The chat will start when you send the first message.
1*Lakini ndugu, sitaki, ninyi mkose kuyajua mambo ya Kiroho.
2Mnajua: Mlikuwa wamizimu, napo po pote, mlipoongozwa, mlipenda kuyafuata matambiko ya vinyago visivyosema.[#Hab. 2:18-19.]
3Kwa hiyo nawatambulisha, ya kuwa hakuna mwenye Roho ya Mungu anayeweza kusema: Yesu na awe ameapizwa! Tena hakuna anayeweza kusema: BWANA NI YESU! asipokuwa na Roho takatifu.[#Mar. 9:39; 1 Yoh. 4:2-3.]
4Kweli yako mapitano ya magawio, lakini Roho ni yule mmoja.[#Rom. 12:6; Ef. 4:4-7.]
5Tena yako mapitano ya utumishi, lakini Bwana ni yule mmoja.[#1 Kor. 12:28; Ef. 4:11.]
6Tena yako mapitano ya nguvu, lakini Mungu anayevitia vyote nguvu kwa watu wote ni yule mmoja.
7Lakini kila mtu hufunuliwa kipaji chake cha Roho, kwa kwamba wote wakionee upato.[#1 Kor. 14:26.]
8Kwani mmoja hupewa na Roho kusema ya werevu wa kweli, mwingine kusema ya utambuzi unaopatana na Roho yule yule.
9Mwingine hupewa kumtegemea Mungu kwa nguvu ya Roho yuleyule, mwingine hupewa magawio ya kuponya wagonjwa kwa nguvu ya Roho yule mmoja.
10Mwingine hupewa kutenda ya nguvu, mwingine ufumbuaji, mwingine kuyapambanua ya Kiroho, mwingine misemo migeni, mwingine kuieleza ile misemo.[#1 Kor. 14:5; Tume. 2:4.]
11Lakini haya yote huyatenda Roho yule mmoja akimgawia kila mmoja, kama anavyopenda.*[#1 Kor. 7:7; Rom. 12:3; Ef. 4:7.]
12Kwani ni kama vya mwili: ulio mmoja unavyo viungo vingi; tena viungo vyote vya mwili, ingawa ni vingi, ni mwili mmoja tu; vivyo hivyo naye Kristo.[#1 Kor. 10:17; 12:27.]
13Kwani kwa nguvu ya ile Roho moja tumebatiziwa sisi sote kuwa mwili mmoja, tukiwa Wayuda au Wagriki, tukiwa watumwa au waungwana; nasi sote tulinyweshwa Roho moja.[#Gal. 3:28.]
14Kwani nao mwili sio kiungo kimoja, ila vingi.[#1 Kor. 12:20.]
15Mguu ukisema: Kwa sababu si mkono, mimi si wa mwili, je? Kwa hiyo sio wa mwili?
16Nalo sikio likisema: Kwa sababu si jicho, mimi si la mwili je? Kwa hiyo silo la mwili?
17Mwili wote kama ungekuwa jicho, tungesikiaje? Kama wote ungekuwa sikio, tungenusaje?
18Lakini Mungu ameviweka viungo mwilini kila kimoja hapo, alipokitaka.
19Lakini vyote kama vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungepatikana wapi?
20Sasa viungo ni vingi, lakini mwili ni mmoja.[#1 Kor. 12:14.]
21Jicho haliwezi kuuambia mkono: Sikutumii; wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: Siwatumii ninyi.
22Lakini ni hivyo: vile viungo vya mwili, tunavyoviwazia kuwa vinyonge, hatumika kuliko vingine.
23Navyo, tunavyoviwazia kuwa vyenye soni, hupata heshima kuliko vingine; navyo visivyo vizuri hupambwa kuliko vingine.
24Maana vile vilivyo vizuri machoni petu havipambwi. Lakini Mungu ameuunganisha mwili, nacho kilichopunguka uzuri akakipatia heshima kuliko vingine.
25Maana mwilini msiwe na migawanyiko, ila viungo vipatane kutunzana kila kiungo na mwenziwe.
26Napo kiungo kimoja kinapoumia, basi, viungo vyote huumia pamoja nacho; napo kiungo kimoja kinapotukuzwa, basi, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.
27Lakini ninyi m mwili wake Kristo, tena m viungo kila mmoja mahali pake.[#Rom. 12:5; Ef. 5:30.]
28Wako, Mungu aliowawekea wateule: kwanza mitume, wa pili wafumbuaji, wa tatu wafunzi, kisha wenye nguvu, kisha wenye magawio ya kuponya wagonjwa nao watumikizi nao wenye kuongoza nao wenye misemo migeni.[#Ef. 4:11-12.]
29Wote ni mitume? Wote ni wafumbuaji? Wote ni wafunzi? Wote ni wenye nguvu?
30Wote huponya wagonjwa? Wote husema misemo migeni? Wote hufumbua?
31Jikazeni, mpate magawio yapitayo hayo! Nami nitawaonyesha njia iliyo nzuri kuzipita zote.[#1 Kor. 14:1.]