Mathayo 28

Mathayo 28

Yesu Amefufuka Kutoka Mauti

(Mk 16:1-8; Lk 24:1-12; Yh 20:1-10)

1Alfajiri mapema siku iliyofuata baada ya siku ya Sabato, yaani siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalena na mwanamke mwingine aliyeitwa Mariamu alikwenda kuliangalia kaburi.

2Ghafla malaika wa Bwana akaja kutoka mbinguni, na tetemeko kubwa likatokea. Malaika alikwenda kaburini na kulivingirisha jiwe kutoka kwenye mlango wa kaburi. Kisha akaketi juu ya jiwe.

3Malaika alikuwa anang'aa kama miali ya radi. Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji.

4Askari waliokuwa wanalinda kaburi walimwogopa sana malaika, walitetemeka kwa woga na wakawa kama watu waliokufa.

5Malaika akawaambia wale wanawake, “Msiogope. Ninajua mnamtafuta Yesu, aliyeuawa msalabani.

6Lakini hayupo hapa. Amefufuka kutoka kwa wafu, kama alivyosema. Njooni mwone mahali ulipokuwa mwili wake.

7Nendeni haraka mkawaambie wafuasi wake, ‘Yesu amefufuka kutoka kwa wafu. Amekwenda Galilaya na atafika huko kabla yenu. Na mtamwona huko.’” Kisha malaika akasema, “Sasa nimewaambia.”

8Hivyo wanawake wakaondoka haraka kaburini. Waliogopa sana, lakini walijawa na furaha. Walipokuwa wanakimbia kwenda kuwaambia wafuasi wake kilichotokea,

9ghafla Yesu alisimama mbele yao. Akasema, “Salamu!” Wanawake wakamwendea wakamshika miguu na wakamwabudu.

10Kisha Yesu akawaambia, “Msiogope. Nendeni mkawaambie wafuasi wangu waende Galilaya, wataniona huko.”[#28:10 Kwa maana ya kawaida, “ndugu zangu”.]

Taarifa ya Kufufuka Yesu Yawafikia Viongozi wa Kiyahudi

11Wanawake wakaenda kuwaambia wafuasi. Na wakati huo huo baadhi ya askari waliokuwa wanalinda kaburi waliingia mjini. Walikwenda kuwaambia viongozi wa makuhani kila kitu kilichotokea.

12Ndipo makuhani wakakutana na viongozi wazee wa Kiyahudi na kufanya mpango. Wakawalipa wale askari pesa nyingi

13na kuwaambia, “Waambieni watu kuwa wafuasi wake walikuja usiku na kuuiba mwili mlipokuwa mmesinzia.

14Gavana atakaposikia juu ya hili, tutazungumza naye ili msiadhibiwe.”

15Hivyo wale askari wakachukua pesa na kuwatii makuhani. Na jambo hili bado linasambaa miongoni mwa Wayahudi hata hivi leo.[#28:15 Uongo kuwa mwili wa Yesu uliibwa usiku na wafuasi wake.]

Yesu Awatokea Wafuasi Wake

(Mk 16:9-18; Lk 24:36-49; Yh 20:19-23; Mdo 1:6-8)

16Wale wafuasi kumi na mmoja walikwenda Galilaya, kwenye mlima ambao Yesu aliwaambia waende.

17Wakiwa mlimani, wafuasi wale walimwona Yesu na wakamwabudu. Lakini baadhi ya wafuasi hawakuwa na uhakika kama alikuwa Yesu.

18Kisha Yesu akawajia na akasema, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.

19Hivyo nendeni ulimwenguni kote mkawafanye watu kuwa wafuasi wangu. Mkiwabatiza katika jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.

20Wafundisheni kutii kila kitu nilichowaambia. Na tambueni hili: Niko pamoja nanyi daima. Na nitaendelea kuwa pamoja nanyi hata mwisho wa wakati.”

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International