The chat will start when you send the first message.
1Yesu alitoka mtoni Yordani akiwa amejaa Roho Mtakatifu, akaongozwa na Roho mpaka jangwani.[#4:1 Luka kwa namna ya pekee, kama ilivyosemwa katika utangulizi, hupendelea sana kutaja kuhusika kwake Roho Mtakatifu katika matukio mengi maalumu ya Yesu. Na hata pale ambapo matukio hayo ni sambamba katika Injili zile tatu na ambapo Injili mbili za kwanza hazimtaji Roho Mtakatifu, Luka anamtaja: 4:1,14,18; 10:21; 11:13.]
2Huko alijaribiwa na Ibilisi kwa muda wa siku arubaini. Wakati huo wote hakula chochote, na baada ya siku hizo akasikia njaa.[#4:2 Tukio hilo linathibitisha au kudhihirisha uthabiti wake Yesu kuhusu kuambatana na matakwa ya Mungu kwa uaminifu. Siku arubaini zatukumbusha miaka arubaini Waisraeli waliyotumia jangwani.]
3Ndipo Ibilisi akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, amuru jiwe hili liwe mkate.”
4Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Mtu haishi kwa mkate tu.’”
5Kisha Ibilisi akamchukua hadi mahali pa juu, akamwonesha kwa mara moja falme zote za ulimwengu. Huyo Shetani akamwambia,
6“Nitakupa uwezo juu ya falme zote hizi na fahari zake, kwa maana nimepewa hivi vyote; nikitaka kumpa mtu ninaweza.
7Hivi vyote vitakuwa mali yako wewe, kama ukiniabudu.”
8Yesu akamjibu, “Imeandikwa:
‘Utamwabudu Bwana Mungu wako,
na kumtumikia yeye peke yake.’”
9Ibilisi akamchukua mpaka Yerusalemu, kwenye mnara wa hekalu, akamwambia, “Kama wewe ni Mwana wa Mungu, jitupe chini[#4:9 Lilikuwa kitovu cha ibada ya Wayahudi.]
10kwa maana imeandikwa:
‘Atawaamuru malaika wake wakulinde,’
11na tena,
‘Watakuchukua mikononi mwao,
usije ukajikwaa mguu kwenye jiwe.’”
12Lakini Yesu akamjibu, “Imeandikwa: ‘Usimjaribu Bwana Mungu wako.’”
13Ibilisi alipokwisha mjaribu kwa kila njia, akamwacha kwa muda.[#4:13 Tafsiri nyingine yamkini: Shetani anatokea tena katika simulizi la Luka 22:3.]
14Hapo Yesu alirudi Galilaya akiwa amejaa nguvu za Roho Mtakatifu, na habari zake zikaenea katika sehemu zote za jirani.
15Naye akawa anawafundisha watu katika masunagogi yao, akasifiwa na wote.[#4:15-44 Ilikuwa nyumba ya kukutania na ya ibada ya hadhara ya Wayahudi huko Palestina na nje ya Palestina ambapo waliishi Wayahudi. Katika ibada ya Sabato ambapo aweza kuitwa mtu yeyote Myahudi kuiongoza, mmoja alisimama, akasoma kwa sauti Maandiko ya A.K. kisha, kama desturi, akaketi na kuyaeleza.]
16Basi, Yesu alikwenda Nazareti, mahali alipolelewa, na siku ya Sabato, aliingia katika sunagogi kama ilivyokuwa desturi yake. Akasimama ili asome Maandiko Matakatifu kwa sauti.
17Akapokea kitabu cha nabii Isaya, akakifungua na akakuta mahali palipoandikwa:
18“Roho wa Bwana yu juu yangu,
kwani ameniweka wakfu
niwaletee maskini Habari Njema.
Amenituma niwatangazie mateka uhuru wao,
na vipofu watapata kuona tena;
amenituma niwakomboe wanaoonewa,
19na kutangaza mwaka wa neema ya Bwana.”
20Baada ya kusoma, akafunga kile kitabu, akampa mtumishi, kisha akaketi; watu wote wakamkodolea macho.[#4:20 Neno kwa neno: Vitabu vya wakati huo vilikuwa na umbo tofauti na vyetu; vilikuwa mviringomviringo na vya ngozi.]
21Naye akaanza kuwaambia, “Andiko hili mlilosikia limetimia leo.”[#4:21 Hapa, neno hili aghalabu lahusu wakati wa wokovu, ambao Yesu anawaletea watu. Taz Ebr 3:7-4:13. Katika Luka na pia katika Matendo, kukamilika kwa Maandiko Matakatifu kunatiliwa mkazo (Luka 2:11; 5:26; 13:32; 19:9; 23:43; Mate 3:7—4:13).]
22Wote wakavutiwa sana naye, wakastaajabia maneno mazuri aliyosema. Wakasema, “Je, huyu si mwana wa Yosefu?”
23Naye akawaambia, “Bila shaka mtaniambia msemo huu: ‘Mganga jiponye mwenyewe,’ na pia mtasema: ‘Yote tuliyosikia umeyafanya kule Kafarnaumu, yafanye pia hapa kijijini mwako.’”
