Waebrania 8

Waebrania 8

Yesu Kuhani Wetu Mkuu

1Hii ndiyo hoja tunayosema: Tunaye kuhani mkuu wa jinsi hiyo, anayeketi upande wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu Mkuu mbinguni.[#8:1 Mahali pa heshima na mamlaka (nguvu).]

2Kuhani wetu mkuu anahudumia katika Patakatifu pa Patakatifu. Anahudumia katika mahali pa hakika kwa ibada palipotengenezwa na Bwana, siyo na mtu yeyote duniani.[#8:2 Kwa maana ya kawaida, “patakatifu” kwa “Patakatifu pa patakatifu”, mahali pa kiroho ambapo Mungu anaishi na anaabudiwa. Mahali hapa pa kiroho kiliwakilishwa na chumba ndani ya Hema Takatifu katika Agano la Kale. Tazama na katika Orodha ya Maneno.; #8:2 Kwa maana ya kawaida, “Hema ya kuabudia” au “hema”.]

3Kila kuhani mkuu anayo kazi ya kutoa sadaka na sadaka kwa Mungu. Hivyo kuhani wetu mkuu pia anahitajika kutoa kitu kwa Mungu.

4Kama kuhani wetu mkuu angekuwa anaishi duniani, asingekuwa kuhani. Nasema hivi kwa sababu tayari hapa wapo makuhani ambao wanafuata sheria kwa kutoa sadaka kwa Mungu.

5Kazi ambayo makuhani hawa wanafanya hakika ni nakala tu na kivuli cha yaliyoko mbinguni. Ndiyo sababu Mungu alimwonya Musa alipokuwa amejiandaa kujenga Hema Takatifu: “Uwe na uhakika kufanya kila kitu sawasawa na kielelezo nilichokuonesha kule mlimani.”[#Kut 25:40]

6Lakini kazi ambayo tayari imetolewa kwa Yesu ni kuu zaidi ya kazi iliyotolewa na makuhani hao. Kwa jinsi hiyo hiyo, agano jipya ambalo Yesu alilileta kutoka kwa Mungu kuja kwa watu wake ni kuu zaidi kuliko lile la zamani. Na agano jipya limeelemea katika ahadi bora zaidi.

7Kama kusingekuwa na makosa katika agano la kwanza, kisha kusingekuwa na haja ya agano la pili.

8Lakini Mungu aligundua kitu kilichokuwa na kasoro kwa watu, akasema:

“Wakati unakuja, asema Bwana,

nitakapofanya agano jipya na watu wa Israeli na watu wa Yuda.

9Halitakuwa sawa na agano lililotengenezwa na baba zao.

Hilo ni agano nililowapa nilipowachukua kwa mkono na kuwatoa Misri.

Hawakuendelea kufuata agano nililowekeana nao,

na nikageuka mbali nao, asema Bwana.

10Hili ni agano jipya nitakalofanya

na watu wa Israeli siku zinazokuja, asema Bwana:

Nitaziweka sheria zangu katika fahamu zao,

na nitaandika sheria zangu katika mioyo yao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

11Hakuna tena atakayemfundisha jirani yake au familia yake kumjua Bwana.

Watu wote, wakuu zaidi na wasio na umuhimu kabisa, watanijua.

12Na nitawasamehe makosa waliyotenda,

na sitazikumbuka dhambi zao.”

13Mungu aliliita hili ni agano jipya, hivyo amelifanya agano la kwanza kuwa la zamani. Na chochote kilicho cha zamani na kisichokuwa na matumizi kiko tayari kutoweka.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International