Waefeso 3

Waefeso 3

Huduma ya Paulo kwa Wasio Wayahudi

1Hivyo, mimi Paulo ni mfungwa kwa sababu ninamtumikia Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi msio Wayahudi.

2Mnajua hakika ya kuwa Mungu alinipa kazi hii kupitia neema yake ili niwasaidie.

3Mungu alinionyesha na nikaweza kuujua mpango wake wa siri. Nimekwisha kuandika kiasi fulani juu ya hili.

4Na ikiwa mtasoma nilichowaandikia, mtajua kuwa ninaielewa siri ya kweli kuhusu Kristo.

5Watu walioishi zamani hawakuambiwa siri hiyo. Lakini sasa, kupitia Roho, Mungu amewawezesha mitume na manabii wake watakatifu kuijua siri hiyo.

6Na siri hiyo ni hii: Kwa kuikubali Habari Njema, wale wasio Wayahudi watashiriki pamoja na Wayahudi katika baraka alizonazo Mungu kwa ajili ya watu wake. Wao ni sehemu ya mwili mmoja, na wanashiriki manufaa ya ahadi ambayo Mungu aliitimiza kupitia Kristo Yesu.

7Kwa kipawa cha neema ya Mungu, nilifanywa mtumishi wa kuihubiri Habari Njema. Alinipa neema hiyo kwa nguvu zake.

8Mimi nisiye na umuhimu zaidi miongoni mwa watu wa Mungu. Lakini alinipa kipawa hiki cha kuwahubiri wasio Wayahudi Habari Njema kuhusu utajiri alionao Kristo. Utajiri huu ni mkuu na si rahisi kuuelewa kikamilifu.

9Pia Mungu alinipa kazi ya kuwaambia watu kuhusu mpango wa siri yake ya kweli. Aliificha siri hii ya kweli ndani yake tangu mwanzo wa nyakati. Ndiye aliyeumba kila kitu.

10Lengo lake lilikuwa kwamba watawala wote na mamlaka zote zilizo mbinguni zijue njia nyingi anazotumia kuionesha hekima yake. Watalijua hili kwa sababu ya kanisa.

11Hii inaendana na mpango aliokuwa nao Mungu tangu mwanzo wa nyakati. Alitekeleza mpango wake kupitia Kristo Yesu Bwana wetu.

12Kwa kuwa tu wake Kristo tunakuja mbele za Mungu tukiwa huru bila woga. Tunaweza kufanya hivi kwa sababu ya uaminifu wake Kristo.[#3:12 Au “kwa sababu ya imani katika Kristo”.]

13Hivyo ninawaomba msikate tamaa kutokana na yale yanayonipata. Mateso yangu ni faida kwenu, na pia ni kwa ajili ya heshima na utukufu wenu.

Upendo wa Kristo

14Hivyo ninapiga magoti nikimwomba Baba.

15Ambaye katika yeye kila familia iliyoko mbinguni na duniani inapewa jina.

16Ninamwomba Baba kwa kadri ya utajiri wa utukufu wake awajaze nguvu za ndani kwa nguvu za Roho wake.

17Ninaomba kwamba Kristo aishi katika mioyo yenu kwa sababu ya imani yenu. Ninaomba maisha yenu yawe na mizizi mirefu na misingi imara katika upendo.

18Na ninaomba ili ninyi na watakatifu wote wa Mungu muwe na uwezo wa kuuelewa upana, urefu, kimo na kina cha ukuu wa upendo wa Kristo.

19Upendo wa Kristo ni mkuu kuliko namna ambavyo mtu yeyote anaweza kujua, lakini ninawaombea ili mweze kuujua. Ndipo mtajazwa kwa kila kitu alichonacho Mungu kwa ajili yenu.

20Tukiwa na nguvu za Mungu zinazotenda kazi ndani yetu, anaweza kufanya zaidi, zaidi ya kila kitu tunachoweza kuomba au kufikiri.

21Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu kila wakati, milele na milele. Amina.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International