Warumi 7

Warumi 7

Kielelezo Kutoka Katika Ndoa

1Ndugu zangu, ninyi nyote mnailewa sheria ya Musa. Hivyo kwa hakika mnafahamu kuwa sheria huwatawala watu wanapokuwa hai tu.

2Ni kama ambavyo sheria kuhusu ndoa inavyosema: ni lazima mwanamke abaki katika ndoa mume wake akiwa hai. Lakini mume wake akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa.

3Iwapo ataolewa na mwanaume mwingine, mume wake akiwa angali hai, sheria inasema kuwa ana hatia ya uzinzi. Lakini mumewe akifa, atakuwa amewekwa huru kutoka katika sheria ya ndoa. Hivyo akiolewa na mwanaume mwingine baada ya mumewe kufa, hatakuwa na hatia ya uzinzi.

4Kwa njia hiyo hiyo, kaka na dada zangu, mliwekwa huru kutoka katika sheria utu wenu wa zamani ulipokufa pamoja na Kristo. Sasa ninyi ni mali yake yeye yule aliyefufuliwa kutoka kwa wafu. Sote ni mali ya Kristo ili tutumike kwa ajili ya huduma kwa Mungu.

5Hapo zamani tulitawaliwa na udhaifu wetu wa kibinadamu. Sheria ilitufanya tutake kutenda dhambi. Na tamaa hizo za dhambi ziliitawala miili yetu, na yale tuliyofanya yalituletea mauti ya rohoni.

6Sasa, kama watu waliokufa, tuko huru kutoka katika sheria iliyotushikilia kama wafungwa. Hivyo hatumtumikii Mungu tena kwa jinsi ya zamani, kwa sheria zilizoandikwa. Sasa tunamtumikia Mungu kwa namna mpya, kwa Roho.

Dhambi na Sheria

7Mnaweza kudhani ninasema ya kwamba dhambi na sheria vinafanana. Sisemi hivyo. Lakini sheria ilikuwa njia pekee ya kunifundisha maana ya dhambi. Nisingeweza kujua kwamba ni kosa kutamani kitu kisichokuwa changu. Lakini sheria inasema, “Usitamani mali ya mtu mwingine.”[#Kut 20:17; Kum 5:21]

8Na dhambi kwa kutumia amri hiyo, ikanifanya nitamani kila kitu kisichokuwa changu. Hivyo dhambi ilikuja kwangu kutokana na amri hiyo. Lakini bila sheria, dhambi imekufa na haina nguvu.

9Kabla sijaijua sheria, nilikuwa hai. Lakini nilipoijua sheria, dhambi ikaanza kuishi ndani yangu,

10na hiyo ikawa na maana ya kifo kwangu. Amri ilikusudiwa kuleta uzima, lakini kwangu iliniletea kifo.

11Dhambi ilipata njia ya kunidanganya kwa kutumia amri ili nife.

12Hivyo, sheria ni takatifu na amri ni takatifu, sahihi na nzuri.

13Je! hii ina maana kuwa kitu ambacho ni kizuri kiliniletea kifo? Hapana, ni dhambi iliyoitumia amri nzuri ndiyo iliyoniletea kifo. Hii inaonesha kwa hakika kuwa dhambi ni dhambi. Dhambi inaweza kutumia amri iliyo nzuri na kuleta matokeo yanayoonesha ubaya wake mkubwa.

Vita ndani Yetu

14Tunafahamu kuwa sheria ni ya rohoni, lakini mimi si wa rohoni. Mimi ni mwanadamu hasa. Dhambi inanitawala kana kwamba mimi ni mtumwa wake.

15Sielewi ni kwa nini ninatenda jinsi ninavyotenda. Sitendi mema ninayotaka kuyatenda, bali ninatenda maovu ninayoyachukia.

16Na ikiwa ninatenda kile nisichotaka kutenda, inamaanisha kuwa ninakubali kuwa sheria ni njema.

17Lakini kwa hakika siyo mimi mwenyewe ninayetenda maovu. Bali dhambi inayokaa ndani yangu ndiyo inatenda hayo.

18Ndiyo, ninajua kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu, nina maana kuwa hakuna kitu chema kinachoishi ndani yangu kisichokuwa cha rohoni.

19Sitendi mema ninayotaka nitende. Ninatenda maovu nisiyotaka kutenda.

20Hivyo ikiwa ninatenda yale nisiyotaka kutenda, hakika si mimi ninayeyatenda hayo. Bali dhambi inayoishi ndani yangu ndiyo inayotenda.

21Hivyo nimejifunza hivi kuhusu sheria: Ninapotaka kutenda mema ambayo sheria inaamrisha, uovu unakuwa hapo hapo pamoja nami.

22Moyoni mwangu nafurahi kuifuata sheria ya Mungu.

23Lakini naiona “sheria” nyingine ikitenda kazi ndani yangu, nayo imo vitani dhidi ya sheria inayokubalika akilini mwangu. “Sheria” hii nyingine ni utawala wa dhambi inayonishinda na inanifanya kuwa mfungwa wake.

24Mimi ni mtu mwenye taabu kiasi gani! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu unaoniletea kifo?

25Namshukuru Mungu kwa wokovu wake kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo katika ufahamu wangu mimi ni mtumwa wa sheria ya Mungu, lakini katika udhaifu wangu wa kibinadamu mimi ni mtumwa wa sheria ya dhambi.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International