Waebrania 13

Waebrania 13

Ibada Inayompendeza Mungu

1Endeleeni kupendana ninyi kwa ninyi kama kaka na dada katika Kristo.

2Mkikumbuka kuwasaidia watu kwa kuwakaribisha majumbani mwenu. Watu wengine wamefanya hivyo na wakawa wamewasaidia malaika pasipo wao kujua.

3Msiwasahau wale walioko magerezani. Wakumbukeni kama vile mko magerezani pamoja nao. Na msiwasahau wale wanaoteseka. Wakumbukeni kama vile mnateseka pamoja nao.

4Ndoa iheshimiwe na kila mmoja. Na kila ndoa itunzwe kwa usafi kati ya mume na mke. Mungu atawahukumu kuwa na hatia wale wanaofanya uzinzi na uasherati.

5Yatunzeni maisha yenu yawe huru kutokana na kupenda fedha. Na mridhike na kile mlichonacho. Mungu amesema: “Sitakuacha kamwe; Sitakukimbia kamwe.”[#Kum 31:6]

6Hivyo tunaweza kuwa na uhakika na kusema:

“Bwana ndiye msaidizi wangu;

Sitaogopa.

Watu hawawezi kunifanya chochote.”

7Wakumbukeni viongozi wenu. Waliwafundisha ujumbe wa Mungu. Kumbukeni jinsi walivyoishi na walivyokufa, na muiige imani yao.

8Yesu Kristo ni yeye yule jana, leo na hata milele.

9Msiruhusu aina yoyote ya mafundisho mageni yawaongoze hadi katika njia isiyo sahihi. Itegemeeni neema ya Mungu pekee kwa ajili ya nguvu za kiroho, siyo katika sheria kuhusu vyakula. Kuzitii sheria hizi hakumsaidii yeyote.

10Tunayo sadaka. Na wale makuhani waliotumika ndani ya Hema Takatifu hawawezi kula sadaka tuliyo nayo.

11Kuhani mkuu hubeba damu za wanyama hadi Patakatifu pa Patakatifu na hutoa damu hiyo kwa ajili ya dhambi. Lakini miili ya wanyama hao huchomwa nje ya kambi.

12Hivyo Yesu naye alitesekea nje ya mji. Alikufa ili awatakase watu wake kwa damu yake mwenyewe.

13Hivyo tumwendee Yesu nje ya kambi na kuikubali aibu hiyo hiyo aliyoipata yeye.

14Hatuna mji unaodumu milele hapa duniani. Lakini tunaungoja mji tutakaoupata hapo baadaye.

15Hivyo kwa njia ya Yesu hatupaswi kuacha kumtolea Mungu sadaka zetu. Dhabihu hizo ni sifa zetu, zinazotoka katika vinywa vyetu vinavyolisema jina lake.

16Na msisahau kutenda mema na kushirikishana na wengine mlivyo navyo, kwa sababu sadaka kama hizi zinamfurahisha sana Mungu.

17Muwatii viongozi wenu. Muwe tayari kufanya yale wanayowaambia. Wanawajibika katika maisha yenu ya kiroho, hivyo nyakati zote wanaangalia jinsi ya kuwalinda ninyi. Muwatii ili kazi yao iwafurahishe wao, siyo kupata majonzi. Haitawasaidia ninyi mnapowasababishia matatizo.

18Endeleeni kutuombea. Tunajisikia tuko sahihi katika tunayoyafanya, kwa sababu nyakati zote tunajitahidi kadri tuwezavyo.

19Na nawasihi muombe ili Mungu anirudishe tena kwenu mapema. Nalitamani sana hili kuliko kitu chochote.

20-21Ninawaombea Mungu wa amani awape ninyi mambo mazuri mnayohitaji ili muweze kufanya anayoyapenda. Mungu ndiye aliyemfufua Bwana Yesu kutoka katika kifo, Mchungaji Mkuu wa kondoo wake. Alimfufua kwa sababu Yesu aliitoa sadaka ya damu yake ili kulianza agano jipya lisilo na mwisho. Namwomba Mungu atuwezeshe kwa njia ya Yesu Kristo kufanya mambo yanayompendeza yeye. Utukufu ni wake milele. Amina.

22Ndugu na dada zangu, nawasihi msikilize kwa uvumilivu katika yale niliyoyasema. Niliandika barua hii ili kuwatia moyo. Na siyo ndefu sana.

23Nawataka mjue kwamba ndugu yetu Timotheo ametoka gerezani. Akija kwangu mapema, sote tutakuja kuwaona ninyi.

24Fikisheni salama zangu kwa viongozi wote na kwa watu wote wa Mungu. Wote walioko Italia wanawasalimuni.

25Naomba neema ya Mungu iwe nanyi nyote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International