Ufunuo 12

Ufunuo 12

Joka na Mwanamke Anayezaa

1Jambo la ajabu lilionekana mbinguni: Mwanamke aliyevalishwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake alionekana. Alikuwa na taji yenye nyota kumi na mbili kichwani pake.

2Alikuwa na mimba na alilia kwa uchungu kwa sababu alikuwa karibu ya kuzaa.

3Kisha ajabu nyingine ikaonekana mbinguni: Alikuweko huko joka mkubwa mwekundu. Joka huyo alikuwa na vichwa saba na alikuwa na taji juu ya kila kichwa. Na alikuwa na pembe kumi.

4Mkia wake ulizoa theluthi ya nyota na kuziangusha duniani. Joka hili lilisimama mbele ya mwanamke aliyekuwa karibu ya kuzaa mtoto. Lilitaka kumla mtoto mara atakapozaliwa.

5Mwanamke alimzaa mtoto wa kiume, atakayewatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya chuma. Na mwana wa mwanamke huyu alichukuliwa juu mbinguni kwa Mungu, kwenye kiti chake cha enzii.

6Mwanamke alikimbilia jangwani mpaka mahali ambako Mungu amemwandalia. Huko angetunzwa kwa siku 1,260.

7Kisha kulikuwa vita mbinguni. Mikaeli na malaika zake walipigana na joka. Nalo joka na malaika zake wakapigana na Mikaeli pamoja na malaika zake,[#12:7 Malaika mkuu ambaye ni kiongozi wa malaika wa Mungu. Tazama Yud 9.]

8lakini joka na malaika zake hawakuwa na nguvu za kutosha kushinda, na hivyo wakapoteza nafasi zao mbinguni.

9Likatupwa chini kutoka mbinguni. (Joka hili kubwa ni nyoka yule wa zamani, aitwaye Ibilisi au Shetani, anayeudanganya ulimwengu wote.) Joka na malaika zake walitupwa duniani.

10Kisha nilisikia sauti kubwa mbinguni ikisema:

“Ushindi na uweza na ufalme wa Mungu wetu

na mamlaka ya Masihi wake umekuja sasa,

kwa sababu mshitaki wa kaka na dada zetu

ametupwa chini.

Ndiye aliyewashitaki kwa Mungu,

mchana na usiku.

11Walimshinda kwa sadaka ya damu ya Mwanakondoo

na kwa ujumbe wa Mungu waliowaambia watu.

Hawakuyapenda maisha yao sana.

Hawakuogopa kifo.

12Hivyo furahi, ewe mbingu

na wote waishio humo!

Lakini ole kwa nchi na bahari,

kwa sababu Ibilisi ameshuka kwako.

Amejaa ghadhabu.

Anajua ana muda mchache.”

13Joka alipoona amekwisha tupwa chini duniani, alimkimbiza mwanamke aliyemzaa mtoto wa kiume.

14Lakini mwanamke alipewa mabawa mawili ya tai mkuu. Aliweza kuruka mpaka mahali palipoandaliwa kwa ajili yake jangwani. Huko atatunzwa kwa muda wa miaka mitatu na nusu akiwa mbali na joka.

15Kisha joka lilitoa maji kama mto kutoka katika kinywa chake kuelekea kwa mwanamke ili mafuriko yamchukue.

16Lakini nchi ilimsaidia mwanamke. Nchi ilifungua kichwa chake na kumeza mto uliotoka kwenye kinywa cha joka.

17Kisha joka lilimkasirikia sana mwanamke. Likaenda kufanya vita na watoto wake wengine. Watoto wa mwanamke ni wale wanaozitii amri za Mungu na wanayo kweli ambayo Yesu aliifundisha.

18Joka lilisimama ufukweni mwa bahari.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International