24Akaendelea kusema, “Hakika nawaambieni, nabii hatambuliwi kijijini mwake.
25Lakini, sikilizeni! Kweli kulikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli nyakati za Elia. Wakati huo mvua iliacha kunyesha kwa muda wa miaka mitatu na nusu; kukawa na njaa kubwa katika nchi yote.
26Hata hivyo, Elia hakutumwa kwa mjane yeyote ila kwa mwanamke mjane wa Sarefathi katika Sidoni.
27Tena, katika nchi ya Israeli nyakati za Elisha kulikuwa na wenye ukoma wengi. Hata hivyo, hakuna yeyote aliyetakaswa ila tu Naamani mwenyeji wa Siria.”
28Wote waliokuwa katika lile sunagogi waliposikia hayo walikasirika sana.[#4:28 Kwa maana Yesu aligusia kwa maneno yake (25-27) kwamba wema wake Mungu si kwa ajili ya Waisraeli tu bali kwa ajili ya watu wa mataifa yote.]
29Wakasimama, wakamtoa nje ya mji wao uliokuwa umejengwa juu ya kilima, wakampeleka mpaka kwenye ukingo wa kilima hicho ili wamtupe chini.
30Lakini Yesu akapita katikati yao, akaenda zake.
31Kisha Yesu akashuka mpaka Kafarnaumu wilayani Galilaya, akawa anawafundisha watu siku ya Sabato.
32Wakastaajabia uwezo aliokuwa nao katika kufundisha.
33Na katika lile sunagogi kulikuwa na mtu aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu; akapiga ukelele wa kuziba masikio:[#4:33 Au: Watu wa nyakati hizo waliamini kwamba magonjwa mbalimbali yaliyopata watu kimwili na kiakili yalitokana na pepo wabaya. Hao pepo walifahamika kuwa nafsi wasio na mwili, ambao walikuwa maadui za watu na waasi wa Mungu. Yesu anakuja kuwafungua watu kutoka nguvu za pepo hao na uvamizi wa mkuu wa pepo yaani Shetani.]
34“Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninakufahamu wewe ni nani. Wewe ni Mtakatifu wa Mungu!”[#4:34 Maneno yanayodhihirisha uadui.]
35Yesu akamkemea huyo pepo akisema: “Nyamaza! Mtoke mtu huyu!” Basi, huyo pepo baada ya kumwangusha yule mtu chini, akamtoka bila kumdhuru hata kidogo.
36Watu wote wakashangaa, wakawa wanaambiana, “Hili ni jambo la ajabu, maana kwa uwezo na nguvu anawaamuru pepo wachafu watoke, nao wanatoka!”
37Habari za Yesu zikaenea mahali pote katika eneo lile.
38Yesu alitoka katika lile sunagogi, akaenda nyumbani kwa Simoni. Mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa na homa kali; wakamwomba amponye.[#4:38 Yaani nyumba ya Simoni Petro kule Kafarnaumu.]
39Yesu akaja akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, nayo ikamwacha. Yule mama akainuka mara, akawatumikia.
40Jua lilipokuwa linatua, wote waliokuwa na wagonjwa wao mbalimbali waliwaleta kwake; naye akaweka mikono yake juu ya kila mmoja wao, akawaponya wote.[#4:40 Yaani wakati ambapo Sabato na miiko yake ilimalizika na, watu walianza mara moja kuwabeba wagonjwa wao na kuwapeleka kwa Yesu, kwani wasingeruhusiwa kufanya hivyo siku ya Sabato.]
41Pepo waliwatoka watu wengi, wakapiga kelele wakisema: “Wewe ni Mwana wa Mungu!” Lakini Yesu akawakemea, wala hakuwaruhusu kusema, maana walijua kwamba yeye ndiye Kristo.[#4:41 Katika Injili tatu za kwanza zijulikanazo kama ‘sunoptiki’ kwa vile zinapatana sana katika muundo wa masimulizi yao, na hasa Injili ya Marko, Yesu anawakataza sio tu pepo bali hata watu wanaoponywa naye wasimseme hadharani kuwa yeye ni Mwana wa Mungu na Masiha. Kisa ni kwamba huenda alitaka kuepa wasimwekee fikira na hisia ambazo hazikupatana na malengo yake kama Masiha au Mkombozi ambaye si wa kisiasa, bali mwenye ujumbe wa Mungu wa kuwaokoa watu utumwani mwa dhambi. Yeye mwenyewe alikubali tu kuitwa hivyo pale alipoulizwa na kuhani mkuu muda mfupi tu kabla ya kusulubiwa kwake (Marko 14:61-62).]
42Kesho yake asubuhi, Yesu aliondoka akaenda mahali pa faragha. Watu wakawa wanamtafuta. Hao watu walipofika mahali alipokuwa, wakajaribu kumzuia ili asiondoke kwao.
43Lakini yeye akawaambia, “Ninapaswa kuhubiri Habari Njema za ufalme wa Mungu katika miji mingine pia, maana nilitumwa kwa ajili hiyo.”
44Akawa anahubiri katika masunagogi ya Yudea.[#4:44 Taz 1:5; hati nyingine za mkono zina Galilaya.]