Matendo 8

Matendo 8

1-2-3Sauli aliridhia kuwa kuuawa kwa Stefano lilikuwa jambo jema. Baadhi ya wacha Mungu walimzika Stefano, wakaomboleza na kumlilia kwa sauti kuu.

Matatizo Kwa waamini

Kuanzia siku hiyo Wayahudi walianza kulitesa sana kanisa na waamini katika mji wa Yerusalemu. Sauli pia alijaribu kuliharibu kanisa. Aliingia katika nyumba za waamini, akawaburuta wanaume na wanawake, na kuwafunga gerezani. Waamini wote walikimbia kutoka Yerusalemu, mitume peke yao ndiyo walibaki. Waamini walikwenda mahali tofauti tofauti katika Uyahudi na Samaria.

4Walitawanyika kila mahali, na kila walikokwenda waliwahubiri watu Habari Njema.

Filipo Ahubiri Katika Samaria

5Filipo alikwenda katika mji mkuu wa jimbo la Samaria na kuwahubiri watu kuhusu Masihi.[#8:5 Siyo mtume aliyeitwa Filipo.]

6Watu wa Samaria walimsikiliza Filipo na kuona miujiza aliyotenda. Wote walisikiliza kwa makini yale aliyosema.

7Watu wengi miongoni mwao walikuwa na mapepo, lakini Filipo aliyakemea mapepo na yaliwatoka watu. Mapepo yalipiga kelele nyingi yalipokuwa yanawatoka watu. Walikuwepo pia watu wengi waliopooza na walemavu wa miguu pale. Filipo aliwaombea na wote walipona.

8Kulikuwa furaha kubwa katika mji ule wa Samaria siku ile!

9Mtu mmoja aliyeitwa Simoni alikuwa anaishi katika mji huo. Kabla Filipo hajaenda huko, Simoni alikuwa akifanya uchawi na kuwashangaza watu wote wa Samaria. Alijigamba na kujiita mtu mkuu.

10Watu wote, kuanzia mdogo hadi mkubwa, waliamini yale aliyosema Simoni. Walisema, “Mtu huyu ndiye anayeitwa ‘Nguvu Kuu ya Mungu.’”

11Simoni aliwashangaza watu kwa muda mrefu kwa uchawi wake na watu wote wakawa wafuasi wake.

12Lakini Filipo alipowahubiri watu Habari Njema kuhusu Ufalme wa Mungu na Nguvu za Yesu Kristo. Wanaume na wanawake waliamini alichosema Filipo na wakabatizwa.

13Simoni mwenyewe aliamini, na baada ya kubatizwa, alikaa karibu na Filipo. Alipoona miujiza na matendo makuu ya ajabu yaliyofanyika kupitia Filipo, alishangaa.

14Mitume mjini Yerusalemu, waliposikia kuwa watu wa Samaria wameupokea Ujumbe wa Mungu, waliwatuma Petro na Yohana kwenda kwa watu wa Samaria.

15Petro na Yohana walipofika, waliomba ili Roho Mtakatifu awashukie waamini wa Samaria.

16Watu hawa walikuwa wamebatizwa katika jina la Bwana Yesu, lakini Roho Mtakatifu alikuwa bado hajamshukia hata mmoja wao. Na hii ndiyo sababu Petro na Yohana waliomba.

17Mitume hawa wawili walipoweka mikono yao juu ya watu, Roho Mtakatifu aliwashukia.

18Simoni aliyekuwa mchawi alipoona Roho Mtakatifu anatolewa kwa watu kwa kuweka mikono juu yao. Aliwapa pesa mitume.

19Akasema, “Nipeni na mimi nguvu hii ili nitakapoweka mikono yangu juu ya mtu yeyote, atampata Roho Mtakatifu.”

20Petro akamwambia Simoni, “Wewe pamoja na pesa zako mwangamie kwa sababu unadhani unaweza kununua karama kutoka kwa Mungu kwa pesa.

21Huwezi kushirikiana nasi katika kazi hii. Moyo wako si safi mbele za Mungu.

22Badili moyo wako! Achana na mawazo haya maovu na umwombe Bwana. Yumkini atakusamehe!

23Kwa kuwa ninaona umejaa wivu mwingi nawe ni mfungwa wa uovu.”

24Simoni akajibu, “Niombeeni kwa Bwana, ili haya uliyosema yasinipate.”

25Ndipo wale mitume wawili waliwaambia watu waliyoona Yesu akitenda. Wakawaambia ujumbe wa Bwana. Kisha wakarudi Yerusalemu. Wakiwa njiani kurudi, walipitia katika miji mingi ya Wasamaria na kuwahubiri watu Habari Njema.

Filipo Amfundisha Mtu Kutoka Ethiopia

26Malaika wa Bwana alimwambia Filipo, “Jiandae na uende kusini katika barabara ya jangwani inayoteremka kutoka Yerusalemu kwenda Gaza.”

27Filipo alijiandaa na kwenda. Akiwa njiani alimwona mwanaume kutoka Ethiopia. Alikuwa towashi na ofisa muhimu wa Kandake, malkia wa Ethiopia. Alikuwa na mweka hazina mkuu wa malkia. Mtu huyu alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu.

28Na alikuwa anarudi Ethiopia. Alikuwa ameketi katika gari lake la kukokotwa na farasi akiwa anasoma kitabu cha nabii Isaya.

29Roho Mtakatifu akamwambia Filipo, “Nenda kwenye gari hilo na uwe karibu yake.”

30Hivyo Filipo akaenda karibu na gari, akamsikia mtu yule akisoma kutoka katika kitabu cha nabii Isaya. Filipo akamwuliza, “Unaelewa unachosoma?”

31Yule mtu akajibu, “Nitaelewaje? Ninahitaji mtu wa kunifafanulia.” Ndipo akamwomba Filipo apande garini na aketi pamoja naye.

32Sehemu ya Maandiko aliyokuwa anasoma ilikuwa hii:

“Alikuwa kama kondoo

anayepelekwa kwa mchinjaji.

Alikuwa kama mwana kondoo asivyopiga kelele

anapokatwa manyoya yake.

Hakusema kitu.

33Alidhalilishwa,

na kunyimwa haki zake zote.

Maisha yake duniani yamekoma.

Hivyo hakutakuwa simulizi yoyote kuhusu wazaliwa wake.”

34Afisa akamwambia Filipo, “Tafadhali niambie, nabii anazungumza kuhusu nani? Anazungumza kuhusu yeye mwenyewe au mtu mwingine?”[#8:34 Kwa maana ya kawaida, “towashi”. Pia katika mstari wa 36,38,39.]

35Filipo akaanza kuzungumza. Alianzia na Andiko hili na kumwambia mtu yule Habari Njema kuhusu Yesu.

36Walipokuwa wanasafiri waliyakuta maji mahali fulani. Afisa akasema, “Tazama! Hapa kuna maji! Nini kinanizuia nisibatizwe?”

38Ndipo Afisa akaamuru gari lake lisimame. Wote wawili, Filipo na Afisa, wakatelemka wakaingia kwenye maji na Filipo akambatiza towashi.

39Walipotoka kwenye maji, Roho wa Bwana akamchukua Filipo; afisa hakumwona Filipo tena. Afisa aliendelea na safari yake kurudi nyumbani, akiwa mwenye furaha sana.

40Lakini Filipo alionekana katika mji ulioitwa Azoto. Alikuwa akienda kwenye mji wa Kaisaria. Aliwahubiri watu Habari Njema katika miji yote wakati anasafiri kutoka Azoto kwenda Kaisaria.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International