

14Simoni Petro ametueleza namna ambavyo siku za mwanzoni Mungu alilionyesha pendo lake kwa watu wasio Wayahudi, kwa kuwakubali na kuwafanya kuwa watu wake.

15Maneno ya manabii yanakubaliana na hili:

16‘Nitarudi baada ya hili.

Nitaijenga nyumba ya Daudi tena.

Imeanguka chini.

Nitazijenga tena sehemu za nyumba yake zilizoangushwa chini.

Nitaifanya nyumba yake kuwa mpya.

17Kisha wanadamu wengine wote,

watu niliowachagua kutoka mataifa mengine,

watataka kunifuata mimi, Bwana.

Hivi ndivyo Bwana anasema,

naye ndiye anayefanya mambo haya yote.’

18‘Haya yote yalijulikana tangu zamani.’[#15:18 Tazama Isa 45:21.]

19Hivyo nadhani tusiyafanye mambo kuwa magumu kwa wasio Wayahudi waliomgeukia Mungu.

20Badala yake, tuwatumie barua kuwaambia mambo ambayo hawapaswi kutenda:

Wasile chakula kilichotolewa kwa sanamu maana chakula hiki huwa najisi.

Wasijihusishe na dhambi ya zinaa.

Wasile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.

21Wasitende mojawapo ya mambo haya, kwa sababu bado kuna watu katika kila mji wanaofundisha Sheria ya Musa. Maneno ya Musa yamekuwa yakisomwa katika masinagogi kila siku ya Sabato kwa miaka mingi.”

Barua kwa Waamini Wasio Wayahudi

22Mitume, wazee na kanisa lote wakataka kuwatuma baadhi ya watu wafuatane na Paulo na Barnaba kwenda Antiokia. Wakawachagua baadhi ya watu kutoka miongoni mwao wenyewe. Waliwachagua Yuda (ambaye pia aliitwa Barsaba) na Sila, watu walioheshimiwa na waamini.

23Kundi la waamini likaandika barua na kuwatuma watu hawa. Barua ilisema:

29Msile chakula kilichotolewa kwa sanamu.

Msile nyama inayotokana na wanyama walionyongwa au nyama ambayo bado ina damu ndani yake.

Msijihusishe na uzinzi.

30Hivyo Paulo, Barnaba, Yuda, na Sila waliondoka Yerusalemu na kwenda Antiokia. Walipofika huko walilikusanya kundi la waamini pamoja na wakawapa barua.

31Waamini walipoisoma, wakafurahi na kufarijika.

32Yuda na Sila ambao pia walikuwa manabii, waliwatia moyo waamini kwa maneno mengi na kuwafanya waimarike katika imani yao.

33Baada ya Yuda na Sila kukaa pale kwa muda, waliondoka. Waamini waliwaruhusu waende kwa amani kisha wakarudi Yerusalemu kwa wale waliowatuma.

35Lakini Paulo na Barnaba walikaa Antiokia. Wao na wengine wengi waliwafundisha waamini na kuwahubiri watu wengine Habari Njema kuhusu Bwana.

Paulo na Barnaba Watengana

36Wakati fulani baadaye, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi katika miji yote tulikowahubiri watu ujumbe wa Bwana. Tuwatembelee waamini tuone wanaendeleaje.”

37Barnaba alitaka Yohana Marko afuatane nao pia.

38Lakini Yohana Marko hakukaa nao mpaka mwisho katika safari ya kwanza. Aliwaacha Pamfilia. Hivyo Paulo alisisitiza kuwa wasiende pamoja naye wakati huu.

39Paulo na Barnaba walikuwa na mjadala mkali kuhusu hili. Ulikuwa mbaya sana ikabidi watengane na kwenda njia tofauti. Barnaba akatweka tanga kwenda Kipro, akamchukua Marko pamoja naye.

40Paulo alimchagua Sila kwenda naye. Waamini Antiokia walimweka Paulo katika uangalizi wa Bwana na kumtuma.

41Paulo na Sila walikwenda kwa kupitia katika majimbo ya Shamu na Kilikia, wakiyasaidia makanisa kuimarika.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International