The chat will start when you send the first message.
1*Ijapo niseme misemo ya kimtu na ya kimalaika, nisipokuwa na upendo, ndimi upatu wenye milio au njuga yenye makelele.[#1 Kor. 14.]
2Ijapo niwe mwenye ufumbuaji, nikayajua mafumbo yote na utambuzi wote, hata nikawashinda wote kwa kumtegemea Mungu, nikaweza kuhamisha hata vilima, nisipokuwa na upendo, hakuna nilichokuwa.[#Mat. 7:22; 17:20.]
3Ijapo niwagawie maskini mali zangu zote, nikautoa nao mwili wangu, uunguzwe na moto, nisipokuwa na upendo, hakuna nifaacho.[#Mat. 6:2.]
4Upendo ni wenye uvumilivu na upole; upendo haujui wivu. Upendo haujikwezi, wala haujivuni;
5haukwazi, wala hauyatafuti yaliyo yake, wala hauchukiziki, wala hauyahesabu maovu.[#Mat. 18:21-22; Fil. 2:4,21.]
6Hauyafurahii mapotovu, ila huyafurahia yaliyo ya kweli.[#Rom. 12:9.]
7Hujitwika yote, huyategemea yote, huyangojea yote, huyavumilia yote.[#Fano. 10:12; Rom. 15:1.]
8Hapana, upendo unapokomea; kama ni ufumbuaji, utakoma; kama ni misemo, itanyamaza; kama ni utambuzi, utakoma.
9Kwani tunayoyatambua, ni fungu tu; nayo tunayoyafumbua, ni fungu tu;
10lakini matimilifu yatakapokuja, yale ya kifungufungu yatakoma.
11Nilipokuwa mtoto nalisema kitoto, nikayajua ya kitoto, nikayawaza ya kitoto. Lakini hapo nilipokuwa mtu mzima nimeyaacha yale ya kitoto.
12Maana sasa tunafanana kama tunaona mfano tu wa yale yasiyofumbuka bado; lakini siku ile tutayaona macho kwa macho. Sasa nayatambua fungu tu, lakini siku ile nitayatambua, kama nitakavyokuwa nimetambulika.[#4 Mose 12:8; 2 Kor. 5:7.]
13Sasa kusikokoma ndiko kumtegemea Mungu na kumngojea na kupenda, huku kutatu. Lakini kuliko kukubwa kukupita kwingine ndiko kupenda.*[#1 Tes. 1:3; 1 Yoh. 4:16.]