Warumi 5

Warumi 5

Kuhesabiwa Haki na Mungu

1Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa njia ya imani. Hivyo sote tuna amani pamoja na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.[#5:1 Au “uaminifu wake” au “uaminifu wa Yesu”.; #5:1 Baadhi ya nakala muhimu za Kiyunani zina “hebu sote tuwe”.]

2Kupitia imani yetu, Kristo ametufungulia mlango kuingia katika neema ya Mungu, tunayoifurahia sasa. Na tunashangilia sana kwa sababu ya tumaini tulilonalo la kushiriki utukufu wa Mungu.

3Na tunafurahia matatizo tunayoyapitia. Kwa nini? Kwa sababu tunajua kuwa mateso hutufundisha kuwa jasiri kipindi kigumu.

4Na ujasiri huu ni uthibitisho kuwa tuko imara. Na uthibitisho huu unatupa tumaini.

5Na tukiwa na tumaini hili, hatutakata tamaa kamwe. Tunajua hili kwa sababu Mungu ameumimina upendo wake na kuijaza mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu aliyetupa.

6Yote haya ni kweli kutokana na aliyoyafanya Kristo. Wakati sahihi ulipotimia, tukiwa hatuwezi kujisaidia wenyewe na tusioonyesha heshima yoyote kwa Mungu, yeye Kristo, alikufa kwa ajili yetu.

7Ni watu wachache walio tayari kufa ili kuokoa maisha ya mtu mwingine, hata kama mtu huyo ni mwema. Mtu anaweza kuwa radhi kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema sana.

8Lakini Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa bado ni wenye dhambi, na kwa hili Mungu akatuonyesha jinsi anavyotupenda sana.

9Tumehesabiwa haki mbele za Mungu kwa sababu ya sadaka ya damu ya Kristo. Hivyo kwa njia ya Kristo hakika tutaokolewa kutoka katika ghadhabu ya Mungu.

10Nina maana kuwa tulipokuwa bado adui wa Mungu, Yeye alifanya urafiki nasi kwa njia ya kifo cha Mwanaye. Kutokana na ukweli kwamba sasa tumekuwa rafiki wa Mungu, basi tunaweza kupata uhakika zaidi kwamba Baba atatuokoa kupitia uhai wa Mwanaye.

11Na si kuokolewa tu, bali pia, hata sasa tunafurahi kwa yale ambayo Mungu ametutendea kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ni kwa sababu ya Yesu sisi ni rafiki wa Mungu sasa.

Adamu na Kristo

12Dhambi ilikuja ulimwenguni kwa sababu ya kile alichofanya mtu mmoja. Na dhambi ikaleta kifo. Kwa sababu hiyo ni lazima watu wote wafe, kwa kuwa watu wote wametenda dhambi.

13Dhambi ilikuwepo ulimwenguni kabla ya Sheria ya Musa. Lakini Mungu hakutunza kumbukumbu ya dhambi ya watu wakati sheria haikuwepo.

14Lakini tangu wakati wa Adamu mpaka wakati wa Musa, mauti ilitawala juu ya kila mtu. Adamu alikufa kwa sababu alitenda dhambi kwa kutokutii amri ya Mungu. Lakini hata wale ambao hawakutenda dhambi kwa njia hiyo hiyo walipaswa kufa.

Hivyo mtu mmoja Adamu anaweza kufananishwa na Kristo, Yeye ambaye angekuja baadaye.

15Lakini kipawa cha Mungu hakifanani na dhambi ya Adamu. Watu wengi walikufa kwa sababu ya dhambi ya mtu huyo mmoja. Lakini neema waliyopokea watu kutoka kwa Mungu ilikuwa kuu zaidi. Wengi walikipokea kipawa cha Mungu cha uzima kwa neema ya huyu mtu mwingine, Yesu Kristo.

16Baada ya Adamu kutenda dhambi mara moja, alihukumiwa kuwa na hatia. Lakini kipawa cha Mungu ni tofauti. Kipawa chake cha bure kilikuja baada ya dhambi nyingi, nacho kinawafanya watu wahesabiwe haki mbele za Mungu.

17Mtu mmoja alitenda dhambi, hivyo kifo kikawatawala watu wote kwa sababu ya huyo mtu mmoja. Lakini sasa watu wengi wanaipokea neema ya Mungu iliyo nyingi sana na karama yake ya ajabu ya kufanyika wenye haki. Hakika watakuwa na uzima wa kweli na kutawala kupitia mtu mmoja, Yesu Kristo.

18Hivyo dhambi hiyo moja ya Adamu ilileta adhabu ya kifo kwa watu wote. Lakini kwa njia hiyo hiyo, Kristo alifanya kitu chema zaidi kilichowezesha watu kufanyika wenye haki mbele za Mungu. Na hicho huwaletea uzima wa kweli.

19Mtu mmoja hakumtiii Mungu na wengi wakafanyika wenye dhambi. Lakini kwa namna hiyo hiyo, mtu mmoja alipotii, wengi wamefanyika kuwa wenye haki.

20Baada ya sheria kuja, zilikuwepo njia nyingi za watu kufanya makosa. Lakini kadri watu walivyozidi kufanya dhambi, ndivyo Mungu alivyomimina zaidi neema yake.

21Hapo kale dhambi ilitumia kifo kututawala. Lakini sasa neema ya Mungu inatawala juu ya dhambi na kifo kwa sababu ya wema wake wenye uaminifu. Na hii inatuletea maisha ya milele kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International