Matendo 18

Matendo 18

Paulo Akiwa Korintho

1Baadaye, Paulo aliondoka Athene na kwenda katika mji wa Korintho.

2Akiwa huko alikutana na Myahudi aliyeitwa Akila, aliyezaliwa katika jimbo la Ponto. Lakini yeye na mke wake aliyeitwa Prisila, walikuwa tu ndiyo wamehamia Korintho kutoka Italia. Waliondoka Italia kwa sababu Kaisari Klaudio alikuwa ametoa amri Wayahudi wote waondoke Rumi. Paulo alikwenda kuwatembelea Akila na Prisila.

3Walikuwa watengenezaji wa mahema, kama alivyokuwa Paulo, hivyo alikaa na kufanya kazi pamoja nao.[#18:3 Au pengine “watengenezaji wa sehemu za kufanyia matukio”.]

4Kila siku ya Sabato Paulo alikwenda kwenye sinagogi na kuzungumza na Wayahudi na Wayunani, akijaribu kuwashawishi wamwamini Yesu.

5Lakini baada ya Sila na Timotheo kufika kutoka Makedonia, Paulo alitumia muda wake wote kuuhubiri ujumbe wa Mungu kwa Wayahudi, akiwaeleza kuwa Yesu ndiye Masihi.

6Lakini walimpinga Paulo na wakaanza kumtukana. Hivyo Paulo akakung'uta mavumbi kutoka kwenye nguo zake. Akawaambia, “Msipookolewa, itakuwa makosa yenu ninyi wenyewe! Nimefanya yote ninayoweza kufanya. Baada ya hili nitawaendea watu wasio Wayahudi tu.”[#18:6 Ishara ya onyo au tahadhari kuonesha kuwa Paulo alikuwa amemaliza kuzungumza na Wayahudi haya.]

7Paulo aliondoka katika sinagogi na kuhamia nyumbani kwa Tito Yusto, mtu aliyekuwa anamwabudu Mungu wa Kweli, nyumba yake ilikuwa jirani na sinagogi.

8Krispo aliyekuwa kiongozi wa sinagogi lile, pamoja na watu wote waliokuwa wanaishi nyumbani mwake walimwamini Bwana Yesu. Watu wengi katika mji wa Korintho walimsikiliza Paulo, wakaamini na wakabatizwa.

9Wakati wa usiku, Paulo aliona maono. Bwana alimwambia, “Usiogope, na usiache kuzungumza na watu.

10Niko pamoja nawe, na hakuna atakayeweza kukudhuru. Kuna watu wangu wengi katika mji huu.”

11Paulo alikaa pale kwa mwaka mmoja na nusu akiwafundisha watu ujumbe wa Mungu.

Paulo Afikishwa Mbele ya Galio

12Galio alipokuwa gavana wa Akaya, baadhi ya Wayahudi walikusanyika wakawa kinyume cha Paulo. Wakampeleka mahakamani.

13Wakamwambia Galio, “Mtu huyu anawafundisha watu kumwabudu Mungu kwa namna ambavyo ni kunyume na sheria yetu!”

14Paulo alikuwa tayari kuzungumza, lakini Galio aliwaambia Wayahudi, “Ningewasikiliza ikiwa malalamiko yenu yangehusu dhuluma au kosa jingine.

15Lakini yanahusu maneno na majina tu, mabishano yanayohusu sheria zenu wenyewe. Ni lazima mtatue tatizo hili ninyi wenyewe. Sitaki kuwa mwamuzi wa jambo hili.”

16Hivyo Galio akawafanya waondoke mahakamani.

17Kisha wote kwa pamoja wakamkamata Sosthenesi, kiongozi wa sinagogi. Wakampiga mbele ya mahakama. Lakini Galio hakulijali hili pia.

Paulo Arudi Antiokia

18Paulo alikaa na waamini kwa siku nyingi. Kisha aliondoka na kusafiri majini kwenda Shamu. Prisila na Akila walikuwa pamoja naye pia. Walipofika Kenkrea Paulo akanyoa nywele zake kwa sababu aliweka nadhiri kwa Mungu.[#18:18 Ilikuwa desturi ya Wayahudi kunyoa nywele wakati wa kuweka nadhiri. Ina maana ya kiapo cha kujiweka wakfu ama kufanya huduma maalumu kwa Mungu. Tazama katika Orodha ya Maneno.]

19Kisha walikwenda Efeso, ambako Paulo aliwaacha Prisila na Akila. Paulo alipokuwa Efeso alikwenda katika sinagogi na kuzungumza na Wayahudi.

20Walimwomba akae kwa muda mrefu lakini alikataa.

21Aliwaacha na kusema, “Nitarudi tena kwenu ikiwa Mungu atataka nirudi.” Na hivyo akaabili kwenda Efeso.

22Alipofika Kaisaria, alikwenda Yerusalemu na kulitembelea kanisa pale. Baada ya hapo alikwenda Antiokia.

23Alikaa Antiokia kwa muda kisha akaondoka akipita katika nchi za Galatia na Frigia. Alisafiri kutoka mji mmoja hadi mji mwingine katika mikoa hii, akiwasaidia wafuasi wa Yesu kuimarika katika imani yao.

Apolo Akiwa Efeso na Korintho

24Myahudi aliyeitwa Apolo alikuja Efeso. Alizaliwa katika mji wa Iskanderia, alikuwa msomi aliyeyajua Maandiko vizuri.

25Alikuwa amefundishwa kuhusu Bwana na daima alifurahia kuwaeleza watu kuhusu Yesu. Alichofundisha kilikuwa sahihi, lakini ubatizo alioufahamu ni ubatizo aliofundisha Yohana.[#18:25 Au “Alikuwa katika mito wa Roho Mtakatifu.”]

26Apolo alianza kuzungumza kwa ujasiri katika sinagogi. Prisila na Akila walipomsikia akizungumza, walimchukua wakaenda naye nyumbani mwao kisha wakamsaidia kuielewa njia ya Mungu vizuri zaidi.

27Apolo alitaka kwenda Akaya. Hivyo waamini wa Efeso wakamsaidia. Waliwaandikia barua wafuasi wa Bwana waliokuwa Akaya wakiwaomba wampokee Apolo. Alipofika pale, alikuwa msaada mkubwa kwa wale waliomwamini Yesu kwa sababu ya neema ya Mungu.

28Alibishana kwa ujasiri na Wayahudi mbele ya watu wote. Alithibitisha kwa uwazi kuwa wayahudi walikuwa wanakosea. Alitumia Maandiko kuonesha kuwa Yesu ndiye Masihi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International