The chat will start when you send the first message.
1Nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni. Malaika alikuwa na ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2Malaika alimkamata joka, nyoka wa zamani ambaye pia anajulikana kama Ibilisi au Shetani. Malaika akamfunga joka kwa minyororo kwa muda wa miaka elfu moja.
3Kisha akamtupia kuzimu na akaifunga. Malaika akamfungia joka kuzimu ili asiweze kuwadanganya watu wa dunia mpaka miaka elfu moja iishe. Baada ya miaka elfu moja joka lazima aachiwe huru kwa muda mfupi.
4Kisha nikaona viti vya enzi na watu wamevikalia. Hawa ni wale waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Na nikaona roho za wale waliouawa kwa sababu walikuwa waaminifu kwa kweli ya Yesu na ujumbe kutoka kwa Mungu. Hawakumwabudu mnyama wala sanamu yake. Hawakuipokea alama ya mnyama kwenye vipaji vya nyuso zao au mkononi mwao. Walifufuka na kutawala na Kristo kwa miaka elfu moja.
5(Wengine waliokufa hawakufufuka mpaka miaka elfu moja ilipokwisha.)
Huu ni ufufuo wa kwanza.
6Heri walifufuliwa mara ya kwanza. Ni watakatifu wa Mungu. Mauti ya pili haina nguvu juu yao. Watakuwa makuhani wa Mungu na Kristo. Watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.
7Miaka elfu moja itakapokwisha, Shetani ataachiwa huru kutoka kwenye gereza lake.
8Atatoka na kwenda kuwadanganya mataifa katika dunia yote, mataifa yajulikanayo kama Gogu na Magogu. Shetani atawakusanya watu kwa ajili ya vita. Kutakuwa watu wengi wasiohesabika kama mchanga katika ufukwe wa bahari.
9Nililiona jeshi la Shetani likitembea na kujikusanya ili kuizingira kambi ya watu wa Mungu na mji anaoupenda Mungu. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuliteketeza jeshi la Shetani.
10Na Shetani, yule aliyewadanganya watu hawa, alitupwa kwenye ziwa la moto pamoja na mnyama na nabii wa uongo. Watateseka kwa maumivu usiku na mchana milele na milele.
11Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe. Nikamwona aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha enzi. Dunia na anga vikamkimbia na kutoweka.
12Na nikaona wale waliokufa, wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti cha enzi na vitabu vilifunguliwa. Na kitabu cha uzima kilifunguliwa pia. Watu walihukumiwa kwa yale waliyotenda, kama yalivyoandikwa katika vitabu.
13Bahari ikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Mauti na kuzimu zikawaachia wafu waliokuwa ndani yake. Watu wote hawa walihukumiwa kutokana na matendo yao.
14Mauti na kuzimu vilitupwa kwenye ziwa la moto. Ziwa hili la moto ni mauti ya pili.
15Na yeyote ambaye jina lake halikuonekana limeandikwa kwenye kitabu cha uzima alitupwa kwenye ziwa la moto.