The chat will start when you send the first message.
1Festo akawa gavana na siku tatu baadaye akasafiri kwenda Yerusalemu kutoka Kaisaria.
2Viongozi wa makuhani na viongozi maarufu wa Kiyahudi wakatoa mashitaka dhidi ya Paulo mbele ya Festo.
3Walimwomba Festo awasaidie. Walitaka amrudishe Paulo Yerusalemu kwa sababu walipanga kumwua akiwa njiani.
4Lakini Festo alijibu, “Hapana, Paulo ataendelea kuwekwa Kaisaria. Nitaenda huko mimi mwenyewe hivi karibuni,
5na viongozi wenu wanaweza kufuatana nami. Kama mtu huyu hakika amefanya chochote kibaya, wanaweza kumshitaki huko.”
6Festo alikaa Yerusalemu kwa siku nane au kumi zaidi kisha alirudi Kaisaria. Siku iliyofuata Festo akawaambia askari wamlete Paulo mbele yake. Festo alikuwa amekaa kwenye kiti cha hukumu.
7Paulo aliingia kwenye chumba na Wayahudi waliokuja kutoka Yerusalemu walisimama kumzunguka. Walileta mashitaka mengi mazito dhidi yake, lakini hawakuweza kuthibitisha chochote.
8Paulo alijitetea mwenyewe, akasema, “Sijatenda kitu chochote kibaya kinyume na sheria ya Kiyahudi, kinyume na Hekalu au kinyume na Kaisari.”
9Lakini Festo alitaka kuwaridhisha Wayahudi. Hivyo alimwuliza Paulo, “Unataka kwenda Yerusalemu ili nikakuhukumu huko kutokana na mashitaka haya?”
10Paulo akasema, “Kwa sasa nimesimama kwenye kiti cha hukumu cha Kaisari. Hapa ndipo ninatakiwa kuhukumiwa. Sijatenda lolote baya kwa Wayahudi na unafahamu hilo.
11Ikiwa nilitenda chochote kibaya na sheria inasema ni lazima nife, basi ninakubali kuwa ninapaswa kufa. Siombi kuokolewa kutokana na kifo. Lakini kama mashitaka haya siyo ya kweli, basi hakuna anayeweza kunikabidhi kwa watu hawa. Hapana, Nataka Kaisari aisikilize kesi yangu!”
12Festo alijadiliana na washauri wake kuhusu hili. Kisha akasema, “Umeomba kumwona Kaisari, basi utakwenda kwa Kaisari!”
13Siku chache baadaye Mfalme Agripa pamoja na dada yake aliyeitwa Bernike walikuja Kaisaria kumtembelea Festo.[#25:13 Dada yake Mfalme Agripa, binti mkubwa wa Herode Agripa wa Kwanza.]
14Walikaa huko kwa siku nyingi, na Festo akamwambia mfalme kuhusu kesi ya Paulo. Festo alisema, “Kuna mtu ambaye Feliki alimwacha gerezani.
15Nilipokwenda Yerusalemu, viongozi wa makuhani na viongozi wa wazee wa Kiyahudi walitengeneza mashitaka dhidi yake. Walinitaka nimhukumu kifo.
16Lakini niliwaambia, ‘Mtu anaposhitakiwa kuwa ametenda jambo baya, Warumi hawampeleki kwa watu wengine ili ahukumiwe. Kwanza, ni lazima aonane na watu wanaomshtaki. Na kisha ni lazima aruhusiwe kujitetea yeye mwenyewe dhidi ya mashitaka yao.’
17Hivyo Wayahudi walipokuja hapa kwa ajili ya kesi, sikupoteza muda. Siku iliyofuata nilikaa kwenye kiti cha hukumu na kuamuru Paulo aletwe ndani.
18Wayahudi walisimama na kumshitaki. Lakini hawakumshitaki kwa makosa niliyodhani wangemshitaki.
19Mashitaka yao yote yalihusu dini yao wenyewe na kuhusu mtu anayeitwa Yesu. Yesu alikufa lakini Paulo anasema bado yuko hai.
20Baada ya kuona kuwa sijui jinsi ya kuyachunguza mambo haya. Hivyo nilimwuliza Paulo, ‘Unataka kwenda Yerusalemu ili ukahukumiwe huko?’
21Lakini Paulo aliomba abaki mahabusu hapa Kaisaria. Anataka uamuzi kutoka kwa mfalme mkuu. Hivyo niliamua aendelee kushikiliwa hapa mpaka nitakapompeleka kwa Kaisari huko Rumi.”
22Agripa akamwambia Festo, “Ningependa kumsikiliza mtu huyu pia.”
Festo akasema, “Utaweza kumsikiliza kesho.”
23Siku iliyofuata Agripa na Bernike walikuja kwenye mkutano kwa fahari kubwa, wakijifanya watu wa muhimu sana. Waliingia kwenye chumba pamoja na viongozi wa kijeshi na watu maarufu wa mji. Festo akawaamuru askari wamwingize Paulo ndani.
24Festo akasema, “Mfalme Agripa nanyi nyote mliokusanyika hapa pamoja nasi, mnamwona mtu huyu. Wayahudi wote, hapa na Yerusalemu wamelalamika kwangu juu yake. Wanapolalamika, wanapaza sauti zao wakisema kwamba anapaswa kuuawa.
25Nilipochunguza, sikuona ikiwa alitenda kosa lolote linalostahili hukumu ya kifo. Lakini ameomba kuhukumiwa na Kaisari, hivyo niliamua apelekwe Rumi.
26Hata hivyo, sifahamu kwa hakika ni nini cha kumwandikia bwana wangu Kaisari kama sababu ya kumpeleka mtu huyu kwake. Hivo nimemleta mbele yenu ninyi nyote, hasa wewe, Mfalme Agripa. Ninatumaini kwamba utamwuliza maswali na kunipa kitu cha kumwandikia Kaisari.
27Nafikiri ni upumbavu kupeleka mfungwa kwa Kaisari bila kuainisha mashitaka dhidi yake.”