1 Wakorinto 3

Maziwa na chakula.

1Nami ndugu, sikuweza kusema nanyi, kama m wenye Roho, m wenye miili tu, m vitoto vichanga katika mambo ya Kristo; kwa hivyo nimesema nanyi kitoto.[#Yoh. 16:12.]

2Nimewanyonyesha maziwa, sikuwalisha vyakula vigumu, maana hamjaviweza bado. Lakini hata sasa hamviwezi bado,[#Ebr. 5:12-13; 1 Petr. 2:2.]

3kwa sababu mngali bado wenye miili tu. Maana ukiwako kwenu wivu na ugomvi, basi, ninyi ham wenye miili tu? Huu mwenendo wenu sio wa kimtu?[#1 Kor. 1:10-11; 11:18.]

4Maana mmoja akisema: Mimi wa Paulo, na mwingine: Mimi wa Apolo, basi, ninyi ham wa kimtu?[#1 Kor. 1:12.]

Kupanda na kunywesha.

5Apolo ni nani? Paulo ni nani? Tu watumishi waliowafundisha kumtegemea Bwana, kila mmoja wetu, kama Bwana alivyompa:[#Tume. 18:24,27.]

6mimi nilipanda, Apolo akanywesha, lakini Mungu ndiye aliyeotesha.[#Tume. 18:1-4,11.]

7Kwa hiyo apandeye siye, wala anyweshaye siye, ila Mungu aoteshaye ndiye.

8Lakini apandaye naye anyweshaye sisi tu wamoja, lakini tutapata kila mmoja wake mshahara wa masumbuko yake mwenyewe.[#1 Kor. 4:5.]

9Maana sisi tunasaidiana kazi na Mungu, ninyi m shamba lake Mungu, tena m jengo lake Mungu.[#Mat. 13:3-9; Ef. 2:20.]

Msingi wa Mungu.

10Kwa werevu wa kweli, niliogawiwa na Mungu, mimi niliweka msingi kama fundi aliye mwenye ubingwa wa jengo; lakini mwingine anajenga juu yake. Lakini kila aangalie, jinsi anavyojenga juu yake![#1 Kor. 15:10.]

11*Kwani hakuna anayeweza kuweka msingi mwingine pasipo ule uliokwisha kuwekwa, ulio Yesu Kristo.[#1 Petr. 2:4-6.]

12Lakini mtu akijenga juu ya msingi huo kama dhahabu au fedha au mawe yenye bei kubwa au miti au nyasi au mabua,

13basi, kila mtu kazi yake itatokea waziwazi. Siku ile itaipambanua, maana itafunuliwa kwa kuunguzwa na moto; ni ule moto utakaoumbua, kazi ya kila mtu ilivyo.[#1 Kor. 4:5.]

14Jengo la mtu, alilolijenga juu yake likikaa, atapokea mshahara wake;

15kama jengo la mtu linateketea, atapotelewa nalo, lakini mwenyewe ataokolewa, lakini itakuwa kama kuokolewa motoni.

Nyumba ya Mungu.

16Hamjui, ya kuwa ninyi m nyumba ya Mungu, ya kuwa Roho wa Mungu hukaa ndani yenu?[#1 Kor. 6:19; 2 Kor. 6:16.]

17Mtu akiiangamiza nyumba yake Mungu, Mungu atamwangamiza yeye. Maana nyumba yake Mungu ni takatifu, ndiyo ninyi.

18Mtu asijidanganye! Ikiwa mtu wa kwenu anajiwazia kuwa mwenye werevu wa kweli katika ulimwengu huu, sharti apumbae, apate kuwa mwerevu wa kweli![#Ufu. 3:17-18.]

19Kwani huo werevu wa ulimwengu huu ni upumbavu kwa Mungu, maana imeandikwa:

Wenye ubingwa huwanasa katika werevu wao mbaya.

20Na tena:

Bwana huyatambua mawazo ya wenye werevu kuwa ya bure.

21Kwa hiyo mtu asijivune kwa wenziwe! Kwa maana yote ni yenu,

22akiwa Paulo au Apolo, akiwa Kefa, au ukiwa ulimwengu, kukiwa kuishi au kufa, yakiwa yaliyopo au yatakayokuwapo, yote ni yenu.

23Lakini ninyi m wake Kristo, naye Kristo ni wake Mungu.*[#1 Kor. 11:3.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania