Ufunuo 16

Ufunuo 16

Bakuli Zilizojazwa Ghadhabu ya Mungu

1Kisha nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni. Ikiwaambia malaika saba, “Nendeni mkazimimine bakuli saba zenye ghadhabu ya Mungu juu ya dunia.”

2Malaika wa kwanza akaondoka. Akaimimina bakuli yake duniani. Ndipo wale wote waliokuwa na alama ya mnyama na walioiabudu sanamu yake wakapata majipu mabaya yenye maumivu makali.

3Malaika wa pili akaimimina bakuli yake baharini. Bahari ikawa kama damu ya mtu aliyekufa. Kila kitu kinachoishi baharini kikafa.

4Malaika wa tatu akaimimina bakuli yake juu ya mito na chemichemi za maji. Mito na chemichemi za maji zikawa damu.

5Ndipo nikasikia malaika wa maji akimwambia Mungu:

“Wewe ni yule uliyepo na uliyekuwepo daima.

Wewe ni Mtakatifu.

Uko sahihi kwa hukumu hizi ulizofanya.

6Watu walimwaga damu za

watakatifu na manabii wako.

Sasa umewapa watu hao damu ili wanywe.

Hiki ndicho wanachostahili.”

7Pia nikasikia madhabahu ikisema:

“Ndiyo, Bwana Mungu Mwenye Nguvu,

hukumu zako ni za kweli na za haki.”

8Malaika wa nne akaimimina bakuli yake juu ya jua. Jua lilipewa nguvu kuwachoma watu kwa moto.

9Watu wakaungua kwa joto kali. Wakalilaani jina la Mungu, mwenye mamlaka juu ya mapigo haya. Lakini walikataa kubadili mioyo na maisha yao, na kumpa Mungu utukufu.

10Malaika wa tano akaimimina bakuli lake juu ya kiti cha enzi cha mnyama. Giza likaufunika ufalme wa mnyama. Watu wakauma ndimi zao kwa sababu ya maumivu.

11Wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majipu waliyokuwa nayo. Lakini walikataa kubadili mioyo yao na kuyaacha maovu wanayotenda.

12Malaika wa sita akaimimina bakuli yake juu ya mto mkuu Frati. Maji yaliyokuwa mtoni yakakauka. Hili likaandaa njia kwa ajili ya watawala kutoka mashariki kuweza kupita.

13Kisha nikaona roho chafu tatu zilizoonekana kama vyura. Walitoka katika kinywa cha joka, kinywa cha mnyama, na kinywa cha nabii wa uongo.

14Roho hizi chafu ni roho za mapepo. Zina nguvu za kutenda miujiza. Nazo huenda kwa watawala wa ulimwengu wote na kuwakusanya kwa ajili ya mapigano siku ile Mungu Mkuu Mwenye Nguvu.[#16:14 Hapa inamaanisha miujiza ya uongo. Yaani matendo ya ajabu yanayofanywa kwa nguvu za mwovu.]

15“Sikilizeni! Nitakuja kama mwizi wakati msioutarajia. Heri watakaokuwa macho na waliovaa nguo zao. Hawatakwenda wakiwa uchi na kuona aibu watakapoonwa na watu.”

16Ndipo roho chafu zikawakusanya pamoja watawala pamoja mahali ambapo kwa Kiebrania panaitwa “Armagedoni”.

17Malaika wa saba akaimimina bakuli yake angani. Sauti kuu ikatoka hekaluni katika kiti cha enzi. Ikasema, “Imekwisha!”

18Kisha kukawa na mwako wa radi, kelele, ngurumo za radi na tetemeko kuu la nchi. Hili lilikuwa tetemeko kuu kuwahi kutokea tangu watu walipokuwepo duniani.

19Mji mkuu ukagawanyika vipande vitatu. Miji ya mataifa ikaharibiwa. Na Mungu hakusahau kuuadhibu Babeli Mkuu. Aliupa mji ule kikombe kilichojaa mvinyo wa ghadhabu yake kuu.

20Kila kisiwa kikatoweka na milima ikasawazika, hakukuwa milima yoyote tena.

21Mvua yenye mawe makubwa kutoka mbinguni ikawanyeshea watu. Mawe haya yalikuwa na uzito wa kilo 40 kila jiwe. Watu wakamlaani Mungu kwa sababu ya mvua hii ya mawe. Hali hiyo Ilitisha sana.[#16:21 Kilo 40 (au pauni 80), ni sawa na uzito wa 1.]

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International