Matendo 26

Matendo 26

Paulo Asimama Mbele ya Mfalme Agripa

1Agripa akamwambia Paulo, “Unaweza sasa kujitetea wewe mwenyewe.” Paulo akanyoosha mkono wake ili wamsikilize kwa makini na akaanza kusema.[#26:1 Herode Agripa wa Pili, mjukuu wa herode Mkuu.]

2“Mfalme Agripa, najisikia heshima kusimama hapa mbele yako leo ili nijibu mashitaka yote yaliyotengenezwa na Wayahudi dhidi yangu.

3Ninafurahi kuzungumza nawe, kwa sababu unafahamu sana kuhusu desturi za Kiyahudi na mambo ambayo Wayahudi hubishana. Tafadhali uwe mvumilifu kunisikiliza.

4Wayahudi wote wanafahamu maisha yangu yote. Wanafahamu namna nilivyoishi tangu mwanzo miongoni mwa watu mwangu na baadaye Yerusalemu.

5Wayahudi hawa wamenifahamu kwa muda mrefu. Wakitaka wanaweza kukwambia kwamba nilikuwa Farisayo mzuri. Na Mafarisayo wanazitii sheria za dini ya Kiyahudi kwa uangalifu kuliko kundi lolote.

6Na sasa nimeshitakiwa kwa sababu ninatumaini ahadi ambayo Mungu aliiweka kwa baba zetu.

7Hii ni ahadi ambayo makabila yote kumi na mbili ya watu wetu yanatumaini kuipokea. Kwa sababu ya tumaini hili Wayahudi wanamtumikia Mungu usiku na mchana. Ee Mfalme wangu, Wayahudi wamenishitaki kwa sababu ninatumaini ahadi hii hii.

8Kwa nini ninyi watu mnadhani Mungu hawezi kuwafufua watu kutoka kwa wafu?

9Huko nyuma nilidhani kuwa ninapaswa kufanya kinyume na Yesu kutoka Nazareti kwa kadri ninavyoweza.

10Na ndivyo nilivyofanya, kuanzia Yerusalemu. Viongozi wa makuhani walinipa mamlaka ya kuwaweka gerezani watu wa Mungu wengi. Na walipokuwa wanauawa nilikubali kuwa lilikuwa jambo zuri.

11Nilikwenda katika masinagogi yote na kuwaadhibu, nikijaribu kuwafanya wamlaani Yesu. Hasira yangu dhidi ya watu hawa ilikuwa kali sana kiasi kwamba nilikwenda katika miji mingine kuwatafuta na kuwaadhibu.[#26:11 Kwa maana ya kawaida, “wamkufuru”, sawa na kusema hawataki kumwamini Yesu.]

Paulo Aeleza Alivyomwona Yesu

12Wakati fulani viongozi wa makuhani walinipa ruhusa na mamlaka kwenda katika mji wa Dameski.

13Nikiwa njiani, mchana, niliona mwanga kutoka mbinguni, unaong'aa kuliko jua. Uling'aa kunizunguka mimi pamoja na wale waliokuwa wanasafiri pamoja nami.

14Sote tulianguka chini. Kisha nilisikia sauti iliyozungumza nami kwa Kiaramu. Sauti ilisema, ‘Sauli, Sauli, kwa nini unanitesa? Unajiumiza wewe mwenyewe kwa kunipinga mimi.’

15Nilisema, ‘Wewe ni nani, Bwana?’

Bwana alisema, ‘Mimi ni Yesu. Unayemtesa.

16Simama! Nimekuchagua wewe kuwa mtumishi wangu. Utawaambia watu habari zangu, ulichoona leo na yale nitakayokuonesha. Hii ndiyo sababu nimekuja kwako.

17Nitakulinda dhidi ya watu wako na dhidi ya watu wasio Wayahudi, ninaokutuma kwao.

18Utawafanya waielewe kweli. Watatoka gizani na kuja kwenye mwanga. Watageuka kutoka kwenye mamlaka ya Shetani na kumgeukia Mungu. Ndipo dhambi zao zitasamehewa, na wataweza kupewa nafasi miongoni mwa watu wa Mungu, walifanywa watakatifu kwa kuniamini.’”

Paulo Aeleza Kuhusu Kazi Yake

19Paulo aliendelea kusema: “Mfalme Agripa, baada ya kuona maono haya kutoka mbinguni, nilitii.

20Nilianza kuwaambia watu kubadili mioyo na maisha yao na kumgeukia Mungu. Niliwaambia kufanya yale yatakayoonyesha kwamba hakika wamebadilika. Kwanza nilikwenda kwa watu waliokuwa Dameski. Kisha nikaenda Yerusalemu na kila sehemu ya Uyahudi na nikawaambia watu huko. Nilikwenda pia kwa watu wasio Wayahudi.

21Hii ndiyo sababu Wayahudi walinikamata na kujaribu kuniua Hekaluni.

22Lakini Mungu alinisaidia, na bado ananisaidia leo. Kwa msaada wa Mungu nimesimama hapa leo na kuwaambia watu kile nilichokiona. Lakini sisemi chochote kipya. Ninasema kile ambacho Musa na manabii walisema kingetokea.

23Walisema kwamba Masihi atakufa na kuwa wa kwanza kufufuka kutoka kwa wafu. Walisema kwamba ataleta mwanga wa kweli ya Mungu inayowaokoa wote, Wayahudi na wasio Wayahudi.”[#26:23 Kwa maana ya kawaida, “kutangaza mwanga”.]

Paulo Ajaribu Kumshawishi Agripa

24Paulo alipokuwa bado anajitetea, Festo alipaza sauti akasema, “Paulo, umerukwa na akili! Kusoma kwingi kumekufanya kichaa.”

25Paulo akasema, “Mheshimiwa Festo, mimi si kichaa. Ninachokisema ni kweli na kinaingia akilini.

26Mfalme Agripa analifahamu hili, na ninaweza kuzungumza naye kwa uhuru. Ninafahamu kwamba amekwisha kusikia kuhusu mambo haya, yalitokea mahali ambako kila mtu aliyaona.

27Mfalme Agripa, unaamini yale ambayo manabii waliandika? Ninajua unaamini!”

28Mfalme Agripa akamwambia Paulo, “Unadhani unaweza kunishawishi kirahisi kiasi hicho ili niwe Mkristo?”

29Paulo akasema, “Haijalishi kwangu, ikiwa ni vigumu au rahisi. Ninaomba tu kwa Mungu kwamba si wewe peke yako lakini kila mtu anayenisikiliza leo angeokolewa ili awe kama mimi, isipokuwa kwa minyororo hii!”

30Mfalme Agripa, Gavana Festo, Bernike, na watu wote waliokaa pamoja nao wakasimama

31na kuondoka chumbani. Walikuwa wanaongea wenyewe. Walisema, “Mtu huyu hajafanya chochote kinachostahili kuuawa au kuwekwa gerezani.”

32Kisha Agripa akamwambia Festo, “Tungemwachia huru, lakini ameomba kumwona Kaisari.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International