1 Wakorinto 14

Misemo migeni na ufumbuaji.

1Ukimbilieni upendo! Jikazeni, myapate ya Kiroho, kupita mengine, mweze kufumbua![#1 Kor. 12:10,31.]

2Kwani mwenye misemo migeni hasemi na watu, ila husema na Mungu. Kwani hapana amsikiaye, ila husema rohoni yasiyojulikana.[#Tume. 2:4.]

3Lakini mwenye kufumbua husema na watu akiwajenga na kuwaonya na kuwatuliza mioyo.

4Mwenye misemo migeni hujijenga mwenyewe tu; lakini mwenye kufumbua huwajenga wateule.

5Nataka, ninyi nyote mseme misemo migeni, lakini kupita hapo nataka, mfumbue. Kwani mwenye kufumbua ni mkubwa kuliko mwenye misemo migeni, isipokuwa aifumbue, wateule wakapata kujengwa.[#1 Kor. 12:10; 14:27-29; 4 Mose 11:29.]

6Lakini sasa, ndugu, kama ningekuja kwenu na kusema misemo migeni, ningewafaa nini, nisiposema nanyi nikiifunua au nikiitambulisha au nikiifumbua au nikiifundisha?[#1 Kor. 12:8.]

7Hivyo vingekuwa kama vyombo vinavyojililia tu pasipo roho, ikiwa zomari au zeze; milio isipotambulikana, yatajulikanaje yanayopigwa kwa zomari au kwa zeze?

8Tena ngoma isipolia na kusikilika, yuko nani atakayejitengeneza kwenda penye kondo?

9Vivyo hivyo nanyi mnaposema misemo migeni isiyojulikana, yale maneno yenu yatatambulikanaje? Kwani mtakuwa kama wanaojisemea tu na kupigia upepo.

10Misemo humu ulimwenguni ni mingi mno, lakini hakuna hata mmoja usiotambulika.

11Nisipoijua maana ya msemo, nitakuwa kama mjinga kwake yeye anayeusema, naye asemaye atakuwa mjinga kwangu mimi.

12Nanyi hivyo, mjikazavyo kuyapata ya Kiroho, yatafuteni yaleyale yanayowajenga wateule, myaenee![#1 Kor. 14:1-4.]

13Kwa hiyo mwenye misemo migeni aombe, apate hata kuifumbua![#1 Kor. 12:10.]

14Kwani nikiomba kwa ile misemo migeni, roho yangu huomba, lakini mawazo yangu hayamo.

15Basi, yafaayo ndiyo nini? Niombe rohoni, tena niombe na kuwaza; niimbe rohoni, tena niimbe na kuwaza.[#Ef. 5:19.]

16Maana ukimtukuza Mungu rohoni, kama yuko asiyeyajua matukuzo yako, atawezaje kuyaitikia na kusema Amin? Maana hajui, unayoyasema.

17Kweli wewe unatukuza vizuri, lakini mwingine hajengwi.

18Namtukuza Mungu, ya kuwa naisema ile misemo migeni kuwapita ninyi nyote.

19Lakini kwenye wateule kusema maneno matano tu na kuyawaza, kwamba niwafundishe hata wengine, kwanipendeza kuliko kusema maneno elfu kumi kwa hiyo misemo migeni.

20Ndugu, mawazo yenu yasiwe ya kitoto, ila uovu tu mfanane na vitoto vichanga! Lakini mawazo yenu sharti yawe ya watu wazima![#Ef. 4:14; Fil. 3:12,15.]

21Katika Maonyo imeandikwa:

Ukoo huu nitasema nao misemo migeni kwa midomo migeni,

lakini hata hivyo hawatanisikia; ndivyo, asemavyo Bwana.

22Kwa hiyo ile misemo migeni ni kielekezo, lakini si kwao wamtegemeao Bwana, ila kwao wakataao kumtegemea; lakini ufumbuaji nao ni kielekezo, lakini si kwao wakataao kumtegemea, ila kwao wamtegemeao.

23Kama wateule wote wanakusanyika pamoja, wote wakasema misemo migeni, tena pakiingia watu waliopumbaa au wasiomtegemea Bwana, je? Hawatasema: Mna wazimu?

24Lakini kama wote wanafumbua, tena pakiingia asiyemtegemea Bwana au aliyepumbaa ataonywa nao wote na kuumbuliwa nao wote.

25Hapo yaliyofichika moyoni mwake yanapofunuliwa, ndipo, atakapoanguka kifudifudi na kumtambikia Mungu na kuungama: Kweli Mungu yumo mwenu![#Yoh. 16:8.]

Misemo na mafumbuo.

26Ndugu, yafaayo ndiyo nini? Mnapokusanyika, kila mtu kama yuko na wimbo au fundisho au ufunuo au misemo migeni au mafumbuo yao, yote pia sharti yaje kujenga.[#1 Kor. 11:18,20; 12:8-10; Ef. 4:12.]

27Mtu akisema misemo migeni, basi, wawe kama wawili au watatu tu, wasipite hapo, nao waseme mmoja mmoja, kisha mmoja aifumbue.

28Lakini kama hayuko mwenye kufumbua, basi, wanyamaze penye wateule, ila waseme mioyoni na Mungu.

29Lakini wafumbuaji waseme wawili au watatu, nao wengine wasikilize tu, wayatambue.[#Tume. 17:11; 1 Tes. 5:21.]

30Lakini kama mwingine anayekaa anafunuliwa neno, wa kwanza na anyamaze.

31Kwani mwaweza wote kila mmoja kufumbua, wote wapate kujifunza, wao wote waonyeke.

32Nazo roho za wafumbuaji huwatii wafumbuaji.

33Kwani Mungu si Mungu wa uvurugo, ila ni Mungu wa utulivu.

Wanawake wanyamaze penye wateule.

34Kama ilivyo kwa wateule wote waliotakata, wanawake wanyamaze penye wateule! Kwani wao haiwapasi kusema, ila watii, kama Maonyo yanavyosema.[#1 Kor. 11:3; 1 Mose 3:16; Ef. 5:22; 1 Tim. 2:12; Tit. 2:5.]

35Lakini wanapotaka kujifunza neno, na wawaulize waume wao nyumbani! Kwani haifai kabisa, mwanamke akisema penye wateule.

36Au je? Neno la Mungu limetoka kwenu, au limewafikia ninyi peke yenu tu?

37Mtu akijiwazia kuwa mfumbuaji au mwenye Roho na ayatambue, ninayowaandikia, ya kuwa yameagizwa na Bwana![#1 Yoh. 4:6.]

38Lakini mtu asipoyajua, basi, na akae pasipo kuyajua!

39Kwa hiyo, ndugu zangu, jikazeni mpate kufumbua, nako kule kusema misemo migeni msikukataze!

40Lakini myafanye yote, kama ipasavyo, yaendelee vizuri![#Kol. 2:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania