Waebrania 7

Waebrania 7

Kuhani Melkizedeki

1Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na kuhani wa Mungu Aliye Juu. Alikutana na Abrahamu wakati Abrahamu alipokuwa akirudi baada ya kuwashinda wafalme. Siku hiyo Melkizedeki alimbariki Abrahamu.

2Kisha Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya kila kitu alichokuwa nacho.

Jina Melkizedeki, mfalme wa Salemu, lilikuwa na maana mbili. Kwanza, Melkizedeki inamaanisha “mfalme wa haki.” Na “mfalme wa Salemu” inamaanisha “mfalme wa amani.”

3Hakuna ajuaye baba na mama yake walikuwa ni kina nani au walitokea wapi. Na hakuna ajuaye alizaliwa lini au alikufa lini. Melkizedeki ni kama Mwana wa Mungu kwa vile siku zote atakuwa kuhani.[#7:3 Kwa maana ya kawaida, “Melkizedeki hakuwa na baba, hakuwa na mama, hakuwa na historia ya ukoo.”]

4Unaweza kuona kuwa Melkizedeki alikuwa mkuu sana. Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa yeye sehemu ya kumi ya kila alichoshinda kule vitani.

5Sasa sheria inasema kwamba wale wa ukoo wa Lawi waliokuja kuwa makuhani wanastahili kupata sehemu ya kumi kutoka kwa watu wao, hata kama wao na watu wao ni wa familia ya Abrahamu.

6Melkizedeki wala hakutoka katika kabila la Lawi, lakini Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya alivyokuwa navyo. Na Melkizedeki akambariki Abrahamu yule aliyekuwa na ahadi za Mungu.

7Na kila mtu anajua kwamba mtu aliye wa muhimu zaidi humbariki mtu yule ambaye ana umuhimu mdogo.

8Makuhani hawa hupata sehemu ya kumi, lakini wao ni binadamu tu wanaoishi kisha hufa. Lakini Melkizedeki, aliyepata sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu, anaendelea kuishi, kama Maandiko yanavyosema.

9Sasa wale wa kutoka ukoo wa Lawi ndiyo wanaopata sehemu ya kumi kutoka kwa watu. Lakini tunaweza kusema kuwa Abrahamu alipompa Melkizedeki sehemu ya kumi, kisha Lawi naye akatoa.

10Lawi alikuwa bado hajazaliwa, lakini alikuwepo katika baba yake Abrahamu wakati Melkizedeki alipokutana naye.

11Watu walipewa sheria chini ya mfumo wa makuhani waliotoka katika ukoo wa Lawi. Lakini hayupo awezaye kufanywa mkamilifu kiroho kwa njia ya mfumo wa makuhani. Hivyo lilikuwepo hitaji la kuhani mwingine kuja. Namaanisha kama Melkizedeki, siyo Haruni.

12Na anapokuja kuhani wa aina nyingine, basi sheria pia inabidi ibadilishwe.

13-14Tunazungumza juu ya Bwana Yesu, aliyetoka katika kabila lingine. Hakuwepo yeyote kutoka katika kabila hilo kamwe aliyeweza kutumika kama kuhani madhabahuni. Ni dhahiri kwamba Bwana Yesu alitoka katika kabila la Yuda. Na Musa hakusema chochote kuhusu makuhani waliyetokana na kabila hilo.

Yesu Ni Kuhani Mfano wa Melkizedeki

15Na mambo haya yalizidi kuwa wazi zaidi tunapomwona kuhani mwingine aliye kama Melkizedeki.

16Alifanywa kuhani, lakini siyo kwa sababu alikamilisha mahitaji ya kuzaliwa katika familia sahihi. Alifanyika kuhani kwa nguvu ya uhai ambayo haitakwisha.

17Hivi ndivyo Maandiko yanavyosema kumhusu yeye: “Wewe ni kuhani milele, kama alivyokuwa Melkizedeki.”[#Zab 110:4]

18Hivyo mfumo wa sheria za zamani zilizowekwa sasa zinaisha kwa sababu zilikuwa dhaifu na hazikuweza kutusaidia.

19Sheria ya Musa haikuweza kukamilisha kitu chochote. Lakini sasa tumaini bora zaidi limeletwa kwetu. Na kwa tumaini hilo tunaweza kumkaribia Mungu.

20Vile vile, ni muhimu kwamba Mungu aliweka ahadi kwa kiapo alipomfanya Yesu kuwa kuhani mkuu. Watu hawa wengine walipofanyika makuhani, hapakuwepo kiapo.

21Lakini Yesu akafanyika kuhani kwa kiapo cha Mungu. Mungu alimwambia:

“Bwana anaweka ahadi kwa kiapo

naye hatabadili mawazo yake:

‘Wewe ni kuhani milele.’”

22Hivyo hii inamaanisha kwamba Yesu ni uhakika wa agano zuri zaidi kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watu wake.

23Pia, mmoja wa hawa makuhani wengine alipofariki, asingeendelea kuwa kuhani. Hivyo walikuwepo makuhani wengi wa jinsi hii.

24Lakini Yesu anaishi milele. Hatakoma kufanya kazi kama kuhani.

25Hivyo anaweza kuwaokoa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake. Yesu anaweza kufanya hivi milele, kwa sababu anaishi siku zote na yuko tayari kuwasaidia watu wanapomjia Mungu.

26Hivyo Yesu ni aina ya kuhani mkuu tunayemhitaji. Yeye ni mkamilifu. Hana dhambi ndani yake. Hana kasoro na havutwi na watenda dhambi. Naye amepandishwa juu ya mbingu.

27Hayuko sawa na hawa makuhani wengine. Walitakiwa kutoa sadaka kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zao wenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Lakini Yesu hahitaji kufanya hivyo. Alitoa sadaka moja tu kwa ajili ya nyakati zote. Alijitoa mwenyewe.

28Sheria huchagua makuhani wakuu ambao ni watu na wanao udhaifu ule ule ambao watu wote wanao. Lakini baada ya sheria, Mungu alisema kiapo ambacho kilimfanya Mwana awe kuhani mkuu. Na Mwana huyo, aliyekamilishwa kwa njia ya mateso, atatumika kama kuhani mkuu milele yote.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International