1 Wakorinto 5

Kumtenga mgoni.

1Po pote panasikilika, ya kwamba kwenu uko ugoni; tena ugoni ulio hivyo hata kwa wamizimu hauko, mtu akiwa na mke wa baba yake.[#3 Mose 18:7-8.]

2Nanyi mnajitutumua, hamkusikitika hata kidogo. Je? Aliyekifanyiza kitendo hicho ameondolewa kati yenu?

3Hata nisipokuwako kwenu na mwili wangu, lakini moyo uko kwenu. Hivyo, kama niko kwenu, nimekwisha kumhukumu yule aliyekitenda kibaya kilicho hivyo:[#Kol. 2:5.]

4katika Jina la Bwana Yesu kusanyikeni ninyi na roho yangu pamoja na nguvu ya Bwana wetu Yesu![#Mat. 16:19; 18:18; 2 Kor. 13:10.]

5Kisha yule mtu aliye hivyo mmtoe na kumpa Satani, mwili wake uangamizwe, roho yake ipate kuokoka, siku ile ya Bwana itakapotimia.[#1 Kor. 11:32; 1 Tim. 1:20.]

6Majivuno yenu si mema. Hamjui, ya kuwa chachu kidogo hulichachusha donge lote?[#Gal. 5:9.]

7Iondoeni kabisa ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya kwa hivyo, mlivyo pasipo chachu!

*Kwani nasi tumechinjiwa kondoo wetu wa Pasaka, ndiye Kristo.

8Kwa hiyo tuile sikukuu yetu pasipo chachu ya kale wala chachu yenye uovu na ubaya, tuyapate yale yasiyochachwa, ndiyo mioyo ing'aayo iliyo yenye ukweli.*

9Naliwaandikia ninyi katika barua yangu kwa kwamba: Msichanganyike na wagoni![#Mat. 18:17; 2 Tes. 3:14.]

10Hapo sikuwasema wagoni wa ulimwengu huu au wenye choyo na wanyang'anyi au wenye kutambikia mizimu. Kama vingekuwa hivyo, ingewapasa kutoka ulimwenguni.

11Lakini hapo nimewaandikia, msichanganyike na mtu aitwaye ndugu, akiwa mgoni au mwenye choyo au mtambikia mizimu au mwenye matusi au mlevi au mnyang'anyi; basi, ndugu aliye hivyo msile naye![#2 Tes. 3:6; Tit. 3:10; 2 Yoh. 10.]

12Kwani nina jambo gani nao walioko nje, niwaumbue? Nanyi si kazi yenu kuwaumbua hao, mlionao?[#Mar. 4:11.]

13Walioko nje Mungu ndiye atakayewaumbua. Mwondoeni yule mbaya, atoke katikati yenu ninyi![#5 Mose 13:5.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